Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-01 20:13:31    
Kumkumbuka msanii wa ngonjera ya kuchekesha, Ma Ji

cri

Tarehe 20 Desemba msanii mashuhuri wa ngonjera ya kuchekesha wa China Bw. Ma Ji ghafla alifariki mjini Beijing kutokana na mshtuko wa moyo akiwa na umri wa miaka 72. Bw. Ma Ji ni msanii aliyependwa sana na kujulikana kwa kila familia nchini China. Watu walipigwa na bumbuazi waliposikia habari ya kifo chake, na kwa njia moja na nyingine walieleza kuhuzunishwa na kifo chake.

Tarehe 20 Desemba habari ya kifo cha Ma Ji ilipotangazwa kwenye mtandao wa internet mara ikaenea, watu wengi walionesha huzuni zao kwa barua pepe. Moja ya barua pepe ilisema "Bw. Ma Ji alitumia maisha yake yote kwa ajili ya ustawi wa usanii wa ngonjera ya kuchekesha, namwombea alazwe pema peponi!", na barua pepe nyingine ilisema, "Tumepungukiwa na mchekeshaji mmoja hapa duniani na mlio wa kicheko umeongezeka huko peponi." Baadhi ya watu walikimbilia hospitali kuagana na mwili wake kwa heshima.

Msanii wa ngonjera ya kuchekesha Bw. Jiang Kun ni mwanafunzi wa Ma Ji, alipohojiwa na waandishi wa habari alikuwa akishughulika kupanga ukumbi wa maombolezo. Alisema,

"Watu wengi wamekuja hapa mara baada ya kusikia habari ya kifo chake, ikionesha kuwa Ma Ji alikuwa na nafasi kubwa mioyoni mwa watu. Unaona, waliopo hapa kuna wanafunzi wake, viongozi wake na mashabiki wake, wanatusaidia kupamba ukumbi wa maombolezo."

Miongoni mwa watu hao alikuwapo rafiki mkubwa wa Ma Ji ambaye pia ni msanii wa ngonjera ya kuchekesha, Bw. Yang Shaohua, alisema,

"Bw. Ma Ji ni mwaminifu na mpole, aliandika ngonjera zaidi ya 300 za kuchekesha, amechangia sana kustawisha ngonjera zetu, ametufungulia barabara pana katika maendeleo ya ngonjera nchini China."

Usanii wa ngonjera ya kuchekesha nchini China ulianzia mbali, lakini haukuwa usanii halisi hadi ilipofikia mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20. Mambo yanayozungumwa katika michezo ya ngonjera yanatokana na maisha ya kila siku na yanachekesha kwa kusifu au kudhihaki hali nzuri au mbaya kwenye jamii, ili kuwafundisha watu wakati wanapocheka. Katika muda wa nusu karne hivi Ma Ji alionesha na kutunga michezo ya ngonjera zaidi ya 300, na alionesha michezo yake karibu kila pembe ya China.

Mliyosikia ni sehemu ya ngonjera ya kuchekesha iitwayo "Urafiki" iliyozungumzwa na Ma Ji na Tang Jiezhong katika miaka ya 70, mada yake ni kuusifu urafiki kati ya China na Tanzania uliopatikana katika miaka ya ujenzi wa reli ya Tazara. Hadi sasa mchezo wa ngonjera ya "Urafiki" umekuwa na miaka 30, lakini watu wanakumbuka sana. Katika siku chache zilizopita wakati mkutano wa wakuu wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, watu walipozungumzia Afrika walikuwa aliutaja mchezo huo. Siku chache kabla ya kufa kwake alimwambia mwandishi wetu wa habari akisema,

"Nimekuwa mzee mwenye miaka 72, nitaondoka jukwaani, kwa kuwa nimejishughulisha na mchezo huo kwa maisha yangu yote, nitawasaidia wachezaji vijana kwa uzoefu wangu nilioupata kwa zaidi ya miaka 50, na nitaendelea kuandika michezo."

Ma Ji alizaliwa mwaka 1934 katika familia maskini, kutokana na maisha magumu, alipokuwa na umri wa miaka 14 alikuwa ameanza kufanya kazi katika kiwanda kimoja cha nguo mjini Shanghai. Baada ya China mpya kuasisiwa Ma Ji alikuwa mfanyakazi katika duka moja la vitabu mjini Beijing. Kutokana na tabia yake ya uchangamfu na kuvutiwa na maisha ya wakazi wa Beijing Ma Ji alionekana kuwa na kipaji cha usanii wa ngonjera ya kuchekesha. Kwa mfano, aliweza kuiga jinsi wachuzi wadogo walivyoimba walipotembeza biashara yao na kuiga lafudhi ya lahaja za sehemu mbalimbali za China.

Mwaka 1956 ulikuwa ni mwaka wenye mabadiliko ya maisha yake. Ma Ji alipata nafasi ya kuonesha uhodari wake katika mashindano ya michezo ya sanaa ya wenyeji, na alichaguliwa kuwa mchezaji wa kulipwa katika Kundi la Michezo ya Sanaa ya Kuongea na Kuimba katika Redio ya China, na alianza kufundishwa na kusaidiwa na msanii mkubwa wa ngonjera ya kuchekesha Bw. Hou Baolin. Alipokuwa na umri wa miaka 20 alikuwa anajulikana sana katika nyanja ya ngonjera ya kuchekesha.

Kutokana na athari ya utamaduni wa nchi za nje, kuanzia miaka ya 90 ya karne iliyopita michezo ya ngonjera ilikuwa imefifia, watu waliweza tu kuburudika na michezo hiyo katika tamasha la kila mwaka la kusherehekea sikukuu ya mwaka mpya wa Kichina. Ni katika miaka ya karibuni tu ndio michezo ya aina hiyo imefufuka tena, mashindano ya michezo ya ngonjera yaliyofanyika hivi karibuni katika kituo cha televisheni yaliwavutia washabiki wengi. Ingawa Ma Ji alikuwa mzee lakini aliendelea kuzingatia ustawi wa michezo ya ngonjera. Alisema,

"Naona uhai wa michezo ya ngonjera unategemea kuonesha maisha hasa tuliyo nayo, ama sivyo usanii wa ngonjera hauwezi kustawishwa na kuwavutia watazamaji."

Ma Ji ni msanii mkubwa wa michezo ya ngonjera, ni mtu mpole na mwaminifu, watu wanapozungumza naye huhisi wako karibu naye kama marafiki wa zamani. Katika siku za mkutano wa wakuu wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika Ma Ji alisema anataka kuandika ngonjera kuhusu hifadhi ya mazingira baada ya kutembelea Afrika. Ingawa Ma Ji ameaga dunia, lakini daima atakumbukwa na Wachina.