Mwaka 2006 karibu unamalizika, mwaka huu hali ya eneo la mashariki ya kati lililokuwa na hali ya wasiwasi imezidi kuwa mbaya, mgogoro kati ya Lebanon na Israel ulitokea kabla ya mgogoro kati ya Palestina na Israel kutatuliwa, suala la nyuklia la Iran limekuwa donda ndugu, na mapambano kati ya makundi ya madhehebu ya kidini nchini Iraq yamekuwa makali siku hadi siku, migogoro hiyo imewatia watu wasiwasi kuhusu mustakabali wa sehemu hiyo.
"Damu inamwagika, hofu inatawala na utatanishi unaongezeka, hasa kwa watu wa Palestina wanaoishi katika hali hiyo ngumu ambayo serikali ya nchi yao haina mapato, haina fedha kwa ajili ya elimu, haina fedha kwa ajili ya mishahara kwa wafanyakazi wake, kuwapa ruzuku watu wasiokuwa na ajira. Watu wanaishi katika hali ya kufungwa kabisa."
Profesa wa siasa katika chuo kikuu cha Al-Quds cha Jerusalem Bwana Issa Ibu-Zuhairah aliyasema hayo alipojumuisha hali ya mashariki ya kati ya mwaka kwa mwaka huu unaomalizika. Katika uchaguzi wa bunge la pili la Palestina uliofanyika mwanzoni mwa mwaka huu, Kundi la Hamas ambalo lina msimamo mkali lililishinda kundi la Fatah na kuchukua madaraka ya utawala, na kuwekewa vikwazo na nchi za magharibi zikiongozwa na Marekani, hali hiyo imeongeza migogoro kati ya makundi mbalimbali nchini Palestina, na ni vigumu kuunda serikali ya mseto ya Palestina. Tarehe 28 Machi mwaka huu, Israel ilifanya uchaguzi mkuu wa duru jipya, Bw. Ehud Olmert alishika madaraka ya waziri mkuu badala ya mgonjwa Bw. Sharon, lakini serikali ya Israel inashikilia sera kali dhidi ya Palestina, na kufanya shughuli nyingi za kijeshi dhidi ya Palestina. Wakati huo katibu mkuu wa chama cha Hezbollah cha Lebanon Sheikh Hassan Nasrallah alitangaza kuwa:
"Tunataka kusema, mateka wa kivita wa Israel wako mikononi mwetu, kuna njia moja tu ya kuwarudisha nyumbani, yaani kufanya mazungumzo au kubadilishana mateka."
Tarehe 12 Julai, jeshi la chama cha Hezbollah cha Lebanon liliwakamata askari wawili wa jeshi la Israel, Israel ilianzisha kampeni kubwa ya kijeshi kwa ajili ya jambo hilo, na kutokea mgogoro kati ya Lebanon na Israel ulioitwa "vita ya 6 ya mashariki ya kati. Wachambuzi wameona kuwa, mgogoro huo si kama tu ni mapambano kati ya Israel na chama cha Hezbollah, bali pia ni mapambano ya kisirisiri kati ya pande tatu za Marekani, Syria na Iran. Daktari mmoja aliyefanya uchunguzi wa mkakati wa kimataifa wa chuo kikuu cha George Washington cha Marekani alidhihirisha kuwa:
"Marekani iliiunga mkono Israel kupambana na chama cha Hezbollah ikipuuza mwito wa jumuiya ya kimataifa wa kuitaka Israel isimamishe vita mara moja kwa makusudi ya kutumia nguvu kubwa za kijeshi za Israel kupambana na Syria na Iran, ili kutoa onyo kwa nchi hizo mbili zisiende kinyume na Marekani. Kwa Iran mgogoro kati ya chama cha Hezbollah na Israel utasaidia kuvutia ufuatiliaji wa Marekani kutoka kwa mpango wake wa nyuklia, na kupunguza shinikizo la jumuiya ya kimataifa kuitaka iache utafiti wa nyuklia."
Ingawa mgogoro kati ya Lebanon na Israel uliodumu kwa siku 34 umetulia kwa muda, lakini bado hakuna mchakato wa amani, matatizo kati yao bado hayajatatuliwa. Mgogoro kati ya Palestina na Israel, mapambano kati ya makundi ya madhehebu ya kidini nchini Iraq na suala la nyuklia nchini Iran yameleta utatanishi mkubwa kwenye mgogoro wa mashariki ya kati, pia imeonesha umuhimu wa kuhimiza mchakato wa amani wa mashariki ya kati kwa kufanya ushirikiano kati ya pande mbalimbali.
|