Mkutano wa kipindi cha pili wa duru la tano la mazungumzo ya pande sita uliingia katika siku ya tatu tarehe 20 mwezi Desemba. Msemaji wa ujumbe wa China Bibi Jiang Yu alisema, mazungumzo ya sasa yamepata baadhi ya maendeleo, lakini suala muhimu zaidi ni kufikia msimamo wa namna moja. Tarehe 20 alasiri, waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Li Zhaoxing alipokuwa na mazungumzo pamoja na viongozi wa ujumbe wa nchi mbalimbali zinazoshiriki katika mazungumzo ya pande 6, alisema, anaamini kuwa pande mbalimbali zinazoshiriki katika mazungumzo ya pande 6 zitaweza kuyafanya mazungumzo ya sasa kupiga hatua halisi. "Bw. Li Zhaoxing alisema, kutokana na juhudi za wajumbe wanaoshiriki kwenye mazungumzo hayo, wameweza kuafikiana kwenye mambo mengi mapya; Pande zote zimesisitiza kutekeleza 'taarifa ya pamoja ya tarehe 19 Septemba'; Zimesisitiza kutaka kutatua suala la nyuklia la peninsula ya Korea kwa njia ya mazungumzo, na kutimiza lengo la pamoja la kuifanya peninsula ya Korea iwe sehemu isiyo na silaha za nyuklia. Inatarajiwa kuwa pande mbalimbali zitatumia busara ya kisiasa na uvumbuzi, kuongeza uaminifu na maoni yanayofanana. China itajitahidi kuimarisha mawasiliano na ushirikiano na pande mbalimbali na kuhimiza mazungumzo hayo yapate maendeleo zaidi."
Katika mazungumzo yao viongozi wa ujumbe wa pande mbalimbali walisema, kufanyika upya mazungumzo ya pande 6 ni hatua muhimu, pande mbalimbali zinatakiwa kujitahidi zaidi kuondoa tofauti zilizopo na kuhimiza mazungumzo hayo yapige hatua halisi. Pande mbalimbali hizo zinapongeza mchango muhimu uliotolewa na China, ambayo ni nchi mwenyeji wa mazungumzo katika kuzindua upya na kuhimiza mazungumzo hayo yapate maendeleo mapya.
Kiongozi wa ujumbe wa Korea ya Kusini Bw. Chun Yung Woo alisema, katika mazungumzo yaliyofanyika siku zilizopita, Korea ya Kusini iliwasiliana mara kwa mara na pande nyingi zinazoshiriki kwenye mazungumzo hayo, kupunguza migongano na tofauti kati yao. Alisema Korea ya Kusini itajitahidi zaidi katika siku za baadaye ili kufanikisha mazungumzo hayo. Alisema, "Katika mikutano ya siku hizo, pande mbalimbali zimeona vyanzo vya migongano yao."
Kiongozi wa ujumbe wa Japan katika mazungumzo hayo, Bw. Kenichiro Sasae alisema pande zote zinaona kuwa, ni muhimu sana kupiga hatua katika mazungumzo hayo. Alisema, "Pande zote zinaona ni kitu cha lazima sana kupata maendeleo katika mazungumzo hayo, kwa hiyo mazungumzo hayo yataendelea kufanyika katika siku za baadaye. Japan inaona kuwa pande mbalimbali zingejadiliana zaidi kuhusu utekelezaji wa 'taarifa ya pamoja'."
Bw. Kenichiro Sasae aliongeza kuwa, "ili kutatua migongano iliyopo katika mazungumzo hayo, ninaona kuwa China ikiwa ni nchi mwenyeji licha ya kutakiwa kufuatilia maendeleo ya mazungumzo, inatakiwa pia kufikiria jinsi inavyoweza kuleta uwiano kati ya pande hizo."
Ingawa kulikuwa na migongano mikali kati ya pande hizo kuhusu baadhi ya masuala, lakini katika siku tatu zilizopita pande hizo zilikuwa na majadiliano kuhusu masuala hayo. Bibi. Jiang Yu anaona kuwa mazungumzo ya safari hiyo yamepata baadhi ya maendeleo.
Bibi Jiang Yu alisema, "hali ya hivi sasa inaonesha kuwa mazungumzo yamepata maendeleo: Kwanza, tumezindua upya mazungumzo ya pande 6; Pili, katika mazungumzo hayo pande zote zimesisitiza kuendelea kutekeleza 'taarifa ya pamoja ya tarehe 19 Septemba', kushikilia kutatua suala la nyuklia la peninsula ya Korea kwa njia ya amani, na pande zote zimesisitiza kutimiza lengo la kuifanya peninsula ya Korea iwe sehemu isiyo na silaha za nyuklia; na tatu, pande zote zimeeleza nia yao ya kuendeleza mazungumzo hayo."
Bibi Jiang Yu amesema, kitu muhimu zaidi kwa hivi sasa ni kwa pande zote kutekeleza ahadi zilizotoa katika taarifa ya pamoja na kushikilia msimamo wa 'vitendo kwa vitendo'.
|