Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-13 17:02:07    
China yajitahidi kuanzisha ushirikiano wa kimataifa kuhusu matibabu ya jadi

cri

Nchi nyingi duniani zina matibabu yake ya jadi, kwa mfano matibabu ya mitishamba ya kichina, Yoga ya India na matibabu ya homeopathy ya Ulaya. Matibabu ya aina hizo zote ni nadharia maalum za kisayansi zilizovumbuliwa na watu wa nchi mbalimbali katika muda mrefu wa kazi na mapambano dhidi ya magonjwa, na matibabu hayo yametoa mchango muhimu katika kinga na tiba ya magonjwa ya binadamu na maendeleo ya sayansi ya matibabu. Lakini kutokana na sababu mbalimbali, baadhi ya matibabu hayo yanakaribia kutoweka.

Pamoja na kuwepo kwa maendeleo ya kasi ya sayansi na teknolojia duniani, na mtizamo mpya wa binadamu kuhusu magonjwa, afya na matibabu, watu wameanza kugundua umaalum wa matibabu ya jadi, kwani masuala yanayoshindwa kutatuliwa kwa matibabu ya kisasa yanapata ufumbuzi katika matibabu ya jadi. Hivyo nchi mbalimbali duniani zimeongeza nguvu katika utafiti na matumizi ya matibabu ya jadi.

Dawa na matibabu ya kichina vikiwa ni matibabu ya jadi ya China, ni vitu ambavyo vinaendelea kutiliwa maanani nchini China, hivyo zimepata maendeleo makubwa, na pia zimekuwa ni sehemu muhimu katika matibabu ya jadi duniani kutokana na juhudi za China. Mkurugenzi wa ofisi ya ushirikiano wa kimataifa katika idara ya usimamizi wa dawa na matibabu ya jadi ya kichina Bw. Sheng Zhixiang alieleza:

"nchi nyingi duniani zina aina tofauti za matibabu ya jadi, kutokana na nadharia husika, matibabu ya jadi ya kichina ni mfumo kamili wa matibabu, hivyo yanaenea kwenye sehemu nyingi zaidi duniani."

Jambo la kwanza linalopaswa kufanywa na China katika shughuli za mawasiliano ya kimataifa kuhusu matibabu, ni kufahamisha zaidi dawa na matibabu ya kichina duniani. Kuanzia miaka ya 70 ya karne iliyopita, kutokana na uungaji mkono wa serikali ya China, dawa na matibabu ya kichina yameanza kujulikana duniani. Kwa mujibu wa takwimu za awali, hivi sasa dawa na matibabu ya kichina yameenezwa katika nchi zaidi ya 130 duniani, idara zaidi ya elfu 50 za matibabu ya kichina katika nchi za nje zimeanzishwa na zina madaktari zaidi ya laki 1.2.

Aidha, mawasiliano kati ya China na nchi za nje kuhusu shughuli za kuandaa wataalamu wa matibabu ya kichina na kufanya utafiti wa kisayansi, pia yanafanyika mara kwa mara. Katika miaka mingi iliyopita, idadi ya wanafunzi wa nje waliokuja China kupewa mafunzo kuhusu matibabu ya kichina imeendelea kuchukua nafasi kubwa zaidi, kuliko ile ya taaluma nyingine za kisayansi. Katika miaka ya hivi karibuni, baadhi ya vyuo vya matibabu ya kichina vimeanzisha ushirikiano na vyuo vya nchi au sehemu mbalimbali duniani, na kuanzisha taasisi ya matibabu ya kichina au kuweka mchepuo wa matibabu ya kichina katika vyuo vikuu hivyo. Mbali na hayo, vyuo vikuu vya China na nchi za nje pia vimepanua zaidi ushirikiano na idara za matibabu, utafiti na uzalishaji, na kiwango na ngazi za ushirikiano huo pia zimeinuka. Kwa mfano ushirikiano wa utafiti kati ya China na Tanzania kuhusu tiba na kinga ya ugonjwa wa Ukimwi, na ushirikiano wa utafiti kati ya China na Australia kuhusu tiba na kinga ya magonjwa ya damu.

Mbali na hatua hiyo, China pia inatilia maanani katika ushirikiano wa kimataifa kuhusu usimamizi na utungaji sheria wa matibabu ya jadi, na kuchukua matibabu ya jadi kwenye mfumo wa taifa wa matibabu. Shirika la afya duniani WHO linaona kuwa, matibabu ya jadi ni mali ya pamoja ya ustaarabu wa binadamu, na pia ni raslimali muhimu ya afya. Hivyo shirika la afya duniani linajitahidi kusukuma mbele maendeleo ya matibabu ya jadi, mkurugenzi wa idara ya ushirikiano wa teknolojia kuhusu dawa za kawaida na matatibu ya jadi katika shirika la afya duniani Bi. Malebona Matsoso alisema,

"katika mkakati wa maendeleo ya matibabu ya jadi duniani uliotolewa mwaka 2003 na shirika la afya duniani, shirika hilo linazitaka nchi wanachama wa shirika hilo kuweka sera za taifa za kuendeleza matibabu ya jadi. Hatua nyingi zilizochukuliwa na serikali ya China zinakubaliwa na kusifiwa na shirika hilo.

Nchi nyingi zimewahi kutuma ujumbe kuja China kufanya uchunguzi kuhusu hali ya utungaji sheria na usimamizi wa matibabu ya jadi nchini China. China pia ilisaini mkataba na shirika la afya duniani na kuahidi kulisaidia shirika hilo kuendeleza matibabu ya jadi duniani, kwa njia ya mawasiliano ya taarifa na teknolojia. Naibu mkuu wa idara ya usimamizi wa dawa na matibabu ya jadi ya China Bw. Li Daning alisema,

"China ikiwa ni nchi mwanachama wa shirika la afya duniani, inabeba jukumu na pia ina uwezo wa kuhimiza maendeleo na matumizi ya matibabu ya jadi, kutoa uzoefu wake kwa nchi mbalimbali, hasa kuhusu hatua ya kuchukua matibabu ya jadi ya kichina kwenye mfumo wa taifa wa matibabu. China inataka kutoa mchango wake kwa ajili ya maendeleo ya matibabu ya jadi kutokana na maelekezo ya shirika la afya duniani."

Wakati matibabu ya jadi ya kichina yanapoenezwa kote duniani, matibabu mengi ya jadi ya nchi za nje yakiwemo matibabu ya Yoga na homeopathy pia yameanza kuenezwa nchini China. Mkurugenzi wa Ofisi ya ushirikiano wa kimataifa katika idara ya usimamizi wa dawa na matibabu ya jadi ya China Bw. Shen Zhixiang anaona kuwa, wakati ya kueneza matibabu ya kichina kwa nchi za nje, China pia inapaswa kujifunza kutokana na raslimali za matibabu ya jadi ya nchi za nje, ili kuhudumia afya ya watu wa China.