Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-27 16:53:08    
Idadi ya askari wa Marekani waliouawa katika vita vya Iraq imezidi idadi ya watu waliokufa katika "tukio la Septemba 11"

cri

Jeshi la Marekani tarehe 26 lilitangaza kuwa askari wengine sita waliuawa nchini Iraq, na kuifanya idadi ya askari wa Marekani waliouawa katika vita vya Iraq vilivyoanzishwa mwaka 2003 ifikie 2,977, ambayo ni watu wane zaidi kuliko idadi ya watu waliokufa katika "tukio la Septemba 11". Idadi hiyo iliyotangazwa katika likizo ya siku ya Krismasi, iliwafanya watu wa Marekani kupoteza furaha ya Krismasi. Wachambuzi wanaona kuwa hali ya wasiwasi na idadi ya askari waliouawa nchini Iraq imekuwa usumbufu mkubwa kwa serikali na watu wa Marekani.

Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya vifo na kuwa na matatizo katika kufanya maamuzi yanayohusiana na vita, serikali ya George W. Bush aliyeanzisha vita hivyo inakabiliwa na shinikizo kubwa. Mwezi Machi mwaka 2003 serikali ya Bush ilianzisha vita vya Iraq na kuupindua utawala wa Saddam bila kujali upinzani wa jumuyia ya kimataifa na Umoja wa Mataifa.

Lakini ukweli ni kwamba baada ya kupekua sana nchini Iraq jeshi la Marekani lilishindwa kugundua "silaha kali" ambazo kilikuwa ni kisingizio chake cha kuanzisha vita. Kisingizio kingine cha serikali ya Bush kuanzisha vita dhidi ya Iraq ni kuwa serikali ya Sadddm ilihusika moja kwa moja na "tukio la Septemba 11" lililofanywa na kundi la Al Qaida, lakini hadi sasa serikali ya Bush haijapata ushahidi wowote, kwa hiyo si ajabu hata kidogo kwa chama cha upinzani cha Demokrasia kuipinga sana serikali hiyo, watu wa chama hicho wanasema hakuna ushahidi wowote ambao unaweza kuhusisha vita vya Iraq na "tukio la Septemba 11". Vita vya Iraq kwa kiasi kikubwa vimegawa nguvu za Marekani za kupinga ugaidi na hata kiongozi wa kundi la Al Qaida anaendelea kuwepo kama kawaida.

Ingawa serikali ya Bush inajikaza kwa kusema kwamba jeshi la Marekani limekuwa linaelekea kwenye ushindi au litapata ushindi, lakini kutokana na kukabiliwa na matukio ya kuuana kati ya madhehebu ya kidini nchini Iraq serikali ya Bush haikuwa na budi ila kumwondoa madarakani waziri wa ulinzi Donald Rumsfeld, mtu aliyesanifu vita hivyo.

Ripoti ya "kikundi cha utafiti wa matatizo ya Iraq" iliyotolewa mwanzoni mwa mwezi huu inasema "hali ya Iraq ni mbaya na inazidi kuwa mbaya kila kukicha". Waziri mpya wa ulinzi wa Marekani Bw. Robert Gates kwenye mkutano wa bunge alisema moja kwa moja kwamba jeshi la Marekani halijapata ushindi katika vita vya Iraq. Kutokana na kukabiliwa na ukweli uliopo, rais Bush tarehe 18 kwa mara ya kwanza alikiri kuwa jeshi la Marekani halikupata ushindi katika vita vya Iraq. Kutokana na shinikizo kubwa hata waandishi wa habari walimwuliza rais Bush, je, unaweza kupata usingizi usiku?

Watu wa Marekani wamezidi kufahamu nini wanacholetewa na vita vya Iraq. Uchunguzi wa maoni uliotangazwa tarehe 18 ulionesha kuwa kiasi cha uungaji mkono kwa rais Bush kimeshuka hadi kufikia 28%, kiasi ambacho ni chini kuliko wakati wowote wa hapo kabla, na kiasi cha kuipinga serikali ya Bush kimeongezeka hadi kufikia 70%.

Uchunguzi uliotolewa hivi karibuni unasema watu wa Marekani wamekuwa wanasumbuliwa vibaya na vita vya Iraq, kati ya watu walioulizwa, wengi wanaona kuwa haifai kwa Marekani kuondoka nchini Iraq, lakini huku wanaona fedha zinazotumika katika nchi hiyo ni nyingi sana yaani kwa upande mmoja wanaona inafaa kwa Marekani kurudisha askari wake kutoka Iraq, na kwa upande mwingine wana wasiwasi na vurugu kubwa zinazoweza kutokea baada ya askari kuondolewa. Idadi ya askari waliouawa nchini Iraq iliyozidi idadi ya watu waliokufa katika "tukio la Septemba 11" imewafanya wawe na wasiwasi zaidi na wasiwe na msimamo kuhusu vita vya Iraq.

Serikali ya Bush hivi karibuni itatangaza sera zake kuhusu vita vya Iraq, lakini wataalamu wamesema serikali ya Bush haitakuwa na chaguo zuri, kwa hiyo hata kama sera zitabadilika, mustakbali wa Marekani kuhusu vita vya Iraq utakuwa mbaya tu.

Idhaa ya Kiswahili 2006-12-27