Tarehe 28 hali ya vita nchini Somalia ilibadilika, kwamba jeshi la serikali ya mpito ya Somalia liliingia mjini Mogadishu bila upinzani na kutangaza kuwa serikali hiyo itahamia mjini humo kutoka Baidoa, mji uliopo kusini mwa nchi hiyo.
Msemaji wa serikali ya mpito ya Somalia Bw. Abdirahman Dinari amethibitisha kuwa, muda mfupi kabla ya jeshi la serikali ya mpito kuingia mjini Mogadishu, vikosi vya kundi la Muungano wa Mahakama za Kiislamu vilikuwa vimeondoka mjini Mogadishu, na vikosi vya makabila mbalimbali vilivyokuwa vinaliunga mkono kundi la Muungano wa Mahakama za Kiislamu vimeweka silaha chini. Wakuu wa makabila mbalimbali walikuwa wamejitokeza mapema kusubiri nje ya mji huo kumkaribisha waziri mkuu wa serikali ya mpito Bw. Ali Mohamed Gedi. Katika siku hiyo Bw. Gedi alifanya mazungumzo na wakuu hao na kujadili ukabidhi wa madaraka ya mji wa Mogadishu. Katika siku hiyo kulitokea ghasia, kwamba baadhi ya watu walifanya unyang'anyi katika baadhi ya maduka, ghala la silaha na makazi ya maofisa wa kundi la Muungano wa Mahakama za Kiislamu, lakini serikali ya mpito ilituliza ghasia hizo haraka. Jioni ya siku hiyo serikali ya mpito ilitangaza kuwa mji mzima uko katika hali ya dharura. Msemaji wa bunge la Somalia alisema serikali ya mpito imeunda kamati ya kusimamia mji wa Mogadishu.
Tokea mwaka 2004 serikali ya mpito ya Somalia ilipoundwa, ilikuwa inahama hama kati ya mji mkuu wa Kenya Nairobi, mji wa Jowhar uliopo kilomita 90 kaskazini ya mji wa Mogadishu na hivi sasa inafanya kazi katika mji wa Baidoa, mji uliopo kilomita 250 kaskazini ya mji wa Mogadishu. Kuingia mjini Mogadishu kwa serikali ya mpito kuna maana ya wazi. Wachambuzi wamesema, hivi sasa serikali ya mpito ya Somalia inakabiliwa na masuala mawili, moja ni kupata uungaji mkono wa umma na pili ni kurudisha mazungumzo ya amani.
Katika siku hiyo baada ya kumaliza mazungumzo na wakuu wa makabila, waziri mkuu Bw. Ali Mohamed Gedi alisema, jeshi la serikali ya mpito litapangwa upya ili kudhibiti vilivyo hali ya Mogadishu, lakini "kudhibiti vilivyo" hakumaanishi kudhibiti kijeshi. Kabla ya mwezi Juni mwaka huu mji wa Mogadishu ulikuwa unadhibitiwa na vikosi vya makabila mbalimbali ambavyo vilikuwa vinapingana na kulingana kwa nguvu. Mwezi Juni vikosi vya kundi la Muungano wa Mahakama za Kiislamu viliuteka mji wa Mogadishu na vilidhibiti sehemu kubwa ya kusini ya nchi hiyo bila upinzani mkali. Vikosi hivyo vilipata uungaji mkono wa vikosi vya makabila mbalimbali kwa sababu licha ya kuwa vikosi vya kundi la Muungano wa Mahakama za Kiislamu vina nguvu kubwa zaidi, pia vinapata uungaji mkono wa watu wengi kutokana na kuwa baada ya vikosi vya kundi la Muungano wa Madhehebu ya Kiislamu kuuteka mji wa Mogadishu, vilifanya vitendo vingi mfululizo ikiwa ni pamoja na kurudisha sheria, utaratibu wa kijamii, kufungua viwanja vya ndege, magati, hospitali na shule. Sasa jeshi la serikali ya mpito limeingia mjini, suala la kwanza ni kupata uungaji mkono wa umma na kuufanya umma uikubali serikali hiyo.
Suala linginine ni kurudisha mazungumzo ya amani. Tarehe 22 Juni baada ya vikosi vya kundi la Muungano wa Mahakama za Kiislamu kuuteka mji wa Mogadishu viliwahi kufanya mazungumzo na serikali ya mpito huko Khartum na kusaini taarifa ya pamoja ya kukubali kusimamisha vitendo vya uadui. Lakini mazungumzo hayo yalivunjika kutokana na vikosi vya Ethiopia kuingia nchini Somalia na kusaidia serikali ya mpito. Baada ya jeshi la serikali ya mpito kuingia mjini Mogadishu rais wa serikali hiyo Bw. Abdullahi Yusuf mara alisema serikali ya mpito inaahidi kutatua mgogoro kwa njia ya amani. Pamoja na hayo Umoja wa Afrika na Muungano wa Nchi za Kiarabu pamoja na IGAD pia zilitangaza kuzihimiza pande zote zisimamishe vita na kuitaka serikali ya mpito ifanye mazungumzo ya amani kabla ya tarehe 15 Januari mwaka kesho. Hali ya mabadiliko ya vita hakika itachangia kusimamisha vita na kurejesha mazungumzo hayo.
Idhaa ya kiswahili 2006-12-29
|