Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-21 16:19:16    
Ziara ya mwandishi wa habari wa BBC mkoani Guangdong, China

cri

George Arney ni mwandishi wa habari wa BBC. Mwezi Oktoba mwaka huu, yeye na waandishi wa habari wenzake karibu 10 walitembelea Guangdong, mkoa uliopo kusini mwa China. Katika ziara hiyo ya siku 11, Bw. George alipata picha mpya kuhusu China ambayo ni tofauti kabisa na ile aliyekuwa nayo kabla ya kuja China, kiasi kwamba alipomaliza ziara hiyo alisema, ujuzi wake kuhusu China kweli ni mdogo sana.

"Sasa tuko katika China Bara. Garimoshi tulilopanda sasa hivi liliingia katika China Bara kutoka Hong Kong ya China, kwa hiyo linakwenda kwa polepole. Tunaifahamu sana Hong Kong, ambako kuna mabasi ya ghorofa na magazeti yanayotoa maneno makali. Lakini je, tunaifahamu China Bara iliyo nje ya garimoshi letu? Sijui. Hebu tuangalie ziara hii itaendelea vipi."

Hii ndiyo ripoti aliyoandaa Bw George akiwa ndani ya garimoshi linaloingia China Bara kutoka kwa mkoa wa utawala maalumu wa Hong Kong. Katika ziara hiyo, George alikuwa anawasiliana na ofisi ya BBC kwa mara 3 kila siku, akitoa maelezo kuhusu aliyoiona China.

Bw. George amefanya kazi ya uandishi wa habari kwa miaka 25, katika kipindi hicho, alitembelea nchi na sehemu mbalimbali duniani, lakini hii ilikuwa ni mara yake ya kwanza kutembelea China. Kama ilivyo kwa wageni wengi wasiofahamu China, George alikuwa na shaka kubwa kwa China inayoendelea kwa kasi.

Dada Zheng Yun ni mkalimani aliyemsaidia George katika ziara hiyo huko Guangdong. Alisema "George alionekana ni sawa na wenzake wa kundi hilo la waandishi wa habari wa kigeni, sura aliyo nayo kuhusu China ni kuhusu China ya miaka 60 na 70 ya karne iliyopita, alikuja China akiwa na maswali na wasiwasi mkubwa."

Bw. George pia alikuwa na shauku ya kuifahamu China. Akimkuta kwa mara ya kwanza mkalimani wake Dada Zheng Yun, alitoa maswali mbalimbali, kama vile "Je, wewe ni mtoto pekee wa familia yako? Una pato la kiasi gani? Una pesa za kununua makazi? Unapaswa kulipa fedha kiasi gain kwa ajili ya elimu? Unazifahamu nchi za magharibi? Unakata tamaa kuhusu mustakabali wako wa maisha?" Mkalimani huyo alimwelezea George kuwa, Wachina wanapata habari kwa wakati hali ambayo inafanana na ile katika nchi za magharibi, Wachina pia wanasikiliza nyimbo za Ulaya na Marekani, kutazama filamu za Hollywood, na kupata habari za dunia kwa kupitia radio, televisheni na mtandao wa Internet. George hakuridhika na majibu hayo.

Lakini baada ya kutembelea miji ya Guangzhou, Shenzhen na Dongguan, ambayo ni miji inayofanana na miji mingine ya kusini ya China, George alipata ufahamu mpya kuhusu China. Alisema "Nilipata habari kuhusu maendeleo makubwa ya kiuchumi ya China, kwani suala hili linazungumzwa sana katika nchi za magharibi. Hata hivyo nilishangazwa na nilivyoshuhudia. Huko Shenzhen, kuna majengo yenye ghorofa nyingi na majengo mengine hodari, sikuwahi kuangalia picha ya namna hii, kweli nilishangazwa sana."

Licha ya maendeleo ya uchumi wa China, mambo mengine yaliyomo kwenye mpango wa matembezi ya George yalikuwa sera ya uzazi wa mpango, hatua za kushughulikia uchafuzi wa mazingira na elimu ya vyuo vikuu. Mwandishi wa habari huyo wa BBC alitembelea shule na makazi ya Wachina wa kawaida, akiongea na maofisa wa serikali, wanaviwanda, wanafunzi wa vyuo vikuu na wanamichezo.

Katika shule moja ya msingi, George alifurahia kuona kuwa watoto walikuwa wanaweza kuongea naye kwa Kiingereza.

Katika nyumba ya mzee Li Yongyuan, ambaye ni mkazi wa kawaida wa mji wa Guangzhou, George alishuhudia ukarimu wa watu wa China. Mzee Li mwenye umri wa miaka zaidi ya 80 alikumbusha akisema "Ni fahari kwetu kumkaribisha rafiki wa Uiingereza. Mjukuu wangu anafahamu Kiingereza, alizungumza sana na Bw. George. Pia tulibadilishana zawadi. Nilimpa zawadi ya picha iliyochorwa kwa mtindo wa Kichina, ambayo ina maneno ya Kichina isemayo 'natakia urafiki kati ya China na Uingereza uendelee'."

George pia alithamini sana nafasi hiyo ya kuwatembelea Wachina kwenye nyumba yao. Alieleza maoni yake kuwa, "Kitu kilichonigusa sana ni mambo yanayofanana kati ya binadamu. Nilipozungumza nao kwa moyo wa kawaida, niligudua kuwa watu wanafanana katika mambo mengi, ama watu wa magharibi, Wachina, Wajapan au Warussia, hii haihusiani na mfumo wa kisiasa na utamaduni."

Baada ya ziara hiyo ya siku 11, mkalimani Zheng Yun aliona kuwa George amepata sura mpya kuhusu China. Alisema "Maendeleo ya kiuchumi yaliyopatikana huko Guangdong yalimshangaza sana George. Akishuhudia China alipata ufahamu kuhusu China ya kweli, ziara hiyo ilimfanya abadilishe maoni kuhusu China."

Ziara hiyo ilipomalizika, Bw. George alisema siku nyingine atarudi China, kuongea na Wachina wengi zaidi na kupata ufahamu mwingi zaidi kuhusu China.

Idhaa ya kiswahili 2006-12-21