Mwaka wa 2006 unaokaribia kumalizika, ni mwaka ambao suala kuhusu silaha za nyuklia lilifuatiliwa mara kwa mara. Vitendo vya nchi kadhaa katika sekta ya nyuklia vilichochea utaratibu wa kimataifa wa kutosambazwa kwa silaha za nyuklia na kuwapa watu wasiwasi kuhusu mustakbali wa utaratibu huo..
"Nchi za magharibi zinatakiwa kutambua kuwa watu wa Iran hawataacha haki ya halali ya kutumia nishati za nyuklia kwa amani, kujinufaisha kutoka nishati za nyuklia ni matakwa ya wananchi wote wa Iran".
Hayo ni maneno yaliyomo kwenye hotuba aliyotoa rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mwezi Septemba nchini Iran. Ingawa azimio namba 1696 la baraza la usalama liliitaka Iran isimamishe shughuli za uranium nzito kabla ya tarehe 31 mwezi Agosti, lakini Iran ilipuuza azimio hilo na kuendeleza mpango wake wa nyuklia hatua kwa hatua.
Suala la nyuklia la Iran halijatatuliwa, Korea Kaskazini tarehe 9 mwezi Oktoba ilifikia hatua ya kufanya majaribio ya nyuklia na kutangaza kuwa Korea Kaskazini ni nchi yenye silaha za nyuklia. Kuhusu jambo hilo, mkurugenzi mkuu wa shirika la nishati ya atomiki duniani IAEA Bw. Mohamed El Baradei alitoa hotuba kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York na kusema:
"Majaribio ya nyuklia yaliyofanywa na Korea Kaskazini yaliwatia watu wasiwasi mkubwa na yamekwenda kinyume na mkataba wa kutosambaza silaha za nyuklia na kuweka vikwazo kwenye juhudi zilizofanywa na jumuiya ya kimataifa katika kuhimiza kupunguza silaha za nyuklia".
Bw Fan Jishe wa taasisi ya sayansi ya kijamii ya China anaona kuwa baada ya kutokea kwa vita vya Iraq, kuhisi tishio kutoka nje kwa nchi kadhaa zikiwemo Korea Kaskazini na Iran ni sababu moja ya kufanya majaribio ya nyuklia kwa Korea ya kaskazini na wasiwasi wao kuhusu usalama sio jambo lisilovumiliwa na alisema:
"Wakati nchi fulani inapokabiliwa na tishio la kufa na kupona, kutafuta ulinzi wa silaha kali sio jambo la ajabu".
Zaidi ya hayo nchi fulani zimeacha wajibu wao kuhusu upunguzaji wa silaha za nyuklia kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao ya mkakati wa kijeshi, jambo ambalo limeharibu uwiano wa haki na wajibu uliofikiwa na nchi zenye silaha za nyuklia na nchi zisizo na silaha hizo, wakati wa kusaini mkataba wa kutosambaza silaha za nyuklia. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan atakayemaliza madaraka yake alieleza wasiwasi wake mkubwa, alisema:
"Tunapaswa kufanya juhudi katika pande mbili za kupunguza silaha za nyuklia na kuzuia kusambazwa kwa silaha hizo, kama nchi zenye silaha za nyuklia na zisizo na silaha hizo zitachukua hatua kwanza, basi juhudi za kupunguza silaha za nyuklia na kutosambaza silaha hizo zitaendelezwa kwa pamoja".
Wachambuzi wameainisha kuwa suala la kutosambaza silaha za nyuklia linahusu usalama wa jumuiya nzima ya kimataifa, na haiwezekani kwa nchi moja kukamilisha kazi hizo, jumuiya ya kimataifa inapaswa kufanya juhudi kwa pamoja. Ni kwa kufanya hivyo tu, ndivyo lengo la kujenga dunia yenye amani na usalama isiyo na tishio la silaha kali za maangamizi litakavyoweza kutimizwa.
|