Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-25 15:48:57    
Mtaalamu wa kuhifadhi Ukuta Mkuu nchini China Bw. Dong Yaohui

cri

Tangu tarehe mosi Desemba Sheria ya Kuhifadhi Ukuta Mkuu ilipoanza kutekelezwa rasmi, vitendo vyote vya kuchukua udongo, matofali au mawe, kupanda mimea, kuendesha vyombo vya usafiri kwenye Ukuta Mkuu vimepigwa marufuku. Sheria hiyo ilimfanya Bw. Dong Yaohui aliyejishughulisha na hifadhi ya Ukuta Mkuu kwa zaidi ya miaka 20 aone faraja kubwa.

Bw. Dong Yaohui mwenye umri wa miaka 50, ni naibu mwenyekiti wa Baraza la Ukuta Mkuu. Nyumbani kwake ni karibu na Ukuta Mkuu katika wilaya na Funing mkoani Hebei.

Ukuta Mkuu unasifiwa kama ni moja ya miujiza ya binadamu. Katika karne ya pili mfalme wa kwanza wa China Qin Shihuang aliunganisha kuta zote zilizojengwa na madola mbalimbali kwa ajili ya kuwazuia maaduni kuwa ukuta mrefu, na katika miaka zaidi ya elfu moja baadaye, kila enzi iliufanyia ukarabati na kuurefusha, hatimaye ukawa ukuta wenye urefu wa kilomita elfu kadhaa kutoka ukingo wa bahari upande wa mashariki hadi jangwani upande wa magharibi, baada ya kupita milima mingi. Katika urefu huo, ukuta wa Enzi ya Ming miaka 600 iliyopita, ulijejgwa kwa uhandisi wa hali ya juu zaidi na umebaki kikamilifu zaidi kutokana na hifadhi nzuri. Ingawa Bw. Dong Yaohui anaishi karibu na ukuta huo lakini alipokuwa mtoto hakutegemea kama siku moja angekuwa mtaalamu wa kuuhifadhi ukuta huo.

Bw. Dong Yaohui alikuwa mfanyakazi katika kiwanda cha umeme, asipokuwa kazini alipenda kupanda milima na kuandika makala za fasihi. Katika miaka ya 80 ya karne iliyopita alikuwa na hamu ya kuchunguza ukuta huo, kwa kushirikiana na wenzake wawili walianza safari yao wakiwa na mizigo mgongoni. Bw. Dong Yaohui alisema,

"Nilikulia chini ya Ukuta Mkuu, na nilipenda kupanda milima, niliuona ukuta huo mara nyingi mlimani, hatimaye nilikuwa na hamu ya kuuchunguza. Wakati huo kulikuwa na vitabu vichache sana kuhusu elimu ya ukuta huo, kutokana na nilivyokuwa na hamu kubwa zaidi ya kuufahamu ukuta huo, ndivyo nilivyoona shida zaidi kuvipata vitabu vyake. Nilifikiri litakuwa ni jambo la maana sana kama nikiwa mtu wa kwanza kuacha nyayo zangu kwenye ukuta huo mzima."

Bw. Dong Yaohui alisema ingawa yeye ni mfanyakazi wa kawaida, lakini ana msingi wa kuandika makala na aliwahi kuandika riwaya kadhaa. Baada ya kudhamiria kusafiri kufuata Ukuta Mkuu alitumia juhudi zote kwenye mandalizi ya kukusanya habari kuhusu ukuta huo.

Tarehe 4 Mei mwaka 1984 ilikuwa ni siku isiyosahaulika kwa Dong Yaohui. Baada ya maandalizi ya mwaka mmoja, Dong Yaohui pamoja na wenzake wawili walianza safari yao. Wakati huo alikuwa na umri wa miaka 28. Matatizo waliyopata safarini si rahisi kuyaeleza, walikuwa wanasafiri usiku na mchana kutoka mlima hadi mlima. Lakini, alisema, shida kubwa zaidi sio uchovu bali ni ukiwa uliowapata. Alisema,

"Hali ilivyo ni kwamba baada ya kuanza kusafiri, shida kubwa ilikuwa ni ukiwa unaotokana na kujitenga na jamii, jamaa na marafiki na kila siku kusafiri milimani pasopo na mtu."

Bw. Dong Yaohui na wenzake walisafiri kwa siku 508, walipita miji na wilaya zaidi ya mia moja, mwishowe walikamilisha safari yao. Mafanikio yao yalitangazwa, na tokea hapo Bw. Dong Yaohui ameanza kufanya kazi inayohusiana na Ukuta Mkuu.

Mwaka 1985, Bw. Dong Yaohui alijiunga na Chuo Kikuu cha Beijing na kufundishwa na profesha Hou Renzhi, ambaye ni mtaalamu wa hostoria na jiografia. Katika kipindi chake cha masomo pia aliwasiliana na wataalamu na wasomi wengine kuhusu elimu ya Ukuta Mkuu na aliwahi kushiriki kwenye Baraza la Ukuta Mkuu. Mbali na hayo, aliratibu kumbukumbu alizoandika wakati wa safari yake na baadaye alichapicha kitabu chake cha "Uchunguzi kuhusu Ukuta Mkuu" kwa kushirikiana na wengine. Kitabu hicho kinaeleza kipande kwa kipande mazingira ya ukuta, jinsi ukuta ulivyojengwa na hali ya sasa ya hifadhi. Hatimaye alichapisha vitabu vya "Safari katika Ukuta Mkuu", "Mkusanyiko wa Makala za Dong Yaohui kuhusu Ukuta Mkuu" na kitabu cha "Masuala Kadhaa ya Nadharia ya Kimsingi kuhusu Ukuta Mkuu". Vitabu hivyo vimekuwa na taathira kubwa nchini China na katika nchi za nje.

Mwaka 1995, Bw. Dong Yaohui kwa nyakati tofauti alikuwa katibu mkuu wa Baraza la Ukuta Mkuu na alikuwa naibu mkuu wa baraza hilo. Kutokana na juhudi zake kubwa, alianzisha harakati nyingi za hifadhi ya Ukuta Mkuu na kutaka kutungwa kwa sheria. Kutokana na kilio cha miaka mingi, katika nusu ya pili ya mwaka 2003 sheria kuhusu hifadhi ya Ukuta Mkuu ilianza kuandaliwa. Hivi sasa sheria hiyo imeanza kutekelezwa rasmi. Bw. Dong Yaohui alisema,

"Nilisoma habari nyingi kutoka kwenye magazeti kuhusu vitendo vya kuharibu Ukuta Mkuu na adhabu kuhusu vitendo hivyo hazikuwepo, hii ni hasara kubwa ya ukuta huo. Ukuta Mkuu ukiwa ni jengo lenye historia ya miaka mingi, linahitaji kuhifadhiwa kwa sheria. Baada ya kutangazwa kwa sheria hiyo, hakika itasaidia sana hifadhi ya ukuta huo."

Bw. Dong Yaohui alisema, hivi sasa theluthi moja ya ukuta huo imekarabatiwa na kuhifadhiwa vizuri, theluthi nyingine haipo katika hali nzuri, na theluthi iliyobaki imetoweka kabisa. Hifadhi ya ukuta huo imefikia wakati wa lazima. Ukuta Mkuu sio mali ya China tu bali ni mali ya wanadamu wote, ni alama ya ustaarabu wa binadamu. Alisema, atatumia uhai wake wote katika kazi muhimu ya kuhifadhi ukuta huo.

Idhaa ya kiswahili 2006-12-25