Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-19 18:19:50    
Nchi za Ulaya na Marekani zarekebisha sera za uhamiaji

cri

Hivi sasa hapa duniani kuna wahamiaji kiasi cha milioni 200, na wahamiaji hao karibu wote wanaishi katika nchi zilizoendelea. Ghasia zilizotokea mwezi Oktoba mwaka jana huko Paris zilisababisha nchi za magharibi kutafakari suala la wahamiaji. Baada ya mwaka 2006 kuanza, nchi nyingi za Ulaya na Marekani zilianza kurekebisha sera zao kuhusu uhamiaji.

Mwezi Machi mwaka huu, wahamiaji na waungaji mkono laki kadhaa walifanya maandamano makubwa nchini Marekani wakipinga sheria ya "kupambana vikali na wahamiaji haramu", sheria ambayo ilipitishwa na Baraza la Chini la bunge la nchi hiyo. Kutokana na upinzani, sheria hiyo pamoja na sheria nyingine kuhusu wahamiaji haramu iliyopitishwa na Baraza la Chini la bunge la Marekani mwezi Mei, zote zilifutwa. Hata hivyo rais wa Marekani George W. Bushi alisaini amri ya kujenga ukuta wenye urefu wa maili 700 kwenye mpaka kati yake na Mexico, ili kuzuia wahamiaji wasiingie nchini Marekani. Rais Bush aliposaini amri hiyo alisema haifai kuwaruhusu wahamiaji haramu wajipatie uraia wa Marekani. Alisema,

"Haifai kuwapatia wahamiaji haramu uraia wa Marekani. Huu ni msamaha mkubwa kwa wahalifu na mimi napinga msamaha huo."

Wakati huo huo nchi za Ulaya pia zimechukua hatua mbalimbali dhidi ya wahamiaji. Serikali ya Ufaransa ilitangaza kuacha kabisa sera ya zamani ya kuwapokea wahamiaji bila mchujo, na kuanzia tarehe mosi Januari mwaka 2007 Ufaransa itaongeza vizingiti kwa wahamiaji na kuzidi kuwafukuza wahamiaji haramu. Hispania nchi ambayo iliwahi kuwasamehe mara nyingi wahamiaji haramu, mwezi Septemba mwaka huu pia ilitangaza kuwa itapambana na wahamiaji haramu na waajiri wa wahamiaji haramu. Serikali ya Uholanzi imeamua kuwakataa watu wasioweza kuongea Kiholanzi. Kutokana na idadi kubwa ya wahamiaji serikali ya Uingereza ilitangaza kuwa kuanzia mwezi Oktoba inawazuia wafanyakazi kutoka Romania na Bulgaria.

Kutokana matukio mengi yaliyofanywa na wahamiaji, nchi hizo za Ulaya na Marekani zimerekebisha sera zao kuhusu uhamiaji. Wahamiaji ni wanyonge katika jamii, na haki zao hazilindwi, kwa hiyo ni rahisi kwao kuonesha hasira kwa vitendo visivyo vya kawaida. Tokea ghasia zilizotokea mwezi Oktoba nchini Ufaransa, ghasia nyingine pia ziliendelea kutokea nchini humo.

Kwa upande mwingine, kutokana na utamaduni na dini tofauti na jamii ya nchi za Ulaya na Marekani, wahamiaji ni vigumu kujiunga na jamii ya nchi hizo, kwa hiyo watu wenye msimamo mkali wa kidini wanapata urahisi wa kupata magaidi kutoka nchi hizo. Watu walioongoza na kushiriki kwenye ghasia mbili zilizotokea hivi karibuni nchini Uingereza wote ni kizazi cha wahamiaji wa Asia ya Kusini. Hasira dhidi ya jamii miongoni mwa wahamiaji zinawatishia wenyeji wa nchi hizo. Isitoshe idadi kubwa ya wahamiaji imekuwa shinikizo kubwa kwa mfumo wa huduma za jamii na ajira, kwa hiyo inawaletea wenyeji usumbufu na kuwabagua.

Hapo awali nchi zilizoendelea zilikuwa wazi kwa wahamiaji kwa sababu zilikuwa na upungufu wa nguvu-kazi na ilihitaji watu hodari kutoka nchi za nje. Ni ukweli kwamba kutokana na juhudi kubwa za kazi, wahamiaji walitoa mchango mkubwa katika kuharakisha maendeleo ya nchi hizo na kuimarisha tamaduni za aina nyingi na maingiliano kati ya nchi na nchi. Baada ya rais Bush kusaini sheria ya kuwazuia wahamiaji kutoka Mexico, mhamiaji mmoja aliyeshiriki kwenye maandamano alisema,

"Sisi sio wahalifu, wengi kati yetu tumekuja kufanya kazi na kuishi hapa."

Nchi za Ulaya na Marekani pia zinatambua kwamba kama zikitaka kuwa na nguvu-kazi za kutosha na kuendeleza uchumi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, ni lazima ziwategemee wahamiaji. Kutokana na fikra hizo pamoja na kudhibiti wahamiaji pia zimechukua hatua za kuwapa faraja. Hivi sasa Ufaransa imekuwa ikifikiria kutunga sheria ya "haki sawa" kwa wenyeji na wahamiaji, na mwezi Oktoba imeunda "baraza la umoja wa jamii na haki sawa". Waziri mkuu wa Ufaransa Dominique de Villepin kwenye ufunguzi wa baraza hilo alisema,

"Mimi binafsi nazingatia sana mpango huo, baada ya ghasia za mwaka jana nilifikiria kuunda baraza hilo ili kusuluhisha mgogora wa kijamii."

Lakini suala la wahamiaji haliwezi kutatuliwa kwa siku moja. Wachambuzi wanaona kuwa nchi za Ulaya na Marekani zitaendelea kurekebisha sera zao ili kupata uwiano kati ya mahitaji ya nguvu-kazi na utulivu wa jamii.