Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-28 16:27:50    
Iran yakataa katakata azimio la baraza la usalama

cri

Tarehe 27 bunge la Iran lilipitisha azimio la kuihimiza serikali ya Iran "itimize mapema mpango wa nyuklia na kurekebisha mara moja sera kuhusu ushirikiano wake na shirika la kimataifa la nishati ya atomiki". Kabla ya hapo, tarehe 23 wakati baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilipopitisha azimio la Nam. 1737 serikali ya Iran ilikataa azimio hilo siku hiyo hiyo. Kutokana na jibu hilo la Iran, suala la nyuklia la Iran limevutia tena uangalifu wa jumuyia ya kimataifa.

Azimio lililopitishwa kwenye bunge la Iran tarehe 27 linasema, "serikali ya Iran inawajibika kusukuma mbele mpango wa nyuklia kwa ajili ya matumizi ya amani na kurekebisha mara moja sera kuhusu ushirikiano wake na shirika la kimataifa la nishati ya atomiki". Spika wa bunge la Iran Bw. Gholam Ali Haddad Adel baada ya azimio hilo kupitishwa alisema, kati ya wabunge 203, wabunge 161 walipiga kura za ndio. Na alisema, azimio hilo limeidhinisha serikali ya Iran iwe na haki ya kufikiria kujitoa kutoka kwenye mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia au kubaki kwenye mkataba huo na kufanya mazungumzo. Baada ya azimio hilo kupitishwa mara liliidinishwa na kamati ya usimamizi wa sheria ya Iran, na sasa azimio hilo linasubiri tu saini ya rais Mohamed Ahmadinejad na kuanza kutekelezwa baada ya siku 15 tangu lilipopitishwa.

Vyombo vya habari vya Ulaya vinaona kuwa azimio hilo ni uungaji mkono kwa msimamo wa serikali ya Iran kuhusu azimio la baraza la usalama. Katika siku ambayo azimio la Nam. 1737 lilipitishwa, wizara ya mambo ya nje ya Iran ilishutumu kwamba azimio hilo ni haramu, na Iran haitatekeleza. Rais wa Iran Bw. Ahmadinejad alisema, watu wa Iran hawatatishika na azimio hilo na wataendelea na mpango wa nyuklia na pia alisema, ni bora nchi za magharibi ziishi kwa amani na Iran ambayo itakuwa inamiliki teknolojia ya nyuklia, hatimaye mjumbe wa kwanza wa mazungumzo ya suala la nyuklia Bw. Ali Larijani alitangaza kuwa Ira itafunga mashinepewa 3,000 za kusafisha uranium. Naibu wa kwanza wa waziri wa mambo ya nje Bw. Mahdi Safari alisema Iran itatangaza kuzindua hatua ya kwanza ya kusafisha uranium kwa wingi katika mwezi Februari wakati itakapoadhimisha mwaka wa 28 wa ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu.

Kuna sababu nyingi kwa Iran kuchukua msimamo mkali kuhusu azimio la baraza la usalama. Kwanza, Iran siku zote inasisitiza kwamba lengo lake la kuendeleza mpango wa nyuklia ni matumizi ya amani, na kusema kwamba sababu ya Marekani kuishutumu Iran kuendeleza mpango wa silaha za nyuklia kwa kisingizio cha matumizi ya amani, inatokana na maslahi yake binafsi, na alisisitiza kwamba kuendeleza mpango wa nyuklia ni haki iliyopo kwenye "mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia", ni haki ya Iran isiyonyimika. Zaidi ya hayo hadi sasa shirika la kimataifa la nishati ya atomiki halijagundua ushahidi wowote wa kuthibitisha kuwa Iran imekwenda kinyume na kanuni za mkataba huo.

Wachambuzi wanaona kuwa ingawa azimio la baraza la usalama lilipokuwa katika mchakato wake lilikuwa na kauli tofauti, lakini limeonesha wazi nia ya jumuyia ya kimataifa kutoruhusu kuenezwa kwa silaha za nyuklia. Hili ni onyo kwamba Iran iendeleze mpango wake wa nyuklia kwa kiwango kinachofaa, la sivyo itatengwa na jumuyia ya kimataifa na kukabiliwa na adhabu kali.

Idhaa ya Kiswahili 2006-12-28