Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-12 15:05:22    
Ushirikiano kati ya kampuni binafsi na kampuni za kimataifa nchini China waendelezwa kwa kina

cri

Katika siku za karibuni kampuni binafsi nchini China zilikuwa na mazungumzo na kampuni kubwa za kimataifa kwenye mji wa Wenzhou, mkoani Zhejiang, sehemu ya kusini mashariki mwa China. Kauli-mbiu ya mazungumzo hayo ni "nafasi ya ushirikiano kati ya kampuni za China na za kimataifa", ambapo washiriki wa kampuni binafsi zaidi ya 100 na kampuni za kimataifa zaidi ya 30 zinazochukua nafasi za 500 za mbele duniani, walijadiliana kuhusu mwelekeo na mustakabali wa ushirikiano wao katika siku za baadaye.

Katika miaka 27 iliyopita tangu China ianze kutekeleza mageuzi, uchumi wa China umekuwa ukidumisha ongezeko la kasi, ambapo wastani wa ongezeko la pato la nchini kwa mwaka umefikia 9.6%. Ongezeko la mfululizo la uchumi limeleta mahitaji makubwa na nafasi nzuri ya maendeleo kwa kampuni za kimataifa na kampuni binafsi nchini China. Kiongozi wa shirikisho la makampuni ya China linaloshughulikia uwekezaji wa wafanyabiashara wa kigeni Bw. Shi Guangsheng alisema, kampuni za mitaji ya kigeni na kampuni binafsi nchini China ni nguvu mbili muhimu zinazohimiza maendeleo ya uchumi wa China.

"Hadi kufikia mwezi Septemba mwaka 2006, nchi na sehemu zilizowekeza nchini China zimefikia karibu 200, na thamani ya mitaji yao imezidi dola za kimarekani bilioni 660. Hivi sasa bidhaa zinazozalishwa na kampuni za wawekezaji kutoka nje na kusafirishwa kwa nchi za nje, ni zaidi ya nusu ya bidhaa zote za China zinazosafirishwa katika nchi za nje. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2005, thamani ya uzalishaji mali ya kampuni binafsi nchini China imechukua nusu ya jumla ya thamani ya uzalishaji mali wa taifa, na uwekezaji wa kampuni binafsi nchini China uliongezeka kwa karibu 30% katika miaka 5 iliyopita."

Habari zinasema katika kipindi cha mwanzoni baada ya kutekeleza sera za mageuzi na ufunguaji mlango, karibu kampuni zote binafsi nchini China ni za wastani na ndogo, ambazo zilikuwa na matatizo ya ukosefu wa mitaji na teknolojia ya kisasa, lakini kampuni za kimataifa zilizoingia nchini China wakati ule, ingawa zilikuwa na fedha nyingi zilikuwa hazifahamu vizuri hali ya soka la China. Hivyo, kufanya ushirikiano kati ya kampuni binafsi nchini China na kampuni za kimataifa ilikuwa njia bora. Naibu mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Johnson & Johnson ya Marekani, ambayo ni moja ya kampuni kubwa 500 za duniani Bw. Gao Rui alisema, umaalumu wa pande hizo mbili umezisaidia kufanya ushirikiano wa kunufaishana. Alisema,

"Kwa jinsi ninavyoona hii ni fursa nzuri sana, kampuni za kimataifa kuwa na ushirikiano na kampuni binafsi nchini China kunaweza kutoa uungaji mkono wa teknolojia na mitaji, kukuza uwezo wao wa usimamizi na kuboresha mazingira ya kazi. Kwa upande mwingine, pamoja na maendeleo ya shughuli za biashara za kampuni za nchi za nje hapa nchini, kampuni binafsi za China zinaziletea kampuni za nchi za nje fursa za kuongeza mali, tunatakiwa kuendana na mwelekeo wa maendeleo ya uchumi wa China na kuimarisha uhusiano na kampuni binafsi nchini China."

Mwanzoni ushirikiano kati ya kampuni binafsi za China na kampuni za kimataifa ulikuwa si mkubwa sana, kwa kawaida kampuni binafsi nchini China zilizalisha vipuri na kutoa huduma za ngazi ya chini kwa kampuni za kimataifa. Kampuni ya Coca Cola ilikuwa moja ya kampuni za kimataifa zilizoingia mapema na kuwa na ushirikiano na kampuni binafsi za nchini China. Mkurugenzi mkuu wa tawi la kampuni ya Coca Cola nchini China Bw. Chen Qiwei alisema, tokea mwishoni mwa miaka ya 80 ya karne iliyopita, chupa za soda za Coca Cola zilitengenezwa na kampuni binafsi za China.

"Baada ya kutumia teknolojia yetu kwa muda mrefu, kampuni binafsi za China zimefikia kiwango cha juu duniani katika uzalishaji wa chupa za soda. Kutokana na uzoefu wa kazi, kampuni hizo zikitumia ubora na uwezo wake na kujiimarisha zaidi, zitaweza kuwa kampuni binafsi zenye nguvu kubwa nchini China. Kampuni ya Zhongfu ya mjini Zhuhai na kampuni ya Zhijiang ya mjini Shanghai ni kampuni mbili zilizopata mafanikio makubwa, ambazo sasa ni kampuni zinazouza hisa kwenye soko la hisa, zinaendesha shughuli za aina nyingi, na pia ni kampuni muhimu zinazozalisha chupa za Coca Cola."

Hivi sasa zaidi ya 9% ya kampuni binafsi za nchini China zimejenga uhusiano wa ushirikiano na kampuni za kimataifa, pamoja na uendelezaji wa ushirikiano na kampuni za kimataifa, na kuongezeka kwa idadi ya kampuni binafsi, ushirikiano wa pande mbili unaendelezwa kwa mapana na marefu. Kiongozi wa taasisi ya utafiti wa uchumi wa kampuni binafsi ya China Bw. Bao Yujun alisema, kampuni binafsi za nchini China zinatakiwa kubadilisha zaidi mtindo wa usimamizi wa shughuli za kampuni na kuendeleza ushirikiano kwa undani zaidi katika siku za baadaye. Alisema,  

"Hivi sasa 70% ya kampuni binafsi zinaendeshwa na familia na jamaa zake, na 30% za kampuni binafsi zinatokana na kampuni za serikali au za ushirika. Kampuni za aina hizo mbili zote zimezoea kufanya maamuzi kwa kujitegemea na kujihusisha na wachina tu kutokana na kuathiriwa na utamaduni wa jadi wa China, desturi hiyo ya utamaduni haiendani na wazo la ushirikiano, tunatakiwa kuzifahamisha kampuni binafsi zifahamu kanuni zinazotumika duniani, kujifunza sheria na kanuni husika, mila na utamaduni wa kigeni ili kufanya ushirikiano wao uendelezwe kwa undani zaidi."

Kampuni ya Tianzheng ya mjini Wenzhou ni kampuni binafsi inayozalisha zana za umeme za viwandani. Katika miaka 3 iliyopita kampuni hiyo ilikuwa na ushirikiano mzuri na kampuni moja ya kimataifa. Katika maingiliano yao kampuni ya Tianzheng ilijifunza mambo mengi yanayonufaisha maendeleo ya kampuni binafsi za China, mkurugenzi mkuu wa kampuni Bw. Gao Tianle alisema, "Kwanza kabisa tunatakiwa kujifunza ujenzi wa kundi la watu, jambo muhimu kabisa ambalo kiongozi wa kampuni anatakiwa kufanya, ni kupata wataalamu wanaohitajiwa na kampuni, kampuni ikiwa na wataalamu mwafaka itaweza kuongeza ubora wake, ambao wa kwanza ni ubora wa ushindani katika soko, pili ni kujipanua kwa kutumia gharama ndogo, zaidi ya hayo tunatakiwa kujifunza mtindo wa uendeshaji shughuli, kuongeza uwazi katika usimamizi, hatua ambayo inaweza kuboresha mazingira kwa maendeleo ya kampuni."

Bw. Gao Tianle alisema katika ushirikiano wa kipindi kijacho, kampuni binafsi za China na kampuni za kimataifa zinatakiwa kuzingatia kuleta ufanisi kwa mshiriki mwenzake kwa kutumia ubora wake na kuongeza mali, kwani ni kufanya hivyo tu ndipo pande mbili za washiriki zitafikia hatua ya kunufaishana.

Idhaa ya kiswahili 2006-12-13