Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-19 15:59:16    
Ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki waingia katika kipindi kizuri

cri

Mwaka huu miaka 15 imetimia tangu uhusiano wa mazungumzo kati ya China na umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki uanzishwe. Hivi karibuni viongozi wa China na nchi 10 za umoja wa Asia ya kusini mashariki walishiriki kwenye mkutano uliofanyika katika mji wa Nanning, mji mkuu wa mkoa unaojiendesha wa kabila la wazhuang, China, na kuweka mpango kamambe wa maendeleo katika siku za baadaye. Pande mbili ziliamua kuanzisha eneo la biashara huria kati ya China na umoja huo kabla ya muda uliowekwa wa mwaka 2010.

Miaka 15 iliyopita China na umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki zilizindua mchakato wa mazungumzo, na kufungua ukurasa mpya wa uhusiano wa pande mbili. Pamoja na kuboreshwa kwa mawasiliano na kupunguzwa hatua kwa hatua kwa ushuru wa forodha, thamani ya biashara kati ya China na umoja huo iliongezeka mara 15, hivi sasa umoja huo umekuwa mwenzi wa nne mkubwa katika shughuli za biashara kwa China.

Mwishoni mwa mwezi uliopita kwenye mkutano uliofanyika mjini Nanning wa kuadhimisha miaka 15 tangu uhusiano wa mazungumzo wa pande hizo mbili uanzishwe, mwenyekiti wa sasa wa umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki ambaye ni Rais Gloria Arroyo wa Philippines alisema, umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki unataka kuimarisha uhusiano wa pande mbili na China kwa kupitia kuanzishwa kwa eneo la biashara huria.

"Biashara kati yetu na China inakuzwa kwa mfululizo, tunatarajia kuwa China itaongeza uwekezaji katika nchi za umoja huo. China imenyanyuka kwenye jukwaa la dunia, umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki nao unatakiwa unyanyuke pamoja na China, hivyo mageuzi yatakuwa makubwa sana. Viongozi wa nchi mbalimbali wanataka sana kuimarisha uhusiano kati ya China na umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki kwa kuendeleza eneo la biashara huria.

Mwezi Novemba mwaka 2002, kwenye mkutano wa wakuu wa nchi 10 za umoja huo na China uliofanyika huko Phnom Penh, mji mkuu wa Cambodia, wakuu wa nchi walithibitisha rasmi kuanzishwa kwa eneo la biashara huria kati ya China na umoja huo. Eneo hilo la biashara linahusisha nchi 11 zikiwemo China, Brunei, Cambodia, Indonesia na Vietnam, ambazo idadi ya watu wake ni kiasi cha bilioni 1.8 na zenye pato la dola za kimarekani trilioni 2.

Baada ya kushauriana kwa miaka mingi, hivi sasa pande mbili za China na umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki zimeafikiana na kusaini "mapatano ya biashara ya bidhaa" na "mkataba wa mfumo wa utatuzi wa migogoro". Tokea mwezi Julai mwaka jana, ushuru wa aina zaidi ya 7,000 za bidhaa za China na umoja huo ulianza kupungua, hadi mwaka 2010, ushuru wa zaidi ya 90% ya bidhaa za China na umoja wa Asia ya kusini mashariki utafutwa kabisa. Tangu mpango wa upunguzaji ushuru uanze kutekelezwa, uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na umoja wa Asia ya kusini mashariki umeimarishwa zaidi, thamani ya biashara inaongezeka kwa kasi, na kuleta manufaa halisi kwa viwanda na wanunuzi wa China na nchi za umoja wa Asia ya kusini mashariki.

Mji wa Dongxing wa mkoa wa Guangxi uko kwenye mpaka wa China na Vietnam, na ni forodha muhimu kati ya China na Vietnam. Mfanyabiashara wa Vietnam Bw. He Wenping anaendesha biashara ya mbao aina ya rosewood kwa kushirikiana na mfanyabiashara wa China tangu miaka 10 iliyopita. Hivi sasa anafanya uchunguzi kuhusu soko la samani nchini China, akitaka kusafirisha samani zilizotengenezwa kwa rosewood kwa China.

"Ninafikiria kufanya biashara ya samani ya rosewood kwa kushirikiana na mchina, mshirika wangu ananisaidia kusafirisha samani za rosewood za Vietnam hadi kwenye soko la China, tukishirikiana pamoja mambo yatakuwa rahisi na yenye faida zaidi. Mbali na hayo, nimenuia kujenga kiwanda cha samani za rosewood nchini China."

Katika mji wa Dongxing kuna wafanyabiashara wengi kama Bw. He. Kati ya mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu, zaidi ya watu milioni 2 walipita kwenye forodha ya Dongxing, na thamani ya bidhaa zilizopita kwenye forodha hiyo ilikaribia dola za kimarekani milioni 200.

Jambo muhimu ni kuwa muundo wa biashara kati ya China na umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki unaboreshwa na kubadilishwa, ambao maendeleo yake yanaelekea kuzalisha bidhaa badala ya kusafirisha mali-ghafi kwa nchi za nje, hususan uzalishaji wa mitambo na vyombo vya umeme unatumia teknolojia ya kisasa. Mwaka uliopita thamani ya biashara ya bidhaa za mitambo, vyombo vya umeme na bidhaa za teknolojia ya kisasa inachukua zaidi ya nusu ya jumla ya thamani ya biashara kati ya China na nchi za umoja huo.

Uhusiano tulivu wa kisiasa na soko kubwa vinahimiza ushirikiano wa uwekezaji kati ya China na umoja huo katika hali nzuri hatua kwa hatua. Katika miaka 15 iliyopita, nchi za umoja wa Asia ya kusini mashariki zimekuwa vyanzo muhimu vya uwekezaji nchini China, vilevile nchi hizo zimekuwa sehemu ya kwanza inayochaguliwa kwa uwekezaji wa kampuni na viwanda vya China. Hadi mwishoni mwa mwaka 2005, uwekezaji wa nchi za umoja wa Asia ya kusini mashariki nchini China ulifikia dola za kimarekani bilioni 38.5, wakati viwanda vya China vilijenga viwanda zaidi ya 1,000 katika nchi 10 za umoja wa Asia ya kusini mashariki.

Maonesho ya biashara ya China na umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki, yanafanyika kila mwaka, yamekuwa mahali muhimu pa kuvutia uwekezaji kati ya China na umoja huo. Katika maonesho ya mwaka huu, mwandishi wetu wa habari aliona, nchi zote za umoja huo zimetoa sera nyingi za nafuu ili kuvutia uwekezaji wa viwanda vya China. Kwa mfano, baadhi ya mikoa ya Vietnam inasamehe kodi ya ardhi kwa viwanda vyenye mitaji ya China, kutoa ruzuku kwa gharama za uhamishaji wa nyumba na kupunguza kodi kwa kiwango fulani; Malaysia inasamehe kodi kwa miaka 10 kwa viwanda vya uzalisjaji mitambo vilivyowekezwa na China nchini humo.

Ofisa mtendaji wa kituo cha uhimizaji wa uwekezaji na biashara cha mji wa Hu Chiming wa Vietnam, Bibi Duyoanh alimwambia mwandishi wetu wa habari,

"Tumejenga kituo cha kuhimiza uwekezaji na biashara, ambacho kinatoa huduma za habari na sera kwa viwanda na kampuni zinazowekeza nchini mwetu. Huduma za elimu na mambo ya biashara zinazohusika pia ni maeneo ya uwekezaji tunayohitaji sana."

Dalili nyingi zinaonesha kuwa wakati shughuli za biashara na uwekezaji kati ya China na umoja wa Asia ya kusini mashariki zinapoongezeka, ushirikiano katika maeneo ya mambo ya fedha, uchukuzi na maonesho kati ya pande hizo mbili pia unapanuliwa siku hadi siku. Hivi karibuni, viongozi wa ngazi ya juu wa benki ya maendeleo ya China na benki ya maendeleo ya Vietnam walikuwa na mazungumzo wakiweka mpango wa kuendeleza ushirikiano katika mambo ya fedha; Wizara ya biashara ya Thailand na ofisi za konsela za nchi za Vietnam na Myanmar pia zimesaini mkataba wa ushirikiano na kituo cha maonesho ya kimataifa ya Kunming, mji mkuu wa mkoa wa Yunnan, China zikinuia kujenga majumba ya maonesho yenye eneo la mita za mraba elfu kadhaa kila moja.

Mbali na hayo ushirikiano wa kandarasi ya ujenzi wa miradi na nguvukazi pia unaimarishwa kwa mfululizo. Waziri wa biashara wa China Bw. Bo Xilai amesema, China ina imani kubwa kuhusu mustakabali wa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki.

Idhaa ya kiswahili 2006-12-19