Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-05 16:07:10    
China kuzisaidia nchi za Afrika kupambana na malaria

cri

Tarehe 27 Novemba mwaka 2006, semina ya kupambana na malaria iliyoandaliwa na serikali ya China ilifunguliwa huko Kampala, mji mkuu wa Uganda. Hii ni moja ya hatua zitakazochukuliwa na serikali ya China katika kuongeza misaada kwa nchi za Afrika.

Kwa ajili ya kuandaa semina hiyo, serikali ya China iliwatuma wataalamu watano kufanya mawasiliano na madaktari 50 wa matibabu waliotoka kwenye sehemu 11 za Uganda, na kuwafahamisha uzoefu na mafanikio China iliyoyapata katika kupambana na malaria.

Kaimu balozi wa China nchini Uganda Bwana He Shijing alisema, kufanya semina hiyo ni kufuata ahadi zilizotolewa na serikali ya China ya kuipa Uganda dawa za kutibu malaria na kufanya mafunzo ya kuwaandaa wafanyakazi wa matibabu ili kusaidia kuboresha hali ya afya ya wananchi wa Uganda.

Waziri wa afya wa Uganda Bwana Steven Mallinga kwenye ufunguzi wa semina hiyo alisema, malaria imeleta athari mbaya kwa afya, maisha na kazi za watu wa Afrika, China ina teknolojia mpya katika sekta ya matibabu, hivyo watu wote walioshiriki semina hiyo wangetumia vizuri fursa hiyo kujifunza uzoefu kutoka kwa madaktari wa China. Alisema, kufanya semina hiyo kumeonesha kuwa uhusiano wa kirafiki kati ya Uganda na China umeimarishwa siku hadi siku, serikali ya Uganda inaishukuru China kwa msaada huo.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na wizara ya afya ya Uganda, hivi sasa malaria bado ni ugonjwa unaosababisha vifo vya watu wengi kabisa nchini humo, kila mwaka watu elfu 80 wa Uganda wanakufa kutokana na malaria.

Muda si mrefu uliopita China na Senegal zilifanya kongamano la kupambana na malaria huko Dakar mji mkuu wa Senegal. Konsela wa ubalozi wa China nchini Senegal anayeshughulikia mambo ya biashara Bw. Zhou Zhaoming alisema hilo ni kongamano la kwanza kuandaliwa na wizara ya mambo ya nje ya China kufanyika barani Afrika, na hii inaonesha kuwa kazi ya serikali ya China kusaidia Afrika kuhusu kinga na tiba ya malaria imeingia katika mambo halisi.

Mshauri wa wizara ya afya ya Senegal Bwana Abdulaye Li kwenye kongamano hilo alisema, asilimia 33 ya watu wa Senegal hukumbwa na ugonjwa wa malaria, ugonjwa huo umekuwa ugonjwa mbaya zaidi unaotishia maisha ya watu nchini humo. China imefikia kiwango cha juu kabisa duniani katika kutafiti na kutengeneza dawa za kupambana na malaria kutokana na mitishamba aina ya artemisinin, na kupata mafanikio makubwa. Senegal inahitaji kupata uzoefu na teknolojia ya China katika kupambana na malaria na kutaka China ijenge kituo cha kupambana na malaria nchini Senegal.

Mwenyekiti wa jumuiya isiyo ya kiserikali ya kimataifa ya Senegal Daktari Fadimada Sai alisema, hivi karibuni rais wa Senegal ameeleza nia ya kufanya ushirikiano na China katika kupanda mitishamba ya artemisinin na kutengeneza dawa za kupambana na malaria kutokana na mitishamba hiyo, akieleza matumaini yake kuwa msaada wa China utawanufaisha watu wa Senegal na nchi nyingine za Afrika. Jumuiya yake inatazamia kufanya ushirikiano na China katika kuendeleza na kutumia rasilimali nyingi za mitishamba ya Senegal.

Dawa za Cotexin zilizotengenezwa nchini China kutokana na artemisinin zinapendwa sana na watu wa Afrika. Takwimu zimeonesha kuwa, hivi sasa Cotexin zimechukua theluthi moja ya dawa za kutibu malaria kwenye soko la nchi za Afrika magharibi, na kuchukua theluthi mbili ya dawa za aina hiyo kwenye soko la Afrika mashariki.

Cotexin ni dawa za kupambana na malaria zilizopendekezwa na shirika la afya duniani na shirika la kuwahudumia watoto la Umoja wa Mataifa, mwezi Julai mwaka huu waziri mkuu wa China Bwana Wen Jiabao alipofanya ziara katika nchi za Afrika alizipa nchi alizotembelea dawa hizo kama zawadi.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na shirika la afya duniani, kila mwaka watu milioni 350 hadi 500 duniani wanaugua malaria, ugonjwa huo unaenea katika nchi zaidi ya 100. katika nchi za Afrika, kila mwaka watoto zaidi ya milioni moja wasiozidi umri wa miaka mitano wanakufa kutokana na malaria, ambao ni ugonjwa unaosababisha vifo vya watoto wengi kabisa katika nchi za Afrika.

Kwenye mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika hapa Beijing mwanozni mwa mwezi Novemba mwaka huu, rais Hu Jintao wa China alitangaza kuwa, China itazisaidia nchi za Afrika kujenga hospitali 30, na kutoa Yuan milioni 300 kuzisaidia nchi za Afrika kukinga na kutibu malaria, amabzo zitatumiwa katika kuzipa nchi za Afrika dawa za artemisinin na kuanzisha vituo 30 vya kupambana na malaria.

Idhaa ya kiswahili 2007-01-05