Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-08 18:40:32    
Ripoti ya uchunguzi wa suala la Iraq ya Marekani yaibua maoni tofauti

cri

Baada ya kikundi cha uchunguzi wa suala la Iraq cha Marekani kukabidhi ripoti yake ya uchunguzi kwa rais George Bush tarehe 6 Desemba, nchi husika za Iraq, Iran, Syria na Israel zimetoa maoni tofauti kuhusu ripoti hiyo kutokana na maslahi yao mbalimbali.

Ripoti hiyo imetoa mapendekezo kuhusu sera za serikali ya Marekani kwa Iraq, kama vile kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na nchi jirani za Iraq, Syria na Iran, kulikabidhi jeshi la Iraq jukumu la kulinda usalama wa nchi hiyo na kufanya mkutano wa kimataifa kuhusu Israel kurudisha uwanda wa juu wa Golan kwa Syria ili kuleta amani katika mashariki ya kati.

Watu wa Iraq wana wasiwasi mkubwa kuhusu mambo yaliyomo kwenye ripoti hiyo. Naibu waziri mkuu wa Iraq Bwana Barham Saleh alisema, hivi sasa hali ya Iraq ni mbaya sana, si rahisi kuinua uwezo wa jeshi la Iraq katika muda mfupi, hivyo ni vigumu kwa jeshi la Iraq kuchukua jukumu la kulinda usalama na utulivu. Mbunge maarufu wa kabila la wakurd Bwana Mahmoud Othman alisema, ripoti hiyo ni matokeo ya chama cha Republic na chama cha Demokrasia cha Marekani kuzingatia maslahi yao binafsi. Naye msemaji wa shirikisho la wasomi wa kiislamu wa madhehebu ya Suni Sheik Mohammed Basharal-Fayadh alisema, ripoti ya Marekani inazingatia maslahi yao tu, na wala haijali uwezekano wa kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Iraq.

Lakini nchi tatu husika za Iran, Syria na Israel hazijatoa maoni makali. Waziri wa mambo ya nje wa Iran Bw. Manouchehr Mottaki tarehe 7 alisema, ripoti hiyo imekubali makosa ya sera za Marekani kwa Iraq. Wizara ya mambo ya nje ya Syria ilisema, ripoti ya Marekani inafuata ukweli wa mambo, hasa kukiri umuhimu wa nchi jirani za Iraq katika kulinda usalama na utulivu wa Iraq. Waziri mkuu wa Israel Bw. Ehud Olmert aliondoa uwezekano wa kurejesha mazungumzo ya amani kati ya Israel na Syria, na alikataa kutoa maoni kuhusu kama milima ya Golan itarudishwa kwa Syria au la.

Wachambuzi wamedhihirisha kuwa, maoni hayo tofauti yameonesha maslahi ya nchi mbalimbali. Hali ya Iraq inazidi kuwa mbaya siku hadi siku katika miaka mitatu iliyopita tangu vita ya Iraq imalizike, migogoro ya kisilaha imeongezekeza zaidi. Majeshi ya Marekani na Uingereza nchini Iraq yaliyozatitiwa vizuri bado hayawezi kulinda vizuri usalama wa huko, kwa hiyo haiwezekani kabisa kwa jeshi la Iraq kuchukua jukumu hilo peke yake, hivyo inaeleweka kwa pande mbalimbali za Iraq kuwa na wasiwasi kuhusu pendekezo la Marekani la kuondoa wanajeshi wake nchini Iraq.

Kama Marekani itaamua kufanya ushirikiano na Iran katika suala la Iraq, inapaswa kulegeza msimamo katika suala la nyuklia la Iran, na hiyo siyo nia ya rais George Bush wa Marekani, hivyo Iran haitatoa maoni ya furaha kwa ripoti hiyo. Ikiwa serikali ya Bush inakubali pendekezo la kuialika Syria kushiriki kwenye mchakato wa kutuliza hali ya Iraq na kuhimiza amani kati ya nchi za kiarabu na Israel, basi Marekani inapaswa kupunguza shinikizo dhidi ya Syria.

Israel siku zote inaona kuwa Syria inaunga mkono makundi yenye siasa kali ya Palestina na chama cha Hezbollah cha Lebanon katika mgogoro kati ya Lebanon na Israel, hivyo haitaki kufanya mazugnumzo ya amani na Syria. Mbali na hayo Israel inaifanya uwanda wa juu wa Golan kama ni sehemu yake muhimu ya kimkakati, haitaki kuirudisha sehemu hiyo kwa Syria. Israel inaona kuwa mambo husika yaliyotajwa kwenye ripoti ya uchunguzi ya Marekani hayalingani na maslahi yake.