  
Tsunami kubwa iliyotokea tarehe 26 mwezi Desemba mwaka 2004 kwenye bahari ya Hindi karibu na Asia ya kusini mashariki na Asia ya kusini, ilisababisha vifo vya kiasi cha watu laki 2.2 wa nchi 11 za huko. Janga hilo kubwa lilitokea miaka 2 iliyopita, lakini nchi zote za Asia zilizokumbwa na maafa hayo bado zinakumbuka sana siku hiyo isiyo ya kawaida. Wakati wa kutimiza miaka miwili tangu kutokea kwa maafa ya tsunami, nchi hizo zilifanya shughuli nyingi, sio tu kwa kukumbuka watu waliopoteza maisha yao katika maafa, bali hasa ni kwa kuimarisha imani ya kujenga upya maskani yao yaliyoharibiwa na maafa hayo.
Indonesia ni nchi iliyoathiriwa vibaya zaidi na tsunami katika miaka 2 iliyopita, idadi ya watu wa nchi hiyo waliokufa katika maafa hayo ilichukua theluthi mbili ya jumla ya idadi ya watu waliokufa katika maafa hayo ya tsunami. Tarehe 26 shughuli za kuwakumbuka watu waliopoteza maisha yao katika maafa hayo pamoja na mazoezi ya kujilinda zilifanyika katika sehemu mbalimbali za nchi hiyo. Nchini Sri lanka na India, shughuli za maadhimisho zilifanyika kidini, washiriki walikumbuka watu waliopoteza maisha yao katika maafa na kuwafariji wafiwa na jamaa zao. Nchini Thailand nusu ya idadi ya watu waliokufa katika maafa hayo walikuwa watalii kutoka nchi za magharibi, kwa hiyo shughuli za kumbukumbu zilifanyika kwa jadi ya nchi za magharibi: watu walinyunyiza maua baharini, kuwasha mishumaa kwenye ukuta wa makumbusho na kurusha maputo kwenye sehemu ya makaburi kwa kuonesha huzuni yao.
Hivi sasa miaka miwili imepita tangu maafa ya tsunami yatokee, sekta ya utalii ilikuwa sekta iliyorejeshwa kwanza katika nchi zilizokumbwa na maafa ya tsunami. Tunachukua Thailand kama mfano, baada ya kutokea kwa tsunami mwishoni mwa mwaka 2004, sekta ya utalii kwenye kisiwa cha Phuket nchini Thailand iliathiriwa vibaya, idadi ya watalii ilipungua kwa nusu na pato kutokana na utalii lilipungua kwa zaidi ya theluthi mbili. Hivi sasa hali inabadilika kuwa nzuri siku hadi siku. Makadirio yaliyofanywa katikati ya mwezi Desemba na kituo cha utafiti cha benki ya wakulima ya Thaihua, ambacho ni kituo kinachojulikana sana kwa uchunguzi wa mambo ya kiuchumi nchini Thailand, yanaonesha kuwa kwa kufuata kiasi cha vyumba vya hoteli na tikiti za ndege zilizoagizwa hivi sasa, katika majira ya baridi ya mwaka huu, sekta ya utalii ya Phuket itakuwa na hali nzuri zaidi, idadi ya watalii itaongezeka kwa zaidi ya 87% kuliko siku za kawaida, na pato la sekta ya utalii litafikia dola za kimarekani bilioni 1.8.

Kufufuka kwa sekta ya utalii kunamaanisha kuwa mawasiliano na huduma kwa watalii vimerejea katika kiwango cha kabla ya kutokea kwa maafa ya tsunami, na pia ni maendeleo ziliyoyapata nchi zilizoathiriwa na maafa ya tsunami katika ujenzi wa miundo-mbinu. Kuhusu kujenga mfumo wa kutoa utabiri na tahadhari kuhusu maafa ya tsunami, nchi hizo zinajitahidi kuanzisha utafiti. Mwanzoni mwa mwezi Desemba, mfumo wa kwanza wa kutoa onyo kuhusu tsunami umetumika rasmi kwenye ufukwe wa bahari wa Phuket, wakati nchi nyingine ikiwemo Indonesia zimejenga minara ya kuchunguza, ving'ora vya onyo na mabango ya kuwaelekeza watu njia ya kukimbia ili kutoa misaada kwa watu kabla ya tsunami kufika kwenye sehemu za fukwe.
Mbali na kufufua uchumi na kujikinga na maafa mapya, kupanga watu walionusurika katika maafa pia ni moja ya majukumu muhimu. Hivi karibuni gazeti la the Nation nchini Thailand lilichapisha makala kwenye ukurasa wa kwanza wa gazeti hilo yenye kichwa "Baada ya tsunami, maisha yanaendelea". Mara tu baada ya kutokea maafa ya tsunami mwaka ule, jumuiya ya kimataifa ilitoa misaada mingi, na michango ya fedha iliyoahidiwa na nchi mbalimbali ilifikia dola za kimarekani bilioni 13.6. Lakini hadi hivi sasa michango mingi iliyoahidiwa bado haijatolewa au fedha za baadhi ya michango zimetumika kwa mambo mengine, hivyo matumaini ya watu wengi walionusurika katika maafa ya kuishi maisha mazuri mapya bado hayajaweza kutimizwa.
Maafa makubwa ya tsunami yaliyotokea mwishoni mwa mwaka 2004, yalifanya watu milioni 2 kukosa makazi, leo baada ya miaka miwili kupita, baadhi ya watu hao wamehamia kwenye makazi mapya kutokana na misaada ya serikali za nchi mbalimbali na jumuiya ya kimataifa, lakini bado kuna watu wengi wanaishi katika vibanda vya kawaida wakisubiri misaada ya kimataifa. Tunachukua tena mfano wa Thailand, vyombo vya habari hivi karibuni vilitoa habari kuwa kiasi cha 60% ya fedha za misaada ya maafa ya tsunami na fedha za ujenzi mpya zilitumika kwa matumizi mengine au kutumiwa vibaya. Kutokana na maombi ya Marekani, Umoja wa Ulaya na jumuiya ya kimataifa, polisi ya Thailand itafanya uchunguzi mkali kuhusu matumizi ya fedha za misaada iliyotolewa kwa ajili ya kupunguza athari ya maafa.

Idhaa ya Kiswahili 2006-12-26
|