Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-27 19:40:10    
Teknolojia za upashanaji wa habari za China zang'ara kwenye maonesho ya upashanaji wa habari duniani

cri

Maonesho ya upashanaji wa habari duniani ya mwaka 2006 yaliyoandaliwa na Umoja wa shughuli za mawasiliano ya habari duniani yalifungwa hivi karibuni huko Hongkong. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Maonesho hayo yakiwa ni maonesho makubwa kabisa ya teknolojia na vifaa vya upashanaji wa habari duniani, kufanyika nje ya makao makuu ya umoja huo mjini Geneva. Katika maonesho hayo yaliyofanyika kwenye eneo kubwa kabisa na kushirikisha makampuni mengi kabisa katika historia yake, teknolojia mpya za upashanaji wa habari za China hasa teknolojia ya mawasiliano ya simu ya mkononi ya 3G zilikuwa zinang'ara na kufuatliwa sana.

Katika maonesho hayo kampuni ya teknolojia ya upashanaji habari ya Datang ya China ilionesha maendeleo mapya ya teknolojia ya SCDMA. Watazamaji wanaweza kujaribu kutazama vipindi vya televisheni na kupiga simu ya video kwa simu ya mkononi ya TD-SCDMA. Hivi sasa teknolojia ya TD-SCDMA imeweza kutoa huduma za kupokea matangazo ya moja kwa moja ya televisheni na kutembelea mtandao wa Internet. Mkurugenzi mkuu wa bodi ya kampuni ya Datang Bw. Zhen Caiji alipotoa ufafanuzi kuhusu teknolojia hiyo katika maonesho hayo alisema:

"Teknolojia ya TD-SCDMA inatumia teknolojia maalum ya antenna, na inaweza kusimamia yenyewe matumizi ya mawimbi na uwezo wa upashanaji wa habari. Teknolojia hiyo inaweza kupunguza shinikizo la matumizi ya raslimali za mawimbi kwa makampuni ya huduma za simu. Lengo letu ni kutoa huduma bora na zenye bei nafuu za mawasiliano ya habari. Pamoja na teknolojia ya TD-SCDMA kutumiwa na kuenezwa nchini China, hakika itasukuma mbele maendeleo ya huduma ya 3G kote duniani."

Teknolojia ya juu inaweza kuonesha thamani yake wakati ikienezwa na kutumiwa na watu wengi. Imefahamika kuwa, teknolojia ya 3G itatumiwa katika huduma zinazotolewa na kampuni ya China Mobile. Naibu mkuu wa kampuni hiyo Bw. Li Yue alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema,

"simu ya mkononi ikiwa ni chombo chenye uwezo mkubwa, itafanya kazi muhimu zaidi katika maisha ya watu. Kwa mfano wakati maafa ya dharura yakitokea, tunaweza kuwaarifu watumiaji wa simu kuondoka kwenye sehemu zenye hatari, huduma kama hizo zina mustakabali mzuri."

Bw. Li Yue alisema ili kutimiza malengo hayo, kampuni ya China Mobile itaimarisha zaidi ujenzi wa mtandao, kuinua ubora wa huduma za mawasiliano ya habari, ili kuboresha huduma ya mawasiliano ya habari. Waziri wa upashanaji wa habari wa China Bw. Wang Xudong alisema, katika miaka miwili ijayo, China itafanya upimaji mbalimbali kuhusu teknolojia ya 3G na kutandika mtandao wa mawasiliano, ili kuweza kutoa huduma za 3G kwa wakazi wa Beijing ifikapo mwaka 2008.

Mbali na teknolojia ya 3G inayofuatiliwa sana katika maonesho hayo, makampuni ya China pia yalionesha teknolojia nyingine mpya, ikiwemo teknolojia ya IPTV, yaani teknolojia ya televisheni ya mtandao wa internet. Teknolojia hiyo inatoa huduma ya teknolojia ya kitarakimu, hata watumiaji wanaweza kutumia teknolojia hiyo kuagiza vipindi vya televisheni kwa hiari na kutembelea kwenye mtandao wa Internet.

Kampuni ya upashanaji wa habari ya ZTE ya China ni kampuni ya kwanza nchini China kutoa huduma ya IPTV na broadband kwa wateja wa kimataifa. Naibu meneja mkuu wa idara ya shughuli za mtandao ya kampuni hiyo Bw. Huang Dabin alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema,

"teknolojia hiyo imepanua teknolojia ya televisheni, tunachanganya teknolojia ya IPTV pamoja na huduma za mawasiliano ya sauti, usimamizi kwa video, michezo ya mtandao wa Internet, na huduma nyingine za mawasiliano kupitia Internet. IPTV si huduma ya televisheni peke yake tu, bali ni huduma kamili ya multimedia, televisheni ni sehemu tu ya huduma hiyo."

Kuwa na teknolojia muhimu kwa utafiti wa kujitegemea ni lengo linalofuatiliwa kwa makampuni ya teknolojia za upashanaji wa habari ya China. Katika sherehe ya ufunguzi wa maonesho hayo, spika wa bunge la umma la China Bw. Wu Bangguo alisema, serikali ya China itaendelea kuongeza nguvu kuunga mkono uvumbuzi kwa kujitegemea katika sekta ya upashanaji wa habari ya China. Bw. Wu Bangguo alisema:

"serikali ya China itaongeza nguvu katika kuendeleza huduma mpya za upashanaji wa habari na kukuza soko lake, kuharakisha na kukamilisha utaratibu wa uvumbuzi wa teknolojia katika makampuni, kuimarisha uwezo wa uvumbuzi kwa kujitegemea, na kujenga kituo cha kisasa cha utafiti wa teknolojia za upashanaji wa habari; China pia itaendelea kukuza sekta muhimu za IC (Integrated circuit) na software, na kujitahidi kuendeleza teknolojia mpya za mwasiliano ya simu ya mkononi, mtandao wa Internet na televisheni ya kitarakimu."

Bw. Wu Bangguo pia alisema, China itaendelea kushikilia sera ya kufungua mlango, kuimarisha ushirikiano kati yake na nchi mbalimbali katika sekta ya mawasiliano ya habari. China inakaribisha wanaviwanda kutoka nchi au sehemu mbalimbali duniani kuwekeza nchini China, na kukaribisha makampuni ya kimataifa kuanzisha ushirikiano wa utafiti wa teknolojia na makampuni ya China. Serikali ya China italinda maslahi halali ya wawekezaji wa nje na hakimiliki za nchi mbalimbali kwa mujibu wa sheria, China pia itapambana kithabiti na vitendo vya kukiuka hakimiliki. Aidha, China inahamasisha makampuni makubwa ya China kuanzisha ushirikiano wa kibiashara na kiteknolojia wa kimataifa ili kutoa mchango kwa maendeleo ya sekta ya mawasiliano ya habari duniani.

Wasikilizaji wapendwa, mlikuwa mkisikiliza maelezo kuhusu teknolojia za upashanaji wa habari za China zang'ara kwenye maonesho ya upashanaji wa habari duniani. Asanteni kwa kutusikiliza. Kwaherini!

Idhaa ya Kiswahili 2006-12-27