Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-11 15:11:52    
Shughuli za utamaduni zachangia mkutano wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika

cri

Katika siku ambapo mkutano wa wakuu wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika ulipofanyika mjini Beijing, shughuli nyingi za utamaduni wa Afrika pia zilifanyika mjini Beijing.

Kwenye sehemu maarufu ya biashara Wang Fu Jing kando mbili za barabara zilioneshwa picha nyingi za mandhari nzuri ya Afrika, watoto wengi walipiga picha pamoja na sanamu za simba, twiga na pundamilia. Na mbele ya maduka makubwa picha za video kuhusu Afrika zilioneshwa kwenye skrin kubwa, na kila jioni wasanii wa China na wanafunzi wa Afrika wanaonesha michezo ya sanaa mara tatu uwanjani.

Mliyosikia ni ngoma ya Afrika iliyochezwa na wanafunzi wa Afrika, ngoma hiyo iliwavutia sana watazamaji na hata walichezacheza wakijisahau. Mmoja wa watazamaji aitwaye Zhang Dongbo aliwaambia waandishi wa habari akisema,

"Nimevutiwa sana, natumai kuwa shughuli kama hizo zitafanyika mara nyingi zaidi, shughuli kama hizo zinatusaidia sana sisi Wachina kuifahamu Afrika na kuongeza urafiki kati yetu, sijawahi kuona ngoma zao, wanaonekana ni watu wanaopendeza sana."

Mwanafunzi kutoka Nigeria anayesoma katika Chuo Kikuu cha Beijing Bw. Kelechi Ikonne alisema, anasoma lugha ya Kichina, na amewahi kutembelea miji mingi ya China. Alisema, Wachina na Waafrika wanaweza kueneza utamaduni wao kupitia mawasiliano ya kiutamaduni. Alisema,

"Katika nchi yetu, kuna Wachina karibu elfu ishirini, wao ni wafanyabiashara wanaweza kuongea lugha yetu. Wanaheshimu sheria za nchi yetu. Na wanafunzi wengi kutoka nchi yetu wanasoma lugha ya Kichina nchini China, tunaweza kuimarisha maingiliano ya kiutamaduni. Mimi napenda China kuliko nchi nyingine."

Katika siku za mkutano wa wakuu wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika pia kulikuwa na Maonesho ya Vitu vya Sanaa za Afrika na Maonesho ya Sarafu na Stempu za Nchi za Afrika. Viongozi wengi wakuu waliohudhuria mkutano huo walishiriki kwenye ufunguzi wa maonesho hayo. Naibu waziri wa utamaduni wa China Bw. Meng Xiasi kwenye ufunguzi alisema,

"Maingiliano ya kiutamaduni kati ya China na Afrika yalianzia mbali, sanaa za Afrika zenye historia ndefu zinavutia kila Mchina aliyewahi kuitembelea Afrika. Wachina wanapaswa kutazama maonesho hayo kwa makini na kuelewa nguvu zao kubwa za uhai, uwezo wao mkubwa wa uvumbuzi na kuelewa historia yao isiyo ya kawaida."

Kwenye Maonesho ya Vitu vya Sanaa za Afrika kuna vinyago zaidi ya 300, picha za tingatinga na vitu vya kusukwa. Na katika Maonesho ya Stempu na Sarafu kuna sarafu karibu 400 na stempu karibu seti 300 kutoka nchi 48 zenye uhusiano wa kibalozi na China. Vitu hivyo vimeonesha utamaduni, mila na desturi za watu wa nchi mbalimbali za Afrika. Mtazamaji Bi. Xi Bin alisema,

"Nimevutiwa na sanaa za Afrika, ni sanaa za kukaribia maumbile, zina mvuto wa kipekee."

Katika miaka ya karibuni kutokana na kuimarika kwa biashara kati ya China na Afrika maingiliano ya kiutamaduni kati ya pande mbili pia yamestawi, na mawasiliano ya kiserikali pia yameongezeka. Kabla ya kuanzishwa kwa mkutano wa Baraza la Ushirkiano kati ya China na Afrika wizara ya utamaduni ya China ilifanya tamasha la Afrika mjini Beijing, makundi ya wasanii kutoka Afrika ya Kusini, Misri, Gabon na nchi nyingine za Afrika walishiriki kwenye tamasha hilo. Michezo ya sanaa za Afrika imewapatia Wachina fursa ya kuona utamaduni wa Afrika ambao ulikuwa nadra kuuona.

Mkurugenzi wa sanaa katika Jumba la Makunbusho ya Taifa la Botswana Bw. Lesiga Phillip Segola alisema, tamasha hilo kubwa linasaidia sana kuimarisha maelewano kati ya pande mbili. Alisema,

"Kupitia tamasha hilo sisi tunaweza kujifunza mambo mengi hasa sanaa ya uchoraji wa Kichina. Na pia tunaweza kuwafahamisha marafiki zetu wa China utamaduni wa Botswana na wa Afrika. Tamasha hili linaufanya uhusiano wetu wa kirafiki uwe wa karibu zaidi."

Bw. Segola aliongeza kuwa Botswana na China zimeweka mpango wa maingiliano ya kiutamaduni, yaani kila baada ya miaka minne pande mbili zitafanya maonesho makubwa au shughuli kubwa za utamaduni katika kila nchi, ana matumaini makubwa juu ya maingiliano hayo, na anasubiri tena kuja China katika safari ijayo.

Idhaa ya kiswahili 2006-12-11