Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-27 19:53:47    
Watu wanaoaambukiza virusi vya Ukimwi barani Afrika

cri

Katika mwaka wa 2005 pekee, inakadiriwa kuwa watu milioni 2 waliaga dunia, huku wengine wapatao milioni 15 wakiwa wamekufa toka ugonjwa wa Ukimwi ugunduliwe barani Afrika, kutokana na maambukizi ya virusi vya Ukimwi au maradhi yanayosababishwa na virusi hivyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na ugonjwa wa Ukimwi UNAIDS, kwenye maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani tarehe mosi mwezi Desemba kila mwaka, pamoja na kuimarishwa kwa juhudi za kukabiliana na tatizo hilo, katika muda wa miongo miwili iliyopita, nchi zilizoko Kusini mwa jangwa la Sahara, zimeathirika sana katika sekta za elimu, afya na uchumi kwa ujumla kutokana na ugonjwa huo.

Vilevile taarifa hiyo imeongeza kuwa katika sekta za kijamii na kiuchumi, ni kuwa wanawake ndio wanaoathirika zaidi, na hasa wale wanaoishi katika maeneo ya mashambani. Japokuwa takwimu zinaonesha kuwa kwa mwaka jana kasi ya maambukizi ya maradhi hayo ilipungua nchini Kenya kwa asilimia 6.1, kwa wanawake maambukizi yalipungua kuwa asilimia 7.7, ikilinganishwa na wanaume ambao ni asilimia 4.

Nalo Baraza la kudhibiti Ugonjwa wa Ukimwi nchini Kenya (NACC) limesema, huenda idadi kubwa ya wajawazito wenye virusi hivyo hawajaelimishwa vyema jinsi ya kujikinga kikamilifu, na hiyo ni sababu kubwa inayowafanya watoto wengi wazaliwe wakiwa wameambukizwa virusi vya Ukimwi. Takwimu zilizopatikana kutoka kwa Wizara ya Afya nchini humo zinaonesha kuwa, wajawazito wapatao milioni 1.4 wanahitaji ushauri na kufanyiwa upimaji wa virusi vya Ukimwi. Kati ya wanawake wajawazito wapatao laki 4 waliofanyiwa upimaji wa maambukizi ya virusi vya Ukimwi nchini humo, imedhihirika kuwa mmoja kati ya 10 huwa wameambukizwa virusi hivyo.

Hata hivyo habari nzuri zilizopatikana katika mapambano dhidi ya virusi hivyo ni kuwa, tangu mwaka 1996 serikali mbalimbali barani Afrika zimejitahidi kusambaza dawa zenye kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi, zinazofahamika kama ARVs katika vituo kadhaa vya afya.

Hata hivyo bado sio rahisi kwa serikali za bara hilo kusambaza dawa hizo kwa waathirika kutokana na kuzorota kwa miundo mbinu ya nchi hizo. Kwa kuwa wengi wa watu wanaougua ugonjwa wa Ukimwi huwa wanauguzwa na wanawake, hali hiyo inakwamisha kukua kwa uchumi, hasa ikizingatiwa kuwa wanawake ndio wenye hujitokeza na kujituma zaidi katika nyanja mbalimbali za uchumi.

Takwimu nyingine zilizotolewa katika siku za karibuni na UNADIS zinaonesha kuwa, Uganda ni nchi yenye idadi kubwa ya wajane waliofiwa na waume zao kutokana na Ukimwi.

Idhaa ya Kiswahili 2006-12-27