Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-07 20:11:16    
Bibi Katysha anayefundisha lugha ya Kirussia nchini China

cri

Bi. Katysha mwenye umri wa miaka 24 hutoka Russia, hivi sasa anafundisha lugha ya Kirussia katika chuo kimoja cha ualimu mjini Hegang, mkoani Heilongjiang, kaskazini mashariki mwa China. Kutokana na mradi wa kubadilishana walimu kati ya China na Russia, Bi. Katysha alikuja China kutoka maskani yake iliyopo mkoa wa mashariki ya mbali, nchini Russia. Je msichana huyo anaendelea vipi na maisha yake nchini China? Mwandishi wetu wa habari alimtembelea hivi karibuni.

Bi. Katysha mwenye macho makubwa na nywele ndefu zenye rangi ya dhahabu, ni msichana mrembo. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, licha ya hali ya hewa inayofanana na ya kwao, mji wa Hegang unatofautiana na Russia katika mambo mengi. Lakini anaupenda mji huo kutokana na wakazi wake wenye ukarimu mkubwa. Alisema "Naupenda sana mji wa Hegang, mji huu ni mzuri sana, nafurahia kuja hapa. Wakazi wa huku ni wakarimu sana, naridhika na kazi na maisha katika mji huu."

Katysha anatoka mji wa Birobidzan uliopo kusini mashariki mwa Russia. Mji huo na mji wa Hegang ipo katika kando mbili za mto Heilongjiang. Mwaka 1999 miji hiyo miwili ilianzisha uhusiano wa kirafiki.

Hapo awali Bi. Katysha alikuwa amevutiwa na China. Alipokuwa na umri wa miaka 18, Mchina mmoja ambaye ni rafiki wa baba yake alipotembelea familia yake, alimwelezea historia na utamaduni wa China, na Katysha alivutiwa sana na maelezo hayo.

Baadaye alianza kujifunza Kichina kutoka kwa Mchina rafiki wa baba yake, na alipata jina la Kichina liitwalo Hong, maana yake ni upinde wa mvua, kwa vile anataka kujenga daraja la mawasiliano ya utamaduni kati ya Russia na China kama ulivyo upinde wa mvua angani.

Darasani mwalimu Katysha anawasiliana na wanafunzi wake Wachina kwa lugha ya Kichina. Wanafunzi wake ni vijana wenye umri unaofanana naye, kwa hiyo hakuna pengo kati ya mwalimu Katysha na wanafunzi. Ingawa ilikuwa imepita mwaka mmoja tu tangu Katysha aanze kufanya kazi ya ualimu nchini China, wanafunzi wake wanampenda sana. Mwanafunzi mmoja aitwaye Guan Yu alisema, "Hakuna pengo la mawasiliano kati yetu. Anapenda kutuelezea hali kuhusu maskani yake na mambo mbalimbali yaliyotokea katika nchi yake. Pia amempa kila mwanafunzi jina la Kirussia, anatuita kwa majina ya Kirussia, huku tunamwita kwa jina lake la Kichina."

Mwalimu Katysha anapenda kuwafundisha wanafunzi wake lugha ya Kirussia katika mazingira halisi ya maisha. Kwa mfano kama masomo yenyewe yanahusu manunuzi, basi anafuatana na wanafunzi kwenda kwenye supermarket akiwaambia majina ya bidhaa mbalimbali. Mbinu hizo za ualimu zinawafurahisha wanafunzi ambao wanalichukulia darasa la lugha ya Kirussa kama ni jambo lenye furaha. Mwanafunzi mmoja Bibi Liu Falian alisema  "Madarasa ya mwalimu Katysha yanafurahisha sana. Anatumia mbinu mbalimbali kutufundisha neno moja, anatumia lugha, ishara za mikono, na picha. Kutokana na mbinu hizo, tunaelewa maneno kwa haraka na kuweka kumbukumbu imara. Sisi na mwalimu tunashirikiana kama ndugu na marafiki."

Bi. Katysha anapenda sanaa tangu utotoni mwake. Aliposoma katika chuo kikuu, alichagua kujifunza darasa la uchoraji picha. Katika mji wa Hegang, anapenda kuwaonesha wanafunzi wake utamaduni wa Kirussia kwa picha, na yeye mwenyewe pia anapenda kuchora picha za mandhari nzuri ya China. Chumbani kwake ametundika picha kadhaa alizochora mwenyewe, picha hizo zinahusu ukuta mkuu, mto Songhua na ziwa Jingpo, ambavyo ni vitutio vya utalii nchini China.

Bi. Katysha pia ana uhusiano mzuri na walimu wenzake Wachina, ambao wanapenda kumwelezea mila na desturi za Kichina. Walipokula chakula pamoja, wenzake walimwambia kuwa, wakati wa sikukuu ya Spring yaani sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China, Wachina wanapaswa kula samaki, maana yake ni kutakia kupata akiba kila mwaka, huku Mchina anaposherehekea siku ya kuzaliwa, anakula tambi ambayo urefu wake unamaanisha maisha marefu. Mwalimu Mchina Bibi Zhao Haiyan alimwambia mwandishi wetu wa habari akisema,  "Katysha ana uhusiano mwema na walimu wote wa kitivo chetu. Tunaona yeye si mgeni, bali ni dada yetu mdogo."

Katika kipindi alipoishi nchini China, Katysha alikuwa anajitahidi kuongeza kiwango chake cha lugha ya Kichina. Alikuwa anawasalimia Wachina wanaomfahamu kwa Kichina na kuongea nao, na chumbani kwake alibandika leba za maandishi ya Kichina kwenye chupa na televisheni, kwa kutumia mbinu hizo anaweza kufanya mazoezi ya Kichina wakati wote. Hivi sasa Bibi Katysha anaweza kuongea na wenyeji kwa kutumia Kichina bila matatizo.

Kutokana na mpango uliowekwa Katysha atarudi nyumbani mwaka kesho, lakini anataka kuongeza muda wa kufanya kazi nchini China. Alisema "Naipenda China sana. Kuja China ni ndoto nzuri niliyokuwa nayo moyoni mwangu. Nimeifanya China iwe maskani yangu ya pili. Iwapo nahitajika hapa, nitabaki na kuendelea na kazi yangu nchini China."

Mwaka huu China inaandaa harakati za mwaka wa utamaduni wa Russia nchini China. Hivi karibuni ujumbe mmoja kutoka maskani ya Bibi Katysha nchini Russia ulitembelea mji wa Hegang, ambapo Katysha alikutana na marafiki wengi. Msichana huyo alimweleza mwandishi wetu wa habari matumaini yake kuwa, wanafunzi wake wanaweza kujifunza kwa bidii lugha ya Kirussia, na mwaka kesho Russia itakapoandaa harakati za mwaka wa utamaduni wa China, yeye ataweza kuwaongoza wanafunzi wake Wachina kwenda kutembelea maskani yake nchini Russia.