Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-04 15:22:17    
Mashujaa wanaopenda kuogelea maziwani wakati wa siku za baridi

cri

Mji wa Changchun upo mkoani Jilin, kwenye sehemu ya kaskazini mashariki ya China, ambako katika majira ya siku za baridi halijoto ya sehemu hiyo ina wastani wa nyuzi chini ya sifuri. Mkoa huo wa Jilin ni mmoja kati ya mikoa yenye halijoto ya chini kuliko mingine ya China. Tangu miaka ya 60 na 70 ya karne iliyopita, wakazi kadhaa wa mji wa Changchun walianza kuogelea katika ziwa la Nanhu, mjini humo katika majira ya siku za baridi. Kama tunavyofahamu kuwa, kuogelea wakati wa siku za joto ni aina ya michezo ya kujiburudisha, lakini kuogelea ziwani katika majira ya baridi, ni changamoto kubwa kwa binadamu, wakati ambapo sehemu ya juu ya maji inakuwa imeganda na upepo mkali huwa unavuma.

Mzee Wang Lie mwenye umri wa miaka 60 ni mmoja kati ya mashabiki wa mchezo wa kuogelea katika majira ya baridi. Alisema  "Katika majira ya siku za baridi, hapa kwetu maji huwa yanaganda. Kwa hiyo tunapasua barafu kwenye eneo la mita za mraba kati ya 30 na 50 kwenye ziwa, ili tuweze kuogelea ziwani."

Watu wanaovutiwa na mchezo huo wanausifu kama "Jimnastiki ya mishipa ya damu", kwani unaweza kuimarisha nguvu za moyo na mshipa wa damu, na kusaidia kujenga uwezo wa kujikinga na kukabiliana na magonjwa yanayohusu moyo na mishipa ya damu.

Mzee Wang alifafanua kuwa, mwanzoni kulikuwa na watu wanane tu walioshiriki kwenye mchezo huo wa kuogelea katika majira ya baridi. Mwaka 1988 watu hao walianzisha shirika la mchezo wa kuogelea wakati wa majira ya baridi likilenga kueneza mchezo huo. Hivi sasa miaka 18 imeshapita, katika mji wa Changchun kuna watu zaidi ya 300 wanaoshiriki kwenye mchezo huo.

Akiwa mmoja wa watetezi wa mchezo huo, mzee Wang alieleza kufurahia hali ya kuenea kwa mchezo huo. Akikumbusha hali ngumu iliyowakabili wakati walipoanza kogelea wakati wa siku za baridi, alisema  "Wakati huo hali ilikuwa ngumu sana, ambapo kulikuwa hakuna vibanda vya kubadilishia nguo, na ilitubidi sisi wenyewe tupasue barafu, jambo ambalo likichukua saa 2 hadi 3, kwa hiyo tuliweza kuogelea kwa dakika 4 au 5 tu, lakini hivi sasa hali imeboreshwa. Sasa tuna klabu ya mchezo wa kuogelea katika majira ya baridi, ambayo imefungwa zana za kisasa na tunaweza kubadilisha nguo, aidha kuna wafanyakazi wanaoshughulikia kupasua barafu."

Katika ziwa la Nanhu, Bw. Wang Wenxing mwenye umri wa zaidi ya miaka 50 alikuwa amevaa nguo ya kuogelea akifanya maandalizi kabla ya kujitosa majini. Alimwonyesha mwandishi wa habari mashua moja ikiwa ziwani, alisema mashua hiyo inatoa huduma kwa watu wanaoogelea siku za baridi. Alisema  "Mashua hiyo inaitwa mashua ya kupasua barafu, inafanya kazi ya kuyeyusha barafu nyembamba. Lakini inashindwa kushughulikia barafu nene, kwa hiyo inabidi kuzivunja."

Bwana huyo alikwenda ziwani kwa kupitia daraja dogo la mbao, aliruka na kuingia ziwani kwa hali nzuri, na kuanza kuogelea. Ingawa alikuwepo kwenye maji kwa dakika chache tu, lakini hiki ni kitendo cha kishujaa kweli. Kwani katika sehemu ya kaskazini mashariki ya China, kuna baridi kali sana wakati wa majira ya baridi, kiasi kwamba tone la maji linaganda mara moja, inawabidi watu wavae nguo nzito, kofia na glavu ili kujikinga dhidi ya baridi kali. Hata hivyo watu kadhaa wakipuuza baridi kali, wanathubutu kuogelea kwenye maji yenye barafu, jambo ambalo ni la ajabu kweli.

Dada Xue Xiaofu ni shabiki wa mchezo wa kuogelea wakati wa majira ya baridi, alieleza jinsi anavyovutiwa na mchezo huo. Alisema "Ukiogelea wakati wa majira ya baridi unasikia baridi sana, lakini mchezo huo ni mazoezi ya kujenga mwili na imani, pia ni aina ya changamoto, kwani sio kila mmoja anaweza kufanya hivyo."

Watu hao wakimaliza kuogelea na kutoka ziwani, wanaoga mara moja kwa kutumia maji yaliyochotwa kisimani, hali ambayo inawafanya watu wengine wanaoshuhudia wajisikie baridi, lakini wanaopenda kuogelea siku za baridi wanaichukulia kuwa ni hali ya kawaida tu. Mchezo huo ni mchezo wa mashujaa, ambapo mashabiki wanajitetea kuwa, wanataka kushinda woga wao wenyewe na kutafiti maumbile.

Pamoja na kuwa ni aina ya mchezo wa kujengea mwili, kwa maoni ya mashabiki wa kuogelea siku za baridi, mchezo huo pia unaleta raha kubwa. Bw. Wang Lie aliwahi kutunga shairi moja akielezea furaha kubwa aliyopata kutokana na kushiriki kwenye mchezo huo. Shabiki mwingine Bw. Sun Manbin mwenye umri wa zaidi ya miaka 50 pia alitunga wimbo mmoja unaosifu moyo wa ushujaa wa watu wanaoogelea wakati wa majira ya baridi. Hivi sasa kila inapowadia sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China, mashabiki wa kuogelea wakati wa siku za baridi wanafanya onesho kubwa ambalo linawavutia watazamaji wengi.

Bw. Sun alifafanua akisema "Onesho la kuogelea wakati wa majira ya baridi linafanyika kila mwaka huko Changchun kwa ajili ya kusherehekea mwaka mpya wa jadi wa China. Majira ya spring yanapokaribia, joto linaanza kuongezeka na maua yanaanza kuchanua, barafu za mtoni pia zinaanza kuyeyuka, wakati huo tunaogelea kuvuka ziwa la Nanhu."

Idhaa ya kiswahili 2007-01-04