Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-08 18:36:46    
Ushirikiano katika sekta ya kilimo kati ya China na Afrika una mustakabali mzuri

cri

Mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika muda mfupi uliopita, umeamua kuweka mkazo katika sekta ya kilimo. Maofisa wa serikali za nchi kadhaa za Afrika hivi karibuni walipohojiwa na waandishi wa habari wa China walisema, kilimo cha Afrika kina nafasi kubwa ya kuendelezwa, hivyo ushirikiano katika sekta ya kilimo kati ya China na Afrika utakuwa na mustakabali mzuri ukiungwa mkono na sera za pande hizo mbili.

Nchi za Afrika zina raslimali nyingi za kilimo, lakini nchi nyingi za Afrika bado haziwezi kujikimu kwa chakula kutokana na kuwa na teknolojia duni na kutokea kwa migogoro mara kwa mara. Hivi sasa nchi za Afrika zimeweka mkakati wa kuendeleza kilimo ili kujitosheleza kwa chakula na kuinua kiwango cha uzalishaji wa kilimo na mapato ya nafaka

kwa kufanya ushirikiano wa kimataifa. Ili kuvutia uwekezaji kutoka nchi za nje, nchi nyingi za Afrika zimetunga sera zinazotoa kipaumbele kwa kukodisha mashamba, kupunguza au kufuta kabisa ushuru wa kuagiza mitambo ya kilimo.

Waziri anayeshughulikia mambo ya kilimo wa Nigeria Bw. Bamidlai Dada alisema, China licha ya kutatua suala la kuwalisha watu zaidi ya bilioni 1.3, pia inasafirisha nje mazao mengi ya kilimo. Nigeria ni nchi yenye idadi kubwa kabisa ya watu barani Afrika, inataka kujifunza uzoefu wa China katika sekta hiyo.

Ushirikiano katika sekta ya kilimo kati ya China na Afrika ulianza katika miaka ya 60 ya karne iliyopita. Hadi leo China imezisaidia nchi zaidi ya 40 za Afrika kuanzisha miradi 200 ya ushirikiano, na kuweka vituo vya kueneza teknolojia ya kilimo. Serikali ya China kwa nyakati tofauti imewatuma wataalamu elfu kumi wa kilimo kuzisaidia nchi za Afrika kuandaa na kulima hekta elfu 70 za mashamba.

Hivi sasa hali ya kisiasa barani Afrika imekuwa inatulia siku hadi siku, serikali za nchi mbalimbali za Afrika zinatilia maanani kuendeleza kilimo, na kutoa fursa nzuri za kufanya ushirikiano wa kilimo kati yao na China. Imefahamika kuwa hivi sasa licha ya kulima mashamba, nchi za Afrika pia zinahitaji kufanya ushirikiano na China katika ufugaji samaki, ustadi wa ujenzi wa bustani, umwagiliaji maji wa kubana matumizi ya maji, kushughulikia mmomonyoko wa ardhi, matumizi ya gesi ya kinyesi na usindikaji na utengenezaji wa mazao ya kilimo. Ushirikiano huo umetoa fursa nyingi kwa makampuni ya China kuwekeza katika sekta ya kilimo barani Afrika.

Lakini kutokana na hali duni ya miundo mbinu ya mawasiliano na nishati ya nchi za Afrika, vitu vingi vya uzalishaji mali vinapaswa kuagizwa kutoka nchi za nje, hivyo kuanzisha miradi ya ushirikiano barani Afrika pia kuna hatari. Makampuni ya China yanatakiwa kufanya uchunguzi wa kutosha kuhusu mazingira ya uwekezaji na mustakabali wa soko kabla ya kuanzisha miradi rasmi.

Wataalamu wamependekeza kuwa, uwekezaji wa makampuni ya China katika nchi za Afrika unaweza kuanzia kwenye kilimo cha nafaka, halafu kuanzisha viwanda vya aina mbalimbali vya kusindika na kutengeneza mazao ya kibiashara kama vile mihogo, kakao, na michikichi, ili kuongeza thamani ya mazao hayo, bidhaa za mazao hayo si kama tu zitatosheleza mahitaji ya soko la Afrika, bali pia zinaweza kuuzwa kwenye soko la kimataifa.