Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-06 18:33:42    
China yaweka mkazo katika kuboresha mazingira ya watoto wa wakulima wanaofanya kazi mijini kupata elimu

cri
Uchumi wa China umedumisha ongezeko la kasi katika miaka 20 iliyopita, na kutokana na utandawazi wa miji na viwanda, watu wengi vijijini wanatafuta ajira katika miji mikubwa, lakini wanakabiliwa na matatizo mbalimbali: Je watoto wa watu hao watapata elimu kwa njia gani? Na ni vipi wanaweza kuishi katika mazingira mazuri?

Katika miaka ya hivi karibuni, shule zinazowahudumia watoto wa wakulima wanaofanya kazi mijini zimeanzishwa katika miji kadhaa nchini China. Baadhi yao zilianzishwa na serikali, na nyingine zilianzishwa na watu binafsi. Lakini baadhi ya shule hizo zimekumbwa na matatizo ya kutokuwa na fedha za kutosha na walimu, hali ambayo imezifanya shule hizo zisiweze kutoa huduma bora. Ili kuwa na mazingira mazuri ya elimu kwa watoto wa wakulima wanaofanya kazi mijini, sehemu mbalimbali za China zinafanya ukaguzi kwa shule hizo, na kupanga mpango wa kusimamisha shule zisizofikia kiwango cha taifa. Msemaji wa Wizara ya elimu ya China Bw. Wang Xuming alipohojiwa na waandishi wa habari alisema, China inapaswa kufanya usimamizi kwa mujibu wa kiwango cha taifa. Anasema

"Inapaswa kuondoa shule zisizofikia kiwango cha taifa, na kuweka mipango mwafaka kwa ajili ya watoto wa wakulima wanaofanya kazi mijini ambao wanasoma kwenye shule hizo, na kusifu shule zinazotoa huduma bora na kuziunga mkono."

Bw. Wang Xuming alisema Serikali itaziwekea shule zinazowahudumia watoto wa wakulima wanaoishi mijini kwenye utaratibu wa pamoja wa usimamizi, na kutoa misaada na uelekezaji kwa shule zinazofikia kiwango cha taifa

Idara za elimu za sehemu mbalimbali za China zimesema, wanafunzi wa shule zitakazofungwa watawekwa kwenye shule za kawaida. Pia wameeleza bayana kuwa, watoto wa wakulima wanaoishi mijini wana haki ya kupata elimu kama wanafunzi wengine, na shule hizo haziwezi kukiuka sheria za taifa, na kutoza gharama nyingine.

Ji Man mwenye umri wa miaka 12 anatoka mkoa wa Henan, katikati ya China. Alikuja Beijing pamoja na wazazi wake, na kupelekwa kusoma kwenye shule ya msingi inayowahudumia watoto wa wakulima. Mwezi Septemba mwaka huu, alianza kusoma kwenye shule ya kawaida. Alisema mazingira ya shule hiyo mpya ni mazuri kuliko shule alizosoma zamani. Anasema:

"kwenye shule nilizosoma zamani hakuna uwanja wa michezo, na tulipaswa kukaa darasani wakati wa kipindi cha michezo. Na walimu walipaswa kufundisha masomo mengi. Hivi sasa uwanja wa michezo kwenye shule ninakosoma ni mkubwa, tunafurahia kuweza kufanya mazoezi ya michezo uwanjani."

Kuna migongano mikubwa kuhusu hatua za kuanzisha shule zinazowahudumia watoto wa wakulima wanaofanya kazi mijini. Kwani wakulima wanaofanya kazi mijini wana wasiwasi mkubwa kuwa kama shule hizo zinaweza kuwatendea kwa haki watoto wao, pia wanaona kuwa ada za shule za serikali ni kubwa. Hivi sasa sehemu mbalimbali za China zinachukua hatua mbalimbali ili kuondoa matatizo hayo. Kwa mfano, eneo la Haidian la Beijing limetumia RMB Yuan milioni 13 katika kupanua na kuongeza viti na meza za shule za serikali, ili kuwapokea watoto wa wakulima wanaofanya kazi mijini. Katika mji wa Wuxi, mkoani Jiangsu, serikali ya mji huo inawawezesha watoto wa wakulima kujiandikisha kwa pamoja na wanafunzi wenyeji, na kulipa ada sawasawa, na kusoma kwenye shule zilizoko karibu zaidi na nyumbani kwao. Naibu mkuu wa Idara ya elimu ya Wuxi Bw. Zhang Yizhong alimwambia mwandishi wa habari kuwa, watoto wa wakulima wanaosoma mijini wana haki ya kupata elimu kama wanafunzi wenyeji wa Wuxi. Bw. Zhang anasema:

"Hapa Wuxi, watoto wa wakulima wanaofanya kazi mijini wanasoma kwa pamoja na wanafunzi wenyeji, na wanaweza kuishi na kupata maendeleo kama wanafunzi wenyeji."

Aidha sehemu mbalimbali za China zinaweka sera za kutoa misaada kwa shule zinazowahudumia watoto wa wakulima wanaofanya kazi mijini. Mkoani Zhejiang serikali ya huko ilitoa misaada kujenga majengo mapya, na kukodisha nyumba kwa gharama chini, na kuziwezesha shule nyingi zinazowahudumia watoto wa wakulima wanaofanya kazi mijini kufikia kiwango cha taifa, na kutatua tatizo la kupata elimu kwa watoto zaidi ya laki 2. Mkuu wa shule inayowahudumia watoto wa wakulima wanaofanya kazi mijini wa wilaya ya Yuhuan ya mkoa Zhejiang Bw. Weng Lixin alisema, katika majira ya Spring mwaka huu wakati alipokuwa na wasiwasi kutokana na ubovu wa jengo la shule yake, Idara ya elimu ya huko ilimsaidia kutafuta jengo jipya la shule na kuondoa tatizo lake. Bw. Weng Lixin alisema:

"Si rahisi kutafuta jengo zuri la shule, hususan katika wilaya ya Yuhuan ambayo gharama zake ni kubwa."

Msemaji wa Wizara ya elimu ya China Bw. Wang Xuming alisema, China itahakikisha watoto wote wa wakulima wanaofanya kazi mijini kupata elimu kadiri iwezekanavyo na kuanzisha na kufanya marekebisho kwa shule zinazowahudumia watoto wa wakulima hao. Wataalamu wanaohusika wamesema kuwa kufanya usimamizi wa shule zinazowahudumia watoto wa wakulima wanaofanya kazi mijini kunaweka mazingira mazuri kwa watoto wa wakulima hao kupata elimu, na kusaidia wakue kwa afya nzuri. Lakini ili kutatua matatizo ya kusoma shuleni kwa watoto wa wakulima wanaofanya kazi mijini, inapaswa kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo kutoa mazingira ya haki ya elimu, walimu wanapaswa kuzingatia umaalum wa watoto hao, kuheshimu uzoefu wao ya maisha, na kutoa mipango ya kutoa mafunzo kutokana na umaalum wao. Wakati huo huo inapaswa kuwasaidia kuanzisha uhusiano wenye masikilizano kati yao na wanafunzi wengine, ili waweze kujizoeza mapema na mazingira ya shule. Ni hadi hatua hizo zitakapochukuliwa, ndipo watoto wa wakulima wanaofanya kazi mijini watakapoweza kuinua sifa yao wenyewe.

Idhaa ya Kiswahili 2006-12-06