Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-20 18:31:12    
Elimu kuhusu kuanzisha shughuli katika chuo kikuu cha viwanda cha Tianjin

cri

Katika miaka ya hivi karibuni, idadi ya wanafunzi wa vyuo vikuu wa China imeendelea kuongezeka, na baadhi ya wanafunzi hao wanachagua kuanzisha shughuli zao wenyewe baada ya kuhitimu masomo ya vyuo vikuu. Lakini kutokana na kutokuwa na uzoefu na uwezo wa kutosha, baadhi yao walikumbwa na matatizo mbalimbali wakati wakijaribu kuanzisha shughuli zao . Ili kuwasaidia wanafunzi wa vyuo vikuu wa China kuinua uwezo wao wa kuanzisha shughuli zao, mwaka 2005 shirikisho la vijana la China likishirikiana na shirika la wafanyakazi la kimataifa la Umoja wa Mataifa, liliingiza mafunzo ya KAB (Know About Bussiness) yenye lengo la kuinua mtizamo na uwezo wa wanafunzi katika kuanzisha shughuli zao mbalimbali.

Chuo kikuu cha viwanda cha Tianjin ni moja kati ya vyuo vikuu vilivyoanza kutoa mafunzo ya KAB nchini China. Hivi karibuni mwandishi wetu wa habari alikwenda katika darasa la KAB katika chuo kikuu hicho. Tofauti na darasa la kawaida nchini China, meza za wanafunzi hazikupangwa kama kawaida, bali zinapangwa katika duara, wanafunzi 60 wanakaa pamoja kwa vikundi.

Katika darasa hilo, mwalimu alichukua kampuni moja ya kutengeneza samani kuwa kama ni mfano, na kuwaacha wanafunzi wajadiliane na kufanya uchambuzi kwa vikundi, na kuweka mpango wa maendeleo kwa kampuni hiyo. Mwanafunzi Wang Zheng alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, katika kikundi chake chenye wanafunzi 9, wanafunzi wanatoka michepuo mbalimbali. Wanafunzi wa sheria walitoa ushauri wa kisheria kwa maendeleo ya kampuni, wanafunzi wa mchepuo wa usanifu waliwaeleza wanafunzi wengine kuhusu umaalum wa bidhaa mpya, ili kusaidia kundi la wauzaji liweze kufahamisha vizuri zaidi bidhaa hizo mpya kwa wateja. Wang Zheng alisema kuwa darasa hilo lilimfanya ajisikie kama anashiriki kwenye ushindani wa biashara. Alisema:

"zamani niliwahi kushiriki kwenye mafunzo kama hayo, lakini kwa kawaida tulikuwa tunamsikiliza Profesa akitoa ufafanuzi tu, hivyo hatukuweza kujua kama tuna uwezo wa kuanzisha na kuongoza kampuni au la. Kwa kupitia mafunzo ya KAB, tunaweza kufahamu moja kwa moja kuhusu utaratibu wa usimamizi na uendeshaji wa kampuni, pia tunaweza kujua kama kuna uwezekano wa kuanzisha shughuli zetu binafsi au la."

Bw. Kou Shijun ni ofisa wa mradi wa mafunzo ya KAB katika chuo kikuu cha viwanda cha Tianjin, pia ni mmoja wa viongozi wa idara ya kuanzisha shughuli kwa wanafunzi. Alipozungumzia mafunzo ya KAB, Bw. Kou Shijun alisema, mafunzo hayo yanawasaidia wanafunzi kufahamu mbinu na ustadi unaohitajika katika kuendesha kampuni, kama vile namna ya kushughulikia nguvu kazi na namna ya kusimamia mambo ya fedha. Hizo ni mbinu muhimu na za lazima kwa wanafunzi wa China ambao wanafahamu vizuri nadharia mbalimbali, lakini bado wanakuwa hawana uwezo wa kutenda kazi halisi. Bw. Kou Shijun alisema:

"wanafunzi wa vyuo vikuu vya China wanafahamu vizuri nadharia mbalimbali, lakini bado hawana uwezo wa kutosha kutenda kazi halisi. Ili kutatua suala hilo, chuo kikuu chetu kiliwahi kujaribu kutoa mafunzo mbalimbali husika, lakini bado mafunzo hayo hayakuwa na mpango kamili. Mafunzo ya KAB yanawafahamisha wanafunzi kuhusu mambo halisi katika uendeshaji wa kampuni. Kuingiza mafunzo ya KAB kumekamilisha zaidi utaratibu wa elimu ya kuanzisha shughuli katika chuo chetu, pia yametufundisha mfumo wa kisasa wa elimu duniani."

Hivi sasa chuo kikuu cha viwanda cha Tianjin kimepitisha uchunguzi wa shirika la wafanyakazi la kimataifa, na kimekuwa kituo rasmi cha elimu ya KAB kwa wanafunzi. Mwalimu Sun Juan kutoka chuo cha uhasibu ni mwalimu mwenye uzoefu wa elimu ya usimamizi. Alipata uthibithishaji wa sifa za ufundishaji wa KAB baada ya kupita kwenye mafunzo yaliyoandaliwa na shirika la wafanyakazi la kimataifa mwezi Machi mwaka huu. Mwalimu Sun Juan alieleza kuwa utaratibu wa mafunzo ya KAB umebadilisha utaratibu wa kawaida wa kufundisha kwa maelezo, na mafunzo hayo yanashirikisha wanafunzi wote kwenye mawasiliano ya masomo. Mwalimu Sun Juan alisema:

"tofauti kubwa ni kwamba mafunzo ya KAB yanafuata utaratibu wa mawasiliano kati ya walimu na wanafunzi darasani. Zamani walimu walikuwa wanafundisha na wanafunzi walikuwa wanasikiliza. Lakini mafunzo ya KAB yanatumia njia mbalimbali kama vile michezo au majadiliano kuwapatia wanafunzi moyo wa kufanya kazi kwa umoja. Tunaunda kikundi mara kwa mara kwa ajili ya kutatua suala tofauti. Vikundi hivyo ni kama makampuni, wanafunzi wanajadiliana kwanza namna ya kushughulikia masuala mbalimbali sokoni, kisha mwalimu atawajumuisha na kufikia maoni ya pamoja."

Baada ya kuzungumza na wanafunzi kadhaa, mwandishi wetu wa habari anaona kuwa wanafunzi wa China wana uwezo wa uvumbuzi na hamu kubwa ya kuanzisha shughuli zao wenyewe. Mafunzo ya KAB yanawapatia wanafunzi ujuzi wa kimsingi na uwezo wa kufanya mazoezi, na kuwawekea msingi mzuri wa kuanzisha shughuli zao.

Mwezi Machi mwaka 2006, waziri mkuu wa China Bw. Wen Jiabao alisema katika ripoti ya serikali kuwa, China inapaswa kuharakisha ujenzi wa nchi inayofanya uvumbuzi, kuinua kikamilifu uwezo wa uvumbuzi na kutekeleza sera bora za ajira. Mafunzo ya kuinua mtizamo wa wanafunzi kuanzisha shughuli si kama tu yanaonesha mustakabali wa uvumbuzi wa vijana wenye umaalum, bali pia yanaweza kupunguza shinikizo la ajira. Mradi wa elimu ya KAB kwa wanafunzi wa vyuo vikuu umefanya jaribio lenye manufaa la elimu kuhusu kuanzisha shughuli, pia ni msukumo wa kuinua uwezo wa uvumbuzi na kujiajiri kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya China.