Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-05 16:05:47    
Bi. Ge Jie msomi wa China aliyeeneza ufahamu kuhusu Afrika

cri

Kutokana na kufanyika kwa mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, uhusiano kati ya China na nchi za Afrika umefungua ukurasa mpya, watu wengi zaidi wa China wamekuwa na hamu ya kutembelea na kufanya biashara barani Afrika. Lakini baada ya kuanzishwa kwa  Jamhuri ya watu wa China, mwanzoni watu wa China walikuwa wanajua mambo machache kuhusu bara la Afrika. Ili kuwafahamisha watu wa China mambo ya Afrika, baadhi ya wasomi wa China wamejishughulisha utafiti wa mambo ya Afrika, Bibi Ge Jie anayefahamika sana ni mmoja kati ya watu hao. Bibi Ge Jie mwenye umri wa miaka 70 alikuwa mkuu wa idara ya utafiti wa Asia magharibi na Afrika katika taasisi ya sayansi ya jamii ya China. Katika miaka zaidi ya 40 iliyopita ameandika makala mia kadhaa kuhusu mambo ya Afrika, alitafsiri vitabu na makala nyingi husika, pia alikwenda ng'ambo kutoa mihadhara mara kwa mara na kubadilishana maoni na wasomi maarufu wa nchi za nje, hivyo anajulikana sana katika utafiti wa mambo ya Afrika.

Ili kumsifu Bibi Ge Jie aliyetoa mchango mkubwa katika kueneza ujuzi wa Afrika na kuhimiza urafiki kati ya China na Afrika, shirikisho la urafiki na nje la watu wa China muda mfupi uliopita lilimteua Bibi Ge Jie kuwa mmoja kati ya wachina 10 wanaosifiwa na waafrika, na kumpatia "tuzo ya kwanza ya mchango wa urafiki kati ya China na Afrika". Bibi Ge Jie alizaliwa mjini Shanghai wakati mji wa Shanghai ulipokuwa chini ya ukoloni wa Japan, hivyo alikuwa na hisia zilizo sawa sawa na zile za watu wa Afrika waliotawaliwa na kukamdamizwa na wakoloni wa magharibi, ndiyo maana alikaza nia ya kujishughulisha utafiti wa mambo ya Afrika.

Mwaka 1961 chini ya maagizo ya hayati mwenyekiti Mao Zedong, idara ya utafiti wa Afrika ilianzishwa na kutunga kitabu kuhusu mambo ya  Afrika ili kutoa marejeo kwa viongozi wa serikali kuu. Mwaka 1982 Bibi Ge Jie aliongeza mambo mapya na kutunga kitabu kingine cha maelezo ya Afrika pamoja na wengine, kikawa kitabu cha kwanza kilichochapishwa na kutolewa hadharani nchini China kuhusu mambo ya Afrika.

Tokea miaka ya 80 ya karne iliyopita, ili kujulisha zaidi mambo ya Afrika kwa watu wa China, Bibi Ge Jie alipata wazo la kutunga ensaikolopidia ya Afrika. Alisema "wakati huo watu wa China walikuwa na ufahamu mdogo tu kuhusu mambo ya Afrika, wachina wengi waliotarajia kwenda Afrika kufanya biashara na mambo mengine katika nchi za Afrika walikuja kuniuliza mambo ya Afrika."

Mwezi Septemba mwaka 2000, "Ensaikolopidia ya Afrika" ilichowashirikisha wasomi na watafiti 69 na kuhaririwa na Bibi Ge Jie ilichapishwa. Ensaiklopidia hiyo ina maneno zaidi ya milioni 1.66. Bibi Ge Jie alisema, tofauti ya ensaikolopidia nyingine, kitabu hicho kinachoeleza utamaduni na historia ya Afrika kiliundwa na mijadala mbalimbali ya utafiti, milango mingi ni insha huru. Ensaikolopidia hiyo imekuwa marejeo muhimu kwa viongozi wa serikali kuu na watu wanaoshughulikia mambo ya nje.

Afrika ya kusini ni nchi inayositawi zaidi kiuchumi barani Afrika, lakini ilianzisha uhusiano wa kibalozi na China mwaka 1998. Kabla ya hapo ili kujua vizuri kuhusu mambo ya nchi hiyo na kutoa takwimu muhimu kwa idara husika, mwaka 1991 Bibi Ge Jie alikwenda Afrika ya kusini kufanya uchunguzi na utafiti. Katika muda wa mwezi mmoja Bi. Ge Jie aliwahi kutembelea vijiji vilivyo nyuma kimaendeleo, kuingia katika migodi ya dhahabu yenye kina cha zaidi ya mita 3000, na kufanya uchunguzi katika sehemu yenye mapambano kati ya makundi mbalimbali ya wakazi wenyeji. Isitoshe Bibi Ge Jie pia alibadilishana maoni na katibu mkuu wa chama cha kikomunisti cha Afrika ya kusini, wanafunzi vijana, wanachama wa chama cha ukombozi, wazungu wenye msimamo wa kati, waafrika na wabunge wa vyama vyenye mrengo wa kulia. Alikusanya maoni ya aina mbalimbali na kuelewa kwa kina hali ya utatanishi ya migongano ya kijamii nchini Afrika ya kusini. Mwaka 1994, kitabu alichokiandika kiitwacho "Afrika kusini-ardhi yenye maliasili nyingi na matatizo mengi" kilichapishwa, kitabu hicho kilikuwa kinawafahamisha wasomaji wa China hali halisi ya Afrika ya kusini.

Tangu ajiunge na idara ya utafiti wa Asia magharibi na Afrika ya taasisi ya sayansi ya jamii ya China mwaka 1961, Bibi Ge Jie ameshikilia kufanya utafiti kuhusu mambo ya Afrika bila kulegea. Ingawa sasa amezeeka, lakini bado anafuatilia kazi ya utafiti wa mambo ya Afrika. Ana matumaini kuwa kizazi kipya kitafanya kama alivyofanya kuendelea kufanya utafiti wa mambo ya Afrika, na kuimarisha urafiki kati ya China na Afrika.

Idhaa ya kiswahili 2007-01-05