Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-13 15:32:19    
Waziri mkuu wa Israel kudokeza kuhusu silaha za nyuklia nchini Israel kwasababisha mtafaruku

cri

Waziri mkuu wa Israel Bw. Ehud Olmert tarehe 11 alipozungumza na waandishi wa habari aliorodhesha Israel kwenye nchi zinazomiliki silaha za nyuklia. Hii ni mara ya kwanza kwa waziri mkuu wa Israel kuashiria hadharani kuwa Israel inamiliki silaha za nyuklia katika nusu karne iliyopita. Habari hiyo ilipotangazwa mara ikasababisha mtafaruku kote nchini Israel, na vyombo vya habari vikachapisha habari hiyo kwenye ukurasa wa kwanza katika magazeti yao, na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani nchini Israel wanamtaka Bw. Ehud Olmert ajiuzulu. Waziri mkuu huyo sasa amejiingiza kwenye sakata la kisiasa.

Mtafaruku huo ulitokea kituo cha televisheni cha Ujerumani kutangaza mazungumzo kati ya waandishi wa habari na Bw. Ehud Olmert. Waziri mkuu huyo alipoulizwa kuhusu suala la nyuklia la Iran, alisema kwa Kiingereza, "Israel haijawahi kutishia kuangamiza nchi yoyote, lakini Iran inatishia hadharani kuifuta Israel kutoka kwenye ramani ya dunia. Je, wakati Iran inapotamani kumiliki silaha za nyuklia, unaweza kusema hii ni sawa na nchi za Ufaransa, Marekani, Russia na Israel?"

Mazungumzo hayo yalipotangazwa wasaidizi wa waziri mkuu wa Ehud Olmert walijitahidi kujitokeza kumtetea. Ofisi ya waziri mkuu wa Israel ilitoa taarifa ikisema kwamba kauli ya Bw. Olmert ilitafsiriwa bila kikamilifu, vyombo vya habari vimepotosha maana aliyosema. Tarehe 12 kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanywa na Bw. Olmert na chansela wa Ujerumani Bi. Angela Markel, Bw. Olmert mara tatu alisisitiza kwamba Israel haitakuwa nchi ya kwanza kuingiza silaha za nyuklia katika Mashariki ya Kati. Na pia alisisitiza kuwa kwenye mazungumzo na waandishi wa habari hakwenda kinyume na sera ya Israel kuhusu suala la silaha za nyuklia.

Hata hivyo, vyombo vya habari vinaona kuwa Bw. Olmert ameashiria kwamba Israel inamiliki silaha za nyuklia, na amedhirisha msimamo usiokuwa wazi kuhusu umiliki wa silaha za nyuklia katika muda wa miaka 50 iliyopita. Kabla ya hapo, Israel haikuwahi kukubali wala kukataa kuwa na silaha za nyuklia, kufanya hivyo ni kwa ajili ya kutishia nchi adui na kukwepa mashindano ya kisilaha ya kikanda. Marekani na nchi za magharibi zimeikubali kimya kimya sera hiyo ya Israel, mradi tu Israel ikinyamaza kimya nchi hizo hazitaitatiza Israel katika suala hilo kwa mfano kuiwekea vikwazo. Lakini kuwa na silaha za nyuklia kwa Israel kumekuwa siri wazi. Wachambuzi wanaona kuwa tangu miaka ya 60 ya karne iliyopita hadi sasa Israel imetengeneza mabomu ya nyuklia kati ya 80 hadi 200. Siku kadhaa kabla ya ziara ya Bibi Merkel nchini Israel, Bw. Robert Gates atakayekuwa waziri wa ulinzi wa Marekani, kwenye baraza la juu la Marekani pia alidokeza habari hiyo, na alipofafanua nia ya Iran kuwa na silaha za nyuklia alisema Iran inazingirwa na nchi zenye silaha za nyuklia ikiwemo Israel.

Nchi za Kiarabu pia zinafuatilia sana kauli ya Bw. Olmert zikitaka Marekani na jumuyia ya kimataifa ziishughulikie Israel. Katibu mkuu wa Kamati ya Ushirikiano ya Nchi za Ghuba tarehe 12 alisema, Marekani haifai kutumia vigezo viwili katika suala la silaha za nyuklia, na alisema jumuyia ya kimataifa inapaswa kuichukulia kauli ya Bw. Olmert kama ni tishio kwa amani na usalama duniani.

Hivi sasa bado haifahamiki kama kauli ya Bw. Olmert italeta matokeo gani kwa Israel na kwake mwenyewe, lakini gazeti la Israel la Yedioth ilichapisha makala ya mhariri ikisema kauli ya Bw. Olmert imevisaidia sana vyombo vya habari vya Israel, kwamba baadaye vitakapochapisha kuhusu uwezo wa nyuklia havina haja kusema, "kwa mujibu wa habari za nje".

Idhaa ya kiswahili 2006-12-13