Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-05 22:04:38    
Msikilizaji wetu Mutanda Ayub sharif azungumzia safari yake ya China

cri

Sherehe za miaka 65 ya CRI

Hii siku ilikuwa ya kila mtu aliyekuwa amealikwa kuhudhuria akiwa amevaa mavazi rasmi. Na kwa muda mrefu mimi nilikuwa ninavaa mavazi ya kawaida. Sijui ningefanyaje kama asingekuwa Bw. Du aliyeamua kunizawadi nguo nilizotumia kama mavasi rasmi.

Hapa China watu wanaheshimu muda, ilipofika saa mbili ilitupasa tuwe tayari kwenye gari kuelekea chumba cha sherehe ambacho kilikuwa karibu tu na Hoteli ya Minzu. Kwa kweli furaha niliyokuwa nayo ilinifanya nisahau kifungua kinywa. Nilikumbuka tu! Kama tumeshafika kule katika ukumbi wa muziki, nilishangaa kuona maandalizi yenyewe, waandishi wa habari, watangazaji wa idhaa mbalimbali nchini China wote walikuwa tayari wamejaa na wamekaa kwenye nafasi zao wakiwa wamevalia rasmi. Tuliweza kufanya mazoezi kidogo huku vinanda vikitoa sauti ya kupendeza nyororo ya kumtoa nyoka pangoni. Kwa kweli hii ilikuwa nafasi ya heshima, yaani wahariri, washindi wa tuzo maalumu, wakuu wa idhaa mbalimbali akiwemo Mkuu wa KBC kutoka Kenya Bw. Waweru wote walikuwepo.

Ndani ya jengo hilo kulikuwa na mapambo ya rangi tofauti kama vile ya manjano, nyekundu, kijani kibichi na meupe pepe. Yote yalikuwa yanavutia sana. Muda mfupi baadaye washindi wa tuzo maalumu waliitwa jukwaani, na mimi nikiwa mmoja wao niliweza kupokea cheti cha ushindi pamoja na tuzo maalumu ambayo nitaweza kuhifadhi na kujivunia, hata kujigamba kuwa niliipokea katika sherehe ya kimataifa ya nchi ya China.

Na baada ya hapo tulipanda kwenye gari la Radio China kimataifa, hata bila kujua tunaelekea wapi kwa sababu hatujui lugha ya kichina tulikuwa hatuelewi kinaongewa nini, lakini kumbe tulikuwa tunaelekea kwenye maakuli. Kwa kweli huko tulikula vyakula vinono sana. Tulikuwa na wenzetu kutoka Amerika, Brazil, China, Tanzania, Niger, Sri Lanka, Canada, Japan na sehemu nyingine, tulikuwa tunakula pamoja, pia hata viongozi wakuu wa Radio China kimataifa na viongozi wengine wa China pia walikuwepo. Na baada ya kumaliza chakula na burudani nyingine tulikwenda kulala kwenye vyumba maalum.

Pamoja na kuwa kwa sasa mjini Beijing kuna baridi, Tuliweza kupewa makoti na wenyeji wetu. Kina ambacho kitanifanya nikumbuke sana ziara hii ni kwenye ukumbi wa hotel ya Shangrila, kule Nilifurahi sana kujumuika na viongozi wa radio China, huku tulikula na kupata vinywaji pamoja.

Vilevile wakati ngoma moja tuliyoandaliwa ikiwa inachezwa kutokana na furaha kubwa niliyokuwa nayo, nilishindwa kuvumilia nikajikuta nimefika jukwaani na mimi nikijumuika na wacheza ngoma, hapa naweza kusema nilikosa adabu lakini nilishindwa kujizuia kutokana na kufurahia ukarimu wa wenyeji wangu

Idhaa ya Kiswahili 2006-12-05