Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-12 15:02:51    
Mji wa Guizhou wawasaidia watu wenye kipato kidogo kwa mikopo kutoka benki

cri

Benki kutoa mikopo midogo ni njia yenye ufanisi ya kuwasaidia watu wenye kipato kidogo, ambayo ilianzishwa miaka zaidi ya 20 iliyopita na mwana-benki wa Bangladesh Bw. Muhammad Yunus aliyepata tuzo ya Nobel. China ilijaribu kuwasaidia watu wenye kipato kidogo kwa mikopo midogo ya benki kwenye baadhi ya sehemu tokea mwaka 1993. Hivi karibuni mwandishi wetu wa habari alitembelea wilaya ya Pan, mkoani Guizhou, ambapo inafanya majaribio ya kuwasaidia wakulima maskini kwa kuwapatia mikopo midogo ya benki.

Wilaya ya Pan mkoani Guizhou iliyoko sehemu ya kusini magharibi mwa China, ilianza kuwasaidia wakulima maskini kwa mikopo midogo ya Benki tokea mwaka 1998, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2003 jumla ya fedha za mikopo iliyotolewa ilifikia Yuan milioni 260, ambayo imefanya idadi ya watu maskini ipungue hadi kiasi cha laki 1 kutoka zaidi ya laki 2 mwaka 1998. Kijiji cha Heshengdi kilichoko wilayani Pan, kilikuwa ni kijiji chenye watu maskini sana, lakini sasa kimeondokana na umaskini kutokana na mikopo midogo kutoka benki. Kiongozi wa kijiji hicho Bw. Wang Guohua alisema, "mwaka 2001 tulijaribu kuanzisha shughuli za kufuga ng'ombe, lakini baadhi ya familia za wakulima hazikuwa na mitaji ya kuanzisha shughuli za ufugaji, sisi viongozi wa kijiji tulijadili suala hilo na kuzishawishi familia 24 kuomba mikopo kutoka benki ya Yuan laki 1.5. Kabla ya kuanzisha shughuli za ufugaji wastani wa pato la kila mtu ulikuwa Yuan 1,000 kwa mwaka, baada ya miaka 5, sasa kwenye kijiji hicho kuna vituo vinne vya ufugaji ng'ombe, na wastani wa pato la kila mtu kwa mwaka umeongezeka hadi kufikia Yuan 1,800."

Mkulima Hu Wenzheng amefuga ng'ombe wengi katika kijiji cha Heshengdi, mwaka 2002 alipata mkopo wa Yuan 5,000 na kununua ng'ombe 3, sasa ana ng'ombe 15, na kila mwaka anapata Yuan 8,000 kutokana na ufugaji, licha ya kujenga nyumba pia ameweza kununua vyombo vya umeme vya nyumbani.

Baada ya pato la wanakijiji kuongezeka, wanakijiji walijitolea kujenga barabara moja inayokwenda kwenye sehemu ya nje, kwa ujumla hivi sasa ujenzi wa barabara hiyo umekamilika. Mbali na hayo kila familia ya wanakijiji imejenga bwawa la gesi ya asili, ambayo imetatua suala la nishati na kuleta mwanga usiku, na pia imeboresha mazingira ya maisha.

Mikopo midogo ya benki imebadilisha mtizamo wa kukuza uwezo wa uendeshaji shughuli wa serikali za mitaa. Katika mahojiano na watu wa huko, mwandishi wetu wa habari alisikia mara kwa mara neno la "usimamizi" lililosemwa sana maofisa wa huko. Katika wilaya ya Pan mikopo midogo inatolewa na benki za biashara. Kutokana na sera husika za serikali, ingawa benki hizo hazina lengo la kujipatia faida kubwa kutokana na utoaji mikopo midogo, lakini hazitaki kuingia hasara. Ingawa familia za wakulima zinazoomba mikopo hazitakiwi kuweka rehani katika benki, lakini sharti la kupata mikopo kwa tarafa ni kuwa na sifa nzuri za uaminifu. Benki hazitaki kuzipa mikopo tarafa zisizo na uwezo wa kurudisha fedha za mikopo. Hivyo baada ya kupata mikopo, namna ya kusimamia matumizi ya mikopo ya familia za wakulima na kuhakikisha kuwa kila familia ya wakulima inayopata mkopo itarudisha fedha za mkopo katika muda uliowekwa, ni suala jipya linalowakabili maofisa wa vijijini.

Habari zinasema kila tarafa ya wilaya ya Pan imeanzisha kitengo maalumu kinachosimamia matumizi ya mikopo, ambapo kila kijiji kimeanzisha kituo cha kusaidia wakulima maskini kinachowajibika kurudisha fedha za mikopo. Mikopo midogo ya benki imebadilisha mtizamo wa wakulima, sasa wanasema tunaweza kujiendeleza kwa kukopa fedha, ili mradi tuwe na bidii za kazi na uaminifu.

Idhaa ya kiswahili 2006-12-13