Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-03 18:44:09    
Kwa nini Iran kuchukua msimamo mkali katika suala la nyuklia

cri

Rais Mahmud Ahmadinejad wa Iran tarehe 2 Januari alisema Iran itaendelea na mpango wake wa nyuklia, na azimio lililopitishwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuiwekea vikwazo Iran ni la haramu. Siku hiyo msemaji wa serikali ya Iran alisema kama nchi za magharibi zinashikilia kuishinikiza Iran katika suala la nyuklia, huenda Iran itajitoa kutoka kwenye mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia. Wachambuzi wamefafanua sababu kadhaa ni kwa nini Iran inaendelea kuwa na msimamo mkali katika suala la nyuklia:

Kwanza kuchukua msimamo mkali ni njia inayotumiwa na Iran katika kushughulikia uhusiano kati yake na jumuiya ya kimataifa. Tangu rais Ahmadinejad aingie madarakani mwezi Oktoba mwaka 2005, malumbano kati yake na jumuiya ya kimataifa hasa nchi za magharibi kuhusu suala la nyuklia yameongezeka haraka. Mwaka 2006, Iran ilirejesha shughuli za kusafisha uranium, kutangaza kufanikiwa kusafisha uranium nzito, kuanzisha kinu cha maji mazito na kuongeza mashinepewa. Kila mara mazungumzo kati yake na nchi sita za Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Marekani, China na Russia yalipoingia katika wakati muhimu, au kukabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Iran ilikuwa inalegeza msimamo kidogo. Hii imeonesha kuwa, Iran haiwezi kulegeza msimamo wake katika suala la nyuklia bali ni kwa ajili ya kuvuta wakati.

Pili, kuchukua msimamo mkali ni jibu la Iran kwa hali ilivyo ya kimataifa. Baada ya kupitishwa kwa azimio No. 1737 kwenye baraza la usalama, vyombo vya habari vya kimataifa havikutoa maoni mengi, kwa sababu vimeona kuwa azimio hilo halitakuwa na nguvu kwa suala la nyuklia la Iran, na hatua za vikwazo pia hazitakuwa na athari kubwa kwa Iran. Hivi sasa teknolojia na uwezo wa Iran wa kutumia nyuklia umeingia katika kiwango cha kiasi fulani. Baada ya kutangaza kufunga mashinepewa 3000, shughuli za Iran za kusafisha uranium zitaingia katika kipindi cha kuendeleza nyuklia kwa kiwango kikubwa, hivyo Iran kamwe haitaacha kwa urahisi mpango wake wa nyuklia. Iran inaona kuwa Marekani imezama kwenye matope nchini Iraq, haiwezi kuanzisha vita nyingine dhidi ya Iran wakati huo. Mbali na hayo nchi sita za Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Marekani, China na Russia hazina msimamo wa aina moja katika suala la nyuklia la Iran kutokana na maslahi yao tofauti, hali hii imeipa Iran nafasi fulani.

Tatu, mpango wa nyuklia ni maslahi ya kimsingi ya Iran, ili kuhakikisha inatimiza mpango huo, Iran hata imeamua kuwa tayari kujitoa kutoka kwenye mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia. Mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia ni mkataba muhimu katika kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia, wakati nchi zilizosaini mkataba huo zina haki ya kutumia nishati ya nyuklia kwa njia ya amani, pia unazitaka nchi hizo zikaguliwe na shirika la nishati ya atomiki duniani. Lakini mkataba huo una dosari kubwa, yaani haukuweka hatua za kuziadhibu nchi zitakazojitoa kutoka kwenye mkataba huo. Mwishoni mwa karne iliyopita, India na Pakistan zilifanya majaribio ya mabomu ya nyuklia baada ya kujitoa kutoka kwenye mkataba huo, Korea ya kaskazini pia ilifanya majaribio ya nyuklia baada ya kujitoa kutoka kwenye mkataba huo. Nchi hizo zote hazikuwekewa vikwazo vikali na jumuiya ya kimataifa, hivyo Iran huenda itaiga mifano hiyo.

Nne, kuchukua msimamo mkali ni njia moja ya Bw Ahmadinejad kujipatia uungaji mkono wa wananchi wake. Kwenye uchaguzi wa mabunge ya mikoa uliofanyika muda si mrefu uliopita, serikali ya Bw Ahmadinejad ambayo haijapata mafanikio makubwa katika mambo ya ndani, haikupata uungaji mkono mkubwa. Kwa hivyo Bw Ahmadinejad anatumai kujipatia uungaji mkono zaidi kwa kuendeleza mpango wa nyuklia. Hivi sasa Iran bado haijaonesha dalili ya kulegeza msimamo wake katika suala la nyuklia, hivyo pande husika zitakuwa na malumbano makali kuhusu suala hilo.