Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-04 15:11:20    
Lugha ya Kitatar yasaidia kupokezana kwa utamaduni wa kabila la Watatar

cri

Miongoni mwa waislamu wanaoishi katika mkoa unaojiendesha wa kabila la Wauygur wa Xinjiang, China, Watatar ni kabila lenye watu wachache zaidi kuliko makabila mengine. Kabila hilo sasa lina watu elfu 6 hivi, ni kabila dogo kati ya makabila madogomadogo yapatayo 55 ya China. Licha ya kuwa na watu wachache, kabila la Watatar linajivunia mafanikio yaliyopatikana katika kuhifadhi utamaduni na lugha yao. Zaidi ya hayo, hakuna Mtatar mzima hata mmoja asiyejua kusoma wala kuandika. Mafanikio hayo yanatokana na desturi ya Watatar ya kutoa kipaumbele kwa elimu, hasa mafunzo kwa watoto ndani ya familia.

Mzee Ilyar mwenye umri wa miaka 72 amekuwa anajishughulisha na sekta ya elimu kwa miaka yote iliyopita. Mzee huyo anaishi mjini Yining, mkoani Xinjiang. Katika sebule ya nyumba ya mzee Ilyar, mwenye nyumba alielezea mengi kuhusu suala la elimu. Alisema "Ingawa hivi sasa bado hakuna shule inayofundisha lugha ya Kitatar, tumefanikiwa kudumisha lugha na utamaduni wa kabila letu. Lakini Je, watoto wetu wanapata elimu hiyo wapi? Wanapata elimu hiyo kutoka kwenye familia zao. Kwa mfano, watoto wadogo wenye umri wa miaka mitatu au minne, wanakuwa bado hawajaanza kwenda shule, lakini wanaongea lugha ya Kitatar na kufahamu lugha hiyo."

Mzee Ilyar alisema, kwa maoni yake anaona kila kabila linapaswa kujua kwamba, lugha na utamaduni ni utambulisho muhimu kwa kabila hilo, kwa hiyo watu wanapaswa kurithi na kuendeleza lugha na utamaduni wa kabila lao. Mzee Ilyar alifunga ndoa alipokuwa na umri wa miaka 50, mke wake ni wa kabila la Wauzbek. Wana watoto wawili mmoja msichana na mwingine mvulana. Ili kuwafundisha watoto, mama Ilyar alijifunza lugha ya Kitatar, na bwana wake aliamua kila mwanafamilia aongee lugha ya Kitatar nyumbani.

Binti wa mzee Ilyar, dada Ilfira sasa anasoma kwenye kitengo cha menejimenti ya utalii cha chuo kikuu cha Xinjiang. Msichana huyo ana kipaji kweli, anafahamu kuongea lugha sita, zikiwa ni pamoja na Kitatar, Kichina, Kiuygur, Kikhazak, Kirussia na Kiingereza. Mbali na hayo sasa anajifunza lugha ya Kijapan. Dada Ilfira alifafanua ni kwa nini alijifunza lugha nyingi hivyo, kwamba anataka kujishughulisha na sekta ya utalii kuwahudumia wageni wanaotoka kwenye nchi mbalimbali. Dada huyo alisema "Majirani zetu ni wa kabila la Wauygur, ambao hawafahamu Kitatar. Nyumbani kwetu, mama na baba waliamua lazima nizungumze nao kwa lugha ya Kitatar. Nakumbuka kuwa tangu Nilipokuwa mtoto, nikizungumza na baba kwa lugha ya Kiuygur, alikuwa hajibu kabisa."

Mzee Ilyar alieleza kuwa, kabila la Watatar lina desturi ya kutoa kipaumbele kwa elimu. Alitoa mfano wa usemi unaosema kuwa, penye Watatar pana shule. Alisema iwapo hakuna shule katika mahali fulani, Watatar wanajitokeza na kuanzisha shule moja. Zaidi ya hayo, katika utamaduni wa Watatar, watoto wa kike wana nafasi sawa na wa kiume katika shughuli za elimu.

Bw. Habudulah Bubin ni mtaalamu wa elimu wa kabila la Watatar, yeye alisema mama asiyejua kusoma wala kuandika anashindwa kuwalea watoto hodari, kwa hiyo mama ni mtu wa kwanza ambaye angepata elimu. Mwaka 1915 shule ya kwanza ya watoto wa kike Watatar ilianzishwa mkoani Xinjiang, shule hiyo iliwapokea watoto wa kike wanaotoka kwenye makabila ya Watatar, Wauygur na Wakhazak.

Katibu mkuu wa taasisi ya utamaduni ya kabila la Watatar Bw. Haizatula Ainiwar alieleza kuwa, kutokana na sera ya makabila madogomadogo iliyotungwa na kutekelezwa na serikali ya China, hasa sera ya kuunga mkono maendeleo ya makabila madogomadogo yenye watu wachache, Watatar walianza kueneza lugha na utamaduni wao kwa kutegemea nguvu ya jamii nzima. Tokea mwaka 2002, taasisi hiyo ilianza kuandaa madarasa ya kufundisha lugha ya Kitatar huko Yining. Bw. Haizatula alisema  "Madarasa hayo yanafanyika wakati wa likizo ya majira ya baridi, siku joto na siku za mapumziko ili yasiathiri masomo ya watoto shuleni. Madarasa hayo ni sehemu ya juhudi za kutekeleza katiba ya nchi yetu, ambayo inasema makabila yote yana haki ya kupata elimu kwa kutumia lugha na fasihi zao. Sera ya makabila madogomaodog ya China inatusaidia sisi Watatar tuweze kurithi na kuendeleza lugha na fasihi zetu."

Imefahamika kuwa madarasa hayo yanawavutia watu wengi, wakiwemo wazee wa umri wa zaidi ya miaka 60, watoto wadogo wenye umri wa miaka 6 na wazazi wao. Bw. Haizatula alieleza maoni yake kuwa, wazazi wa watoto wakitambua umuhimu wa lugha na fasihi za kabila lao, wakifahamu vizuri lugha na fasihi hizo, ndipo watakapoweza kujifunza na kufahamu lugha na fasihi hizo nyumbani kwao.

Juhudi za kabila la Watatar kuendeleza lugha na utamaduni wao zimepata mafanikio yanayojulikana na kusifiwa na jumuiya ya kimataifa. Mwezi Februari mwaka 2003, mzee Ilyar aliizuru Jamhuri ya Dagestan, nchini Russia kutokana na mwaliko, ambapo alikutana na rais Shamilov wa Jamhuri hiyo. Rais Shamilov alifurahia maelezo ya mzee Ilyar kuhusu jinsi Watatar wanavyoishi huko Ili, China wanavyohifadhi lugha na utamaduni wao, akikubali Watatar wawatume watoto hao hodari waende kupata elimu ya juu katika Jamhuri ya Dagestan bila malipo.

Mbali na lugha, kutokana na juhudi za Watatar, sikukuu ya Saban ambayo ni sikukuu ya jadi ya kabila hilo pia inaanza kujulikana duniani. Sikukuu hiyo inafanyika tarehe 22 Juni, na inawavutia wageni wengi kutoka nchi za kigeni. Mzee Ilyar alisema "Nchi 5 za Asia ya Kati na Jamhuri ya Dagestan ya Russia zinafurahia sikukuu hiyo, na wageni wanaokuja kushiriki kwenye sikukuu hiyo pia wanaogezeka mwaka hadi mwaka. Mwaka 2006, rais wa Jamhuri ya Dagestan alituma wajumbe watatu kusherehekea sikukuu hiyo."

Idhaa ya kiswahili 2007-01-04