Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-15 16:55:22    
Uchumi wa dunia unapiga hatua ukiwa na fursa na changamoto

cri

Ripoti Kuhusu Makadirio ya Uchumi Duniani kwa Mwaka 2007 iliyotangazwa na Benki ya Dunia tarehe 13 Desemba imesema, kwa ujumla hali ya uchumi duniani kwa mwaka 2006 ilikuwa nzuri, na kwa makadirio ongezeko la uchumi litafikia 5.1% ambalo ni kubwa kuliko ongezeko la 3.2% la mwaka 2005. Lakini sambamba na ongezeko hilo, bei kubwa ya mafuta na utetezi wa kujilinda kibiashara vinahatarisha kukua kwa uchumi wa dunia.

Ongezeko la uchumi duniani mwaka 2006 limewatia watu moyo, kwamba uchumi wa Marekani unaendelea kuongezeka, uchumi wa nchi zinazotumia Euro umeanza kufufuka, uchumi wa Japan kimsingi umepita kipindi cha kubana matumizi ya fedha, China inaendelea kuwa kama injini ya kusukuma mbele uchumi duniani, na uchumi wa Asia, Afrika na Latin Amerika pia unaendelea kuongezeka. Kuhusu ongezeko la uchumi duniani kwa mwaka 2006, mkurugenzi wa taasisi ya uchumi duniani nchini China Bw. Jiang Yong alisema kuna sababu tatu zilizochangia ongezeko hilo, alisema,

"Sababu ya kwanza ni kuwa, nguvu za kusukuma uchumi zilikuwepo hapo awali; pili ni kuwa ongezeko la uchumi lilitokana na sehemu nyingi, na matumizi ya fedha nchini Marekani ni kama injini ya kusukuma uchumi toka zamani, na uzalishaji mali nchini China ni injini mpya, injini hizo mbili zimeongeza nguvu y ongezeko la uchumi huo; tatu ni kuwa hali ya sehemu zilizokuwa zinakwamisha maendeleo ya uchumi imeboreshwa, na uwiano wa ongezeko la uchumi kimsingi umepatikana. Licha ya sababu hizo pia sababu nyingine ni kuwepo kwa fedha nyingi, na fedha hizo ziliwekezwa kwenye soko na kuzalisha mali nyingi."

Marekani ikiwa ni nchi yenye uchumi wenye nguvu kabisa duniani mwelekeo wake wa kiuchumi unavutia uangalifu wa watu duniani. Kwa mujibu wa makadirio ya Benki ya Dunia, ongezeko la uchumi nchini Marekani litafikia 3.2% mwaka huu, ongezeko hilo bado ni kubwa miongoni mwa nchi zilizoendelea. Prof. Frederic Joutz wa Chuo Kikuu cha George Washintong alisema,

"Ingawa katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka huu ongezeko la biashara ya viwanja na nyumba nchini Marekani limepungua, lakini kwa ujumla uchumi wa Marekani unaongezeka kwa nguvu. Hivi karibuni shughuli za uwekezaji nchini humo zimepamba moto, na ongezeko la matumizi ya fedha ni sababu moja muhimu ya kukua kwa uchumi wa Marekani."

Hali ya uchumi barani Asia ikiwa ni pamoja na uchumi wa China mwaka huu imevutia sana. Ripoti ya Benki ya Dunia inasema, maendeleo ya uchumi wa China yamesukuma mbele uchumi duniani, na yataendelea kutilia mkazo maendeleo ya uchumi huo. Baadhi ya watu wanaona kuwa ongezeko la uchumi nchini China limekuwa la kasi kupita kiasi. Kuhusu suala hilo Bw. Jiang Yong ana maoni tofauti. Alisema,

"Suala la ongezeko la kasi kupita kiasi haliko kwa sekta zote bali ni suala kwenye sekta fulani na mitaa fulani tu nchini China, kwa ujumla udhibiti wa uchumi wa kitaifa umepata mafanikio kwa kiasi kikubwa."

Ripoti ya Benki ya Dunia pia imetoa maoni hayo hayo, ikisema kwa makadirio, ongezeko la uchumi nchini China litakuwa 9.6% kutoka ongezeko la mwaka huu 10.4%. Hii imanaanisha kuwa udhibiti wa uchumi wa kitaifa nchini China unaelekea kwenye lengo lililopangwa.

Wataalamu wanaona kuwa wakati uchumi duniani unapokua pia unakabiliwa na hatari. Bw. Jiang Yong alisema,

"Hatari inayokabili uchumi wa dunia ni ongezeko la bei ya mafuta na ongezeko la riba za mikopo; hatari nyingine ni kuwa pengine bei ya viwanja na nyumba itashuka kwa kasi. Kwa makadirio ya Kampuni ya Goldman Sachs, kama bei na viwanja na nyumba ikishuka kwa kasi nchini Marekani, ongezeko la uchumi nchini humo litapungua kwa 1.5%, na uchumi wa dunia utaathirika. Hatari ya tatu ni kuwa duru la mazungumzo ya Doha limekwamishwa, hayo ni matokeo ya utetezi wa kujilinda kibiashara, na athari yake yumkini itaonekana wazi baada ya mwaka 2007."

Ripoti ya Benki ya Dunia imesema hivi sasa ongezeko la uchumi wa dunia limefikia kwenye hatua ya kugeuka, ongezeko lake limekuwa likipungua. Kwa makadirio, mwaka 2007 kutakuwa na ongezeko la 4.5%. Shirika la Fedha Duniani linataka nchi zote wanachama ziimarishe ushirikiano na kupunguza kujilinda kibiashara na kupambana na hatari hizo kwa pamoja ili kufanya uchumi wa dunia upate maendeleo endelevu.

Idhaa ya Kiswahili 2006-12-15