Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-28 16:38:45    
Watu wanaojitolea kulinda mito mama ya China

cri

Mito miwili, Huanghe na Changjiang ni mito mikubwa kabisa hapa nchini China. Tangu enzi na dahari, watu wa China walianza kukaa kando ya mito hiyo ambayo inajulikana kama mito ya mama ya China. Katika miaka ya hivi karibuni, viwanda mbalimbali vilijengwa kwenye kando ya mito hiyo miwili, ambavyo licha ya kuleta maendeleo ya uchumi, pia vimechafua maji ya mito hiyo. tokea mwaka 1999 harakati moja inayoitwa "operesheni ya kulinda mito mama" ilianza kutekelezwa nchini China. Harakati hiyo inawahamasisha vijana wengi wajishirikishe katika shughuli za kulinda mazingira ya mito na maziwa mbalimbali nchini China. Mwaka jana harakati hiyo ilipata tuzo ya "watetezi wa dunia" iliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza..

"Operesheni ya kulinda mito mama" ilianzishwa na kamati kuu ya Umoja wa vijana la chama cha kikomunisti cha China kwa kushirikiana na idara ya hifadhi ya mazingira ya China na idara nyingine. Harakati hiyo ina lengo la kulinda mazingira ya maeneo ya mtiririko wa mito ya China, ikiwemo mito ya Huanghe na Changjiang.

Mhusika wa harakati hiyo kutoka shirika la vijana la chama cha kikomunisti cha China Bw. He Junke alieleza kuwa, tangu ilipoanzishwa, operesheni hiyo ilikubaliwa na kufuatiliwa na watu wengi na imepata mafanikio. Alisema "Katika kipindi cha miaka 7 iliyopita, 'operesheni ya kulinda mito mama' ilikuwa inawashirikisha vijana na watoto milioni 350, kuchangisha Yuan milioni 380 kutoka nchini China na nje. Vilevile tulikamilisha miradi zaidi ya 200 ya kupanda miti katika maeneo ya mtiririko wa mito mikubwa ya China, ambapo eneo lenye hekta laki 2 na elfu 81 lilipandwa miti. Hatua hiyo ilifanikiwa kuboresha mazingira ya mito hiyo."

Dada Ma Xiuping ni mmoja kati ya vijana waliojitolea kushiriki kwenye harakati hiyo, yeye anaishi wilayani Datong, mkoani Qinghai, kaskazini magharibi mwa China, ambako ni sehemu ya mtiririko wa juu wa mto Huanghe. Katika miaka ya hivi karibuni, viwanda vya kutengeneza karatasi na kuyeyusha madini vilijengwa katika wilaya hiyo. Viwanda kadhaa vilitoa maji taka mtoni bila kuyashughulikia, jambo ambalo lilisababisha uchafuzi wa mto Beichuan, ambao ni tawi la mto Huanghe.

Dada Ma Xiuping ni mkaguzi wa mazingira wa kituo cha kukagua mazingira cha wilaya hiyo, kazi yake ni kufuatilia hali ya viwanda vinavyochafua mazingira. Alisema  "Mimi na wenzangu tunafuatilia viwanda vinavyotoa maji taka kwenye mto wa Beichuan. Tunapogundua kiwanda kinachochafua mazingira, tunafika kiwandani kwa wakati, ili tuzuie vitendo hivyo vya kutoa maji taka ovyo na kukitoza faini kiwanda hicho."

Kutokana na uingiliaji wa kituo cha ukaguzi wa mazingira cha wilaya hiyo, viwanda zaidi ya 10 vilifungwa au kuhamishwa. Hata hivyo dada Ma Xiuping hakuridhia na mafanikio hayo. Zaidi ya hayo alianzisha kikundika cha vijana waliojitolea kulinda mazingira ya mto wa Beichuan, alichangisha fedha za kupanda miti, pia aliandaa harakati mbalimbali za kueneza elimu ya kulinda mazingira.

Msichana huyo alieleza kuwa, anataka watu wengi zaidi wanaoishi kando ya mto Huanghe wafahamishwe kuwa, kulinda mto huo usichaliwe ni jambo muhimu sana. Alisema "Kulinda mto Huanghe si kama tu ni kwa manufaa ya maskani yetu, bali pia ni kwa lengo la kulinda dunia yetu, kwani kulinda mto wetu kunalingana na kulinda dunia yetu."

Vitendo vya dada Ma Xiuping na wenzake waliojitolea vilifuatiliwa sana na kuwaamsha watu wengi sana ambao wametambua umuhimu wa kuhifadhi mazingira. Hivi sasa wakazi wengi wa huko wanafanya kazi kwa hiari katika shughuli za kuhifadhi mazingira na kulinda usafi wa vyanzo vya Mto Huanghe.

Wilaya ya Dengkou ya mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani ipo katika sehemu ya mtiririko wa juu na katikati wa mto wa Huanghe, ambako pia kuna kikundi cha vijana wanaojitolea kulinda mto huo. Sehemu ya mto Huanghe yenye urefu wa kilomita 50 inapita kwenye wilaya ya Dengkou, ambayo sehemu kubwa ya ardhi yake imebadilika kuwa jangwa, kwa hiyo kila mwaka mchanga wenye uzito wa karibu tani milioni 70 unaingia kwenye mto Huanghe unapopita kwenye wilaya hiyo. Kutokana na kulimbikizwa kwa machanga, sehemu ya chini ya mto huo iko juu ya ardhi ya wilaya hiyo, hali ambayo inaufanya mto huo uonekane kama umetandikwa juu ya ardhi na kuleta hatari kubwa dhidi ya maisha ya wakazi wa huko na mali zao. Kutokana na hali hiyo, kupambana na jangwa na kulinda mazingira ya mto wa Huanghe ni kazi kuu ya wilaya hiyo.

Bw Gao Yong mwenye umri wa miaka 30 ni kiongozi wa kikundi cha vijana wanaojitolea cha wilaya ya Dengkou. Kijana huyo alisema azma yake ni kuwahamasisha vijana wengi zaidi wajishughulishe na kazi ya kuhifadhi mazingira. Kutokana na juhudi zake, vijana wa wilaya hiyo walianzisha kituo cha kukagua hali ya mazingira ya mto mama, ambacho siku zote kinafuatilia sifa ya maji ya mto na kiasi cha mchanga mtoni. Vijana hao pia wanapanda miti na majani kila mwaka ili kushughulikia sehemu ya jangwa.

Bw. Gao Yong alisema "Tulikodi sehemu ya jangwa na kuiendeleza kiuchumi, ambako tunapanda mazao yanayofaa yenye thamani kubwa za kiuchumi. Katika juhudi zetu za kulinda mto mama, kazi kuu ni kushughulikia mchanga usiingie kwenye mto Huanghe."

Hivi sasa shughuli za kupambana na jangwa wilayani Dengkou zimepata mafanikio. Kwa upande mmoja kiasi cha mchanga unaoingia kwenye mto Huanghe kimedhibitiwa vizuri, na kwa upande mwingine, wafanyabiashara wanaokodi sehemu za jangwa pia wamepata faida nzuri.

Idhaa ya kiswahili 2006-12-28