Rais George Bush wa Marekani tarehe 20 kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye Ikulu ya Marekani alisisitiza kuwa, Marekani inapaswa kuongeza nguvu ya jeshi linalofanya mapambano nchini Iraq, na kumwagiza waziri wa ulinzi wa Marekani Bwana Robert Gates atoe mapendekezo kuhusu jinsi ya kuongeza askari nchini Iraq. Bw. Gates aliyefanya ziara nchini Iraq siku hiyo alijadiliana na maofisa wa jeshi la Marekani nchini Iraq kuhusu uwezekano wa kuongeza wanajeshi nchini Iraq. Vyombo vya habari vimedhihirisha kuwa, kutokana na hali mbaya ya Marekani nchini Iraq, sera mpya ya serikali ya Bush kwa Iraq itatolewa haraka.
Vyombo vya habari vya Marekani vimesema lengo la kwanza la sera hiyo ya serikali ya Bush ni kutatua tatizo la usalama la Iraq, halafu kuelekea kwenye mchakato wa kisiasa wa Iraq, kuisaidia serikali ya Iraq kutimiza lengo la kujilinda, kujimudu na kujiendeleza. Hivyo kuongeza askari kumekuwa ni chaguo la kwanza la rais Bush katika kutatua tatizo la usalama nchini Iraq. Wachambuzi wanaona kuwa, kuna sababu mbili kwa Rais Bush kutoa kipaumbele kuongeza wanajeshi nchini Iraq:
Kwanza, hivi sasa wanajeshi wa Marekani walioko nchini Iraq hawawezi kudhibiti hali ya huko, migogoro ya kimabavu nchini Iraq inaongezeka siku hadi siku. Hivyo watu wengi kutoka jeshi la Marekani wanapendekeza kuongeza wanajeshi nchini Iraq, wanaona kuwa jukumu la kwanza la jeshi la Marekani nchini Iraq ni kulinda usalama wa raia wa huko, kuzuia mgogoro kati ya makundi ya madhehebu ya kidini kwa kuongeza idadi ya wanajeshi kwenye eneo wanakoishi kwa pamoja waislamu wa madhehebu ya Suni na madhehebu ya Shia. Watu hao wamedhihirisha kuwa, baada ya watu wanaoipinga serikali ya Iraq kushindwa, hatua ya maafikiano ya kikabila iliyotolewa na serikali ya Iraq itaanza kufanya kazi. Kuongeza wanajeshi wa Marekani nchini Iraq kutasaidia kutuliza hali ya Iraq ili kuweka mazingira mazuri kwa serikali ya Iraq kufanya umuhimu wake.
Pili, Kuongeza wanajeshi nchini Iraq kwa muda hakupata upinzani mkubwa nchini Marekani, hasa kikundi cha utafiti wa suala la Iraq la bunge la Marekani kilichokosoa sana sera ya Bush kwa Iraq kilisema, kama mkuu wa jeshi la Marekani nchini Iraq anaona kudhibiti hali ya Iraq kunahitaji askari wengi zaidi, basi kutuma wanajeshi wengine nchini Iraq kutaleta ufanisi .
Habari zinasema waziri wa ulinzi wa Marekani Bwana Gates aliyeshika madaraka siku chache zilizopita, tarehe 20 Desemba alifanya ziara ghafla nchini Iraq kwa lengo la kujadiliana na maofisa wa jeshi la Marekani nchini Iraq kuhusu uwezekano wa kuongeza askari na majukumu ya askari hao watakaotumwa. Maofisa hao hawakupinga pendekezo la kuongeza askari nchini Iraq, lakini wana wasiwasi kuwa, kuongeza wanajeshi kunamaanisha kuwa askari wengi zaidi wa Marekani watakuwa shabaha ya wanamgambo wa Iraq.
Watu wote wanaounga mkono pendekezo la kuongeza askari nchini Iraq wanaona kuwa, Marekani kuongeza askari nchini Iraq ni sehemu moja tu katika kutatua suala la Iraq, mkakati wa Marekani kwa Iraq hatimaye unapaswa kubadilika kwa suala la kisiasa, kiuchumi na kidiplomasia la Iraq. Wamedhihirisha kuwa baada ya kutulia kwa hali ya Iraq, serikali ya Iraq inatakiwaa kufanya umuhimu wake zaidi, jeshi la Iraq linatakiwa kushiriki katika shughuli nyingi za kijeshi, wakati huo huo Marekani inatakiwa kuongeza nguvu katika ukarabati wa Iraq, na kutoa nafasi nyingi zaidi za ajira kwa watu wa Iraq.
Rais George Bush alisema serikali yake itashirikiana na chama cha Republican na chama cha Democratic kuhusu suala la Iraq, kusikiliza maoni ya pande mbalimbali, kurekebisha sera yake kwa Iraq kutokana na hali halisi ya Iraq. Ofisa wa Ikulu ya Marekani alisema, Rais Bush atatangaza rasmi mkakati wake mpya wa Iraq mwanzoni mwa mwaka kesho.
Idhaa ya kiswahili 2006-12-21
|