Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-28 16:36:40    
Wakhazak wapata uwezo kwa kuendeleza utalii wa aina ya kabila hilo

cri

Wakhazak ni miongoni mwa watu wa makabila 55 madogomadogo ya China. Kabila hilo ni kabila la wafugaji wanaohamahama, kwa hiyo Wakhazak wanatupa taswira ya watu wanaoambatana na farasi. Wakhazak wanamtumia farasi kama chombo cha mawasiliano, wanakula nyama ya farasi, kunywa pombe inayotengenezwa kwa maziwa ya farasi, na kutumia vitu vinavyotengenezwa kwa ngozi za farasi. Hivi sasa Wakhazak wanaokaa katika mkoa unaojiendesha wa kabila la Wauygur wa Xinjiang, kaskazini magharibi mwa China wamepata uwezo kwa kuendeleza utalii wa aina ya Kikhazak unaohusiana na farasi. Mwandishi wetu wa habari alipowatembelea watu hao hivi karibuni alifika kwenye mahema ya mfugaji Mkhazak Bw. Sahat ambaye alikuwa anaongea na rafiki yake mzee Ualbay, ambaye pia ni Mkhazak. Mzee huyo alikuwa akiimba wimbo aliotunga wakati huohuo kumkaribisha mgeni.

Mwandishi wa habari alikuwa akiburudishwa kwa wimbo huo huku akiangalia mapambo ya mahema hayo, kuta na sakafu zilikuwa zimetandikwa mablanketi yenye rangi mbalimbali. Mwenye mahema Bw. Sahat alimfahamisha kuwa, mahema hayo yalijengwa hasa kwa ajili ya shughuli za utalii, lakini kama hakuna watalii familia yake pia huwa inakaa huko. Bw. Sahat alieleza kuwa familia yake ilianza kujishughulisha na utalii miaka mitano iliyopita. Alisema "Nilianza kujishughulisha na utalii mwaka 2001. Kabla ya ukombozi, sisi wafugaji karibu sote tulikuwa tunaishi kwenye mahema. Na baada ya ukombozi sote tulihama milimani na kuanza kuishi kwenye nyumba zisizohamishika, ambako tulianza kujishughulisha na shughuli za kilimo. Katika majira ya siku joto, baadhi yetu tunachunga mifugo milimani na wengine kufanya shughuli za utalii."

Baada ya kuingia kwenye karne mpya ya 21, serikali ya huko iliamua sekta za ufugaji na utalii ziwe uti wa mgongo wa kuendeleza uchumi wa huko. Katibu wa kamati ya tawi la chama cha kikomunisti cha China kwenye wilaya hiyo Bw. Nasihat alimwambia mwandishi wa habari kuwa, "Tumeamua kuendeleza uchumi wa wilaya yetu kwa kutegemea sekta mbili za mifugo na utalii, ili kuinua maisha ya wakazi wa makabila mbalimbali. Katika sekta ya ufugaji, tunazingatia sifa za mifugo na kuingiza mifugo bora. Na kwa upande wa shughuli za utalii, tunajitahidi kuwahamasisha watu wa makabila mbalimbali wajishughulishe na utalii, ili wapate maendeleo kwa pamoja."

Bw. Sahat ni kati ya wafugaji wa kwanza walioitikia mwito wa serikali na kujishughulisha na utalii. Mafanikio yao yalitoa mfano kwa wakulima na wafugaji wengine, ambao pia walianza kushiriki kwenye uchumi wa utalii. Jamaa kadhaa wa Bw. Sahat pia walianza kujishughulisha na utalii kutokana na mafanikio yake.

Bw Sahat akikumbusha siku za mwanzo alipoanza kujishughulisha na utalii alisema, wakati huo utalii ulikuwa ni neno geni kwake, alivutiwa na habari kuhusu watu wa sehemu nyingi kuchuma pesa kutokana na shughuli za utalii. Lakini hakuamini kama kujishughulisha na sekta hiyo. Mwanzoni alitaka kufanya majaribio tu. Akisaidiwa na serikali, alianzisha makazi kwa ajili ya wageni. Baada ya utendaji wa miezi kadhaa tu, aliona kuwa mapato ya shughuli za utalii ni makubwa zaidi kuliko yale yatokanayo na shughuli za ufugaji.

Bw. Sahat alisema "Mwanzoni nilifuga kondoo kati ya 100 na 200, na kupata Yuan zisizozidi elfu 10 kwa mwaka. Lakini nilichuma Yuan zaidi ya elfu 20 katika kipindi cha miezi miwili tu ya Aprili na Mei kutokana na shughuli za utalii. Licha ya hayo kutokana na shughuli za utalii, sisi pia tunaweza kuwasiliana na watu wengi, kupata upeo wa mbali zaidi pamoja na mawazo mapya."

Katika miaka mitano iliyopita tangu aanze kujishughulisha na utalii, Bw. Sahat amepata uzeofu mkubwa. Ameona kuwa, wageni wanafurahia sana shughuli zinazohusiana na utamaduni maalumu wa kabila la Kikhazak, kwa mfano kupanda farasi, kunywa pombe iliyotengenezwa kwa maziwa ya farasi na kula nyama ya farasi.

Mzee Ualbay alisema "Kabla ya kuendeleza utalii, ilikuwa ni we wenyeji tu tuliokunywa maziwa ya farasi, tukichinja farasi, wenyewe tulikula nyama au kuwazawadia jamaa na marafiki, mazao hayo yalikuwa kwa ajili ya kujitosheleza tu badala ya kujipatia faida. Tulipoanza kujishughulisha na utalii, tulianza kuuza nyama za farasi na pombe ya maziwa ya farasi, hiyo ni aina ya vyakula vya kabila letu. Watalii wengi wanakuja wakitaka kupanda farasi. Kwa hiyo tunafuga farasi wengi zaidi ili watalii washuhudie maisha yetu ya kabila la wafugaji wanaohamahama. Baada ya kujishughulisha na utalii, farasi sasa ni chanzo muhimu cha mapato yetu."

Familia ya Bw. Sahat imepata uwezo kutokana na kujishughulisha na utalii, na hali ya maisha yao pia imeinuka. Hivi sasa familia hiyo imenunua motokaa mbili, zaidi ya hayo kila mwanafamilia ana simu ya mkononi.

Bw. Sahat alisema "Simu ya mkononi inanisaidia kupata wageni wengi. Kabla ya kuondoka kwao, wageni wananipigia simu ili niwaandalie vyumba, na hata matakwa yao ya chakula na mahitaji pia wananiambia kwa njia ya simu. Hii ni njia rahisi sana."

Katika nyumba ya Bw. Sahat, mwandishi wetu wa habari alikaribishwa kwa vyakula vya kabila la Wakhazak huku akiburudishwa kwa nyimbo za Wakhazak zilizoimbwa na mzee Ualbay.

Idhaa ya kiswahili 2006-12-28