Michezo ya 15 ya Asia ilifungwa tarehe 15 huko Doha, mji mkuu wa Qatar. Wachezaji zaidi ya elfu kumi kutoka nchi na sehemu 45 walishiriki kwenye michezo hiyo na kugombea medali 424 za dhahabu. Nchi na sehemu 26 zilipata medali za dhahabu na nchi na sehemu 38 zilipata medali. Ujumbe wa China ulishika nafasi ya kwanza kwa kupata medali 165 za dhahabu, medali 88 za fedha na medali 63 za shaba. Korea Kusini na Japan zilishika nafasi ya pili na ya tatu. Michezo ya 16 ya Asia itafanyika mwaka 2010, mjini Guangzhou, China.
Halmashauri ya Olimpiki ya kimataifa IOC na kamati ya maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya Beijing BOCOG tarehe 17 ilithibitisha hoteli mbili zenye nyota tano ziwe makao makuu ya IOC katika kipindi cha michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008. Hoteli hizo mbili ni Beijing Hotel na Grand Hotel Beijing. Katika kipindi hicho maofisa wa IOC na halmashauri za Olimpiki za nchi na sehemu mbalimbali watakaa katika hoteli hizo, ambako pia yatakuwa ni makao makuu na kituo cha uendeshaji cha IOC.
BOCOG tarehe 15 ilianza kazi ya kutangaza zabuni kwa ajili ya vituo vya huduma vya muda kwenye viwanja na majumba 31 ya mashindano na viwanja na majumba 15 ya mazoezi ya michezo ya Olimpiki ya Beijing. Ofisa wa BOCOG alisema kuwa vituo hivyo vitajengwa kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya michezo hiyo kabla ya kufunguliwa kwake na kubomolewa baada ya mashindano. Vituo hivyo ni pamoja na makambi, vibanda, majukwaa ya kuwekea mitambo ya televisheni, viti vya watangazaji wa televisheni, viwanja vya muda vya kuegesha magari na njia za muda. Kazi hizo zilianza tarehe 15 mwezi Desemba na zitamalizika tarehe 8 mwezi Januari mwakani.
Fainali kuu ya mashindano ya marudio ya kulipwa ya mwaka 2006 ya shirikisho la mpira wa meza la kimataifa ilifanyika tarehe 16 hadi tarehe 17 mkoani Hong Kong, China. Timu ya China ilitwaa ushindi kwenye michezo minne yote. Mchezaji wa China Wang Hao alimwangusha mchezaji maarufu wa Korea Kusini Oh Sang Eun na kupata medali ya dhahabu kwenye mchezo wa wanaume mmoja mmoja.
Fainali kuu ya mashindano ya tuzo kuu ya dunia ya kuteleza kwenye barafu kwa vitendo mbalimbali ilifanyika tarehe 16 mjini St. Petersburg, Russia. Wachezaji wa China Shen Xue na Zhang Hongbo walipata medali ya dhahabu kwenye mchezo wa kuteleza kwa vitendo mbalimbali kwa mwanamke na mwanamume.
Kwenye robo fainali ya mashindano ya ubingwa wa snuka ya Uingereza ya mwaka 2006 iliyofanyika tarehe 13, mchezaji wa China Ding Junhui alifungwa na mchezaji maarufu wa Uingereza Peter Ebdon na kushindwa kutetea ubingwa huo.
Idara ya michezo ya mji wa Shanghai tarehe 15 ilitoa taarifa ya upimaji wa ubora wa afya za wakazi wa mji huo kwa mwaka 2005. Taarifa hiyo inaonesha kuwa ikilinganishwa na mwaka 2000, ubora wa afya za raia wa mji wa Shanghai umeimarishwa kidhahiri. Taarifa hiyo inachambua kuwa kufanya mazoezi ya kujenga mwili ni sababu muhimu ya kuimarishwa kwa ubora wa afya za wakazi hao.
Fainali ya mashindano ya kombe la dunia ya klabu ya FIFA ya mwaka 2006 ilifanyika tarehe 17 mjini Yokohama, Japan. Timu ya Internacional ya Brazil iliifunga goli moja timu ya Barcelona ya Hispania na kupata ubingwa.
Idhaa ya kiswahili 2006-12-21
|