Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-05 19:55:54    
Serikali ya China yasaidia viwanda vidogo kupata mitaji

cri

Tokea miaka miwili iliyopita, kutokana na uungaji mkono wa idara husika ya serikali, viwanda vidogo vilivyoko kwenye baadhi ya sehemu za hapa China, sasa vinaweza kupewa mikopo midogo bila kuweka rehani, isipokuwa unaangaliwa uwezo wake wa kurudisha fedha za mikopo, hatua ambayo inaleta nafasi na nguvu ya maendeleo kwa viwanda vidogo vyenye mitaji midogo.

Bw. Li Ronghua na mkewe waliokuwa wanafanya vibarua mkoani Zhejiang, kusini mwa China, mwaka jana walianzisha kiwanda cha kushughulikia mbao huko kwao, lakini muda mfupi baadaye kiwanda chao kilikumbwa na tatizo kubwa la upungufu wa fedha. Hali kadhalika, Bw. Chen Zhigang, mkazi wa mji wa Baotou, mkoa wa Mongolia ya ndani ulioko sehemu ya kaskazini magharibi ya China, aliyehitimu masomo ya chuo kikuu mwaka huu na kujiajiri kwa kufungua duka la kukarabati kompyuta, alikabiliwa na tatizo hilohilo la upungufu wa fedha. Wakati watu hao walipokuwa hawana la kufanya, walipewa mikopo na benki za biashara za huko. Kuhusu mambo hayo, kiongozi wa duka la kukarabati kompyuta la Junxia mjini Baotou Bw. Chen Zhigang alisema,

"Nilifurahi sana nilipopata mkopo wa Yuan elfu 10, kwa kuwa nilibanwa na tatizo kubwa la upungufu wa fedha. Hivi sasa si rahisi kukopeshwa Yuan elfu 10 hata kutoka kwa jamaa."

Shughuli za kukarabati kompyuta zinazofanywa na Bw. Chen Zhigang zinaendeshwa vizuri sana, pamoja na kuwa na ongezeko la wateja, pia alitaka kununua vitendea kazi na kuajiri wafanyakazi wengine, fedha alizokuwa nazo wakati anafungua duka lake, zilikuwa zinatosha tu kuendesha shughuli za biashara za kila siku, na alikuwa hana fedha kwa ajili ya kupanua biashara yake. Na mfanyabiashara wa mbao Bw. Li Ronghua pia alikabiliwa shida kama hiyo, hata alifikia hali ya kushindwa kununua malighafi kutokana na upungufu wa fedha. Hivyo kupata mtaji kulikuwa ni shida kubwa iliyowasumbua katika uendeshaji shughuli za biashara. Ingawa watu hao wawili walikuwa na wazo la kukopa fedha kutoka benki, lakini mmoja ndio alikuwa amehitimu masomo yake katika siku za karibuni, na mwingine alikuwa ni mkulima kibarua aliyeanzisha kiwanda sehemu ya ugenini, ilikuwa ni vigumu sana kwao kupata mikopo kutoka benki. Wakati waliposhindwa kupata utatuzi wa matatizo yao waliona tangazo moja ambalo liliwapa matumaini. Bw. Chen Zhigang alipoeleza hali yake baada ya kuona tangazo hilo alisema,

"Mkopo mdogo unatolewa kwa mteja ndani ya siku 3 bila kutakiwa kuwekwa dhamana. Nilipofikiri kuhusu uhalisi wake, niliona kuwa si rahisi kuwa haraka namna hii, kwa hiyo niliamua kupiga simu nikitaka kujaribu."

Baada ya kuwasiliana na benki, ombi la Bw. Chen Zhigang lilikubaliwa na benki kwa haraka. Baada ya kupata mkopo na kutatua matatizo yake kazini, pato la duka lake la kukarabati kompyuta liliongezeka maradufu. Naye Bw. Li Ronghua aliyeanzisha kiwanda cha kushughulikia mbao mkoani Zhejiang, pia alipata mkopo wa Yuan elfu 50, ambazo alizitumia kununua mali-ghafi ya mbao.

Kwa kawaida kiwanda kinapotoa ombi la kutaka mkopo kutoka benki, si tu kuwa benki inakagua sifa zake, bali pia kiwanda kinatakiwa kuweka rehani, ndipo benki inatoa mkopo kwa kiwanda. Kwa kuwa si rahisi kukadiria thamani ya sifa ya kiwanda, na kutokana na kiwanda kuwa na cha mali kidogo, hivyo ni vigumu kwa viwanda vidogo kutimiza masharti ya benki ili kupata mikopo. Kuhusu suala hilo, tokea mwaka jana kutokana na uungaji mkono wa kamati ya maendeleo na mageuzi ya taifa na kamati ya usimamizi wa sekta ya benki ya China, aina za mikopo midogo kwa viwanda vidogo ilianza kutolewa katika baadhi ya sehemu. Aina hizo za mikopo hazijali sana kama kuna mali iliyowekwa rehani, kinachozingatiwa zaidi ni uwezo wa mwombaji kurudisha fedha za mkopo. Habari zinasema hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Juni mwaka 2006, thamani ya mikopo iliyotolewa na benki kubwa za China kwa viwanda karibu elfu 780 ilifikia Yuan trilioni 2.64.

Bw. Tan Bo wa benki ya maendeleo ya taifa ya China alisema, Bw, Chen Zhigang na Bw. Li Ronghua ni wateja wa benki waliopewa mikopo midogo. Alipoeleza umaalumu wa aina hiyo ya mikopo, alisema,

"Kwanza ni tofauti ya makundi ya waombaji mikopo, husan watu wanaojiajiri, wakulima au wenye viwanda vidogo. Pili, masharti ya utoaji mikopo yanaendana na kiasi cha thamani ya mikopo, mikopo ya aina hiyo ni midogo inayoanzia Yuan elfu kadhaa hadi Yuan elfu kumi kadhaa, benki haijali sana mali inayowekwa rehani, isipokuwa inazingatia zaidi uwezo wa mkopaji katika kurudisha mkopo."

Viwanda vidogo ni moja ya sehemu muhimu ya uchumi wa taifa, maendeleo ya viwanda vidogo yanahusiana na familia nyingi za watu na kuhusika na maendeleo ya taifa na maisha ya watu. Hivi sasa serikali ya China inahimiza utoaji mikopo ya kibiashara kwa viwanda vidogo, bila shaka ni nafasi nzuri kwa watu wanaotaka kuanzisha shughuli za kibiashara na viwanda na wenye ukosefu wa mitaji. Benki zinazoanzisha utoaji huduma ya mikopo kwa viwanda vidogo pia zimefanya mageuzi na marekebisho mengi kuliko zamani. Benki za biashara za mji wa Baotou ulioko sehemu ya kaskazini mwa China zimebuni mpango wa utoaji huduma kwa viwanda vidogo, licha ya hayo zimeanzisha ofisi ya meneja wa huduma kwa kufanya shughuli za ukaguzi wa sifa za viwanda na kufanya uchunguzi husika. Baada ya kukamilisha uchunguzi kuhusu wateja, wafanyakazi wa idara ya mikopo midogo wanafungua faili la mikopo, na kutoa majibu haraka kwa wateja wanaotoa maombi ya mikopo.

Mkuu wa benki ya biashara ya mji wa Baotou Bw. Li Zhenxi alisema,

"Hapo zamani wafanyabiashara wadogo walikuwa hawawezi kupata mikopo ya benki, baada ya sisi kuweka lengo la kutoa huduma kwa watu walioanzisha viwanda au kampuni ndogo, tumeajiri mameneja wengi wa idara ya wateja ili kutoa huduma nzuri kwa watu hao. Kauli yetu ni kuwa hakuna mteja mbaya, isipokuwa benki inapata matatizo kama haikufanya kazi yake vizuri. Endapo tunatoa huduma nzuri kwa viwanda vidogo na kuwasaidia kupata mikopo, nafikiri kazi zetu zitapiga hatua kubwa za maendeleo."

Katika muda wa zaidi ya mwaka mmoja uliopita, benki za biashara za sehemu mbalimbali zilifanya utafiti mwingi, ambapo mabadiliko mengi ya kuvutia yalitokea. Msaidizi wa mwenyekiti wa kamati ya usimamizi ya sekta ya benki Bw. Wang Zhaoxing alipoeleza sababu ya kubuni sera za utoaji mikopo kwa viwanda vidogo alisema, " uamuzi wa Kamati ya usimamizi ya sekta ya benki kuanzisha utoaji mikopo kwa viwanda vidogo, unachangia kuanzisha jamii yenye kupata maendeleo mwafaka ya kiuchumi, na kuanzisha mazingira bora kwa utatuzi wa tatizo la ukosefu wa mitaji na maendeleo ya viwanda vidogo.

Habari zinasema hivi sasa zaidi ya mikoa 10 nchini China imeanzisha shughuli za utoaji mikopo kwa viwanda vidogo. Inatarajiwa kuwa shughuli hizo zitaendelezwa kwa haraka katika nchi nzima.

Idhaa ya Kiswahili 2006-12-05