Tarehe 4 Januari,2007 ni siku isiyo ya kawaida kwa Bibi Margaret Chan, kwani siku hiyo ameanza kazi ya Mkurugenzi mkuu mpya wa Shirika la afya duniani WHO. Akiwa mkurugenzi mkuu wa WHO, atafanyeje kazi yake na ataonesha umuhimu gani? Nje ya Jengo la Shirika la afya duniani WHO kuna kinyago kimoja cha shaba nyeusi cha mvulana mmoja mwafrika anayemvuta baba yake mzazi kwa mwanzi ambapo wakielekea kwa taabu kwenye mlango mkuu wa Jengo la WHO. Kinyago hicho kimeonesha nia ya Shirika la WHO ya kuwahudumua wananchi wa dunia nzima, hasa watu wale wanaohitaji kusaidiwa. Baada ya kuchaguliwa kuwa mkurugenzi mkuu wa WHO, Bibi Margaret Chan aliahidi kwa dhati akisema:
Kwa hakika, Shirika la afya duniani linatakiwa kushughulikia kazi za kusaidia sehemu zote, nchi zote na wananchi wote katika kutatua matatizo ya afya za umma, lakini tunapaswa kutoa kipaumbele kuzisaidia nchi na wananchi ambao wanahitaji misaada ya dharura.
Shirika la afya duniani likiwa shirika la kimataifa lililo muhimu kabisa ambalo linashughulikia mambo ya afya kote duniani, linabeba jukumu kubwa sana. Wajibu na kazi zake kuu ni kuinua kiwango cha afya za wananchi wa duniani; kuwajibika na kazi za kuelekeza na kuratibu kazi za afya duniani; kuzisaidia serikali za nchi mbalimbalil zimarishe shughuli za afya; kuhimiza kinga na tiba ya magonjwa ya kisehemu na maradhi mengine. Na mkurugenzi mkuu akiwa ofisa mkuu wa kiufundi na kiutawala wa shirika hilo, kihalisi anatakiwa kuonesha umuhimu wake katika kuandaa mipango ya kimataifa na kutunga sera zinazohusiana na sekta ya afya, pia anatakiwa kufanya kazi za kuelekeza na kuratibu maendeleo ya mambo ya afya ya nchi mbalimbali duniani. Kuhusu jukumu kubwa linalomkabili, Bibi Margaret Chan ameainisha kazi yake kwa pande 6, na kuthibitisha kazi mbili kubwa zaidi miongoni mwake, yaani afya ya wakazi wa Bara la Afrika na afya ya wanawake wa dunia nzima. Alisema:
Nataka kusisitiza zaidi kuwa, tunapaswa kutumia nguvu za shirika la afya duniani na jumuia ya kimataifa kutatua matatizo ya afya kwa wakazi wa Afrika na wanawake wa dunia nzima. Wakazi wa nchi za Afrika na wanawake wa nchi maskini wamekandamizwa na magonjwa mabaya na hata wanashindwa kupumua vizuri, hali hiyo haivumiliki, na ni lazima kuibadili.
Bibi Margaret Chan ana uzoefu na maarifa mengi kuhusu usimamizi wa afya za umma, na anaelewa vizuri kanuni za kazi, pia ana mpango uliopevuka kuhusu siku za mbele za shirika la afya duniani. Lakini hivi sasa dunia inakabiliwa na tishio za magonjwa ya kimataifa na kisehemu, bibi Margaret Chan anatakiwa kubeba jukumu zito. Mwandishi wa habari wa Gazeti la Guangmingribao la China huko Geneva Bwana Liu Jun aliwahi kufanya mahojiano mara kadhaa na Bibi Margaret Chan alisema:
Margaret Chan amechaguliwa kuwa mkurugenzi mkuu wa WHO katika wakati ambapo shirika hilo linakabiliwa na changamoto kubwa. Katika miaka ya hivi karibuni, wakati magonjwa ya kuambukizwa ya tangu zamani bado hayajatokomezwa, magonjwa mapya ya maambukizi yameibuka, tena virusi vya magonjwa hayo mapya vina madhara makubwa zaidi kuliko vile vya zamani.
Bwana Liu Jun alisema, nchi zaidi ya 50 za Bara la Afrika ni nchi zilizothibitishwa na Benki ya dunia kuwa ni nchi zilizoko nyuma kabisa kimaendeleo, kama magonjwa ya maambukizi yataibuka katika nchi hizo wakati wowote, na huenda athari kubwa zitatokea duniani. Hivyo Margaret Chan anakabiliwa na jukumu kubwa la kuratibu kazi na kuzisaidia nchi hizo kutatua matatizo mbalimbali ya afya kwa wananchi.
|