Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-09 15:35:22    
Mazingira ya kuanzisha shughuli kwa kampuni ndogo na za wastani za Beijing yaboreshwa kwa udhahiri

cri

Eneo la ustawishaji wa sayansi na teknolojia la Zhongguancun la Beijing linachukua nafasi ya kwanza kwa umuhimu katika maeneo ya sayansi na teknolojia ya nchini China, karibu kampuni zote kiasi cha elfu 16 zilizoko kwenye eneo hilo, ziko katika kipindi cha mwanzo au kipindi cha kukua. Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na uungaji mkono wa idara za serikali, mazingira ya uanzishaji shughuli na maendeleo ya kampuni ndogo na za wastani za sayansi na teknolojia yameboreshwa kwa udhahiri.

Bw. Yu Zhou alianzisha kampuni inayojulikana kwa "Sayansi na Teknolojia ya Kupeng" mwanzoni mwa mwaka jana ndani ya jengo la "Huduma za Uanzishaji Shughuli" lililoko kwenye eneo la sayansi na teknolojia la Zhongguancun. Huko kuna mawasiliano mepesi na mazingira bora kwa shughuli za biashara. Shughuli muhimu za kampuni hiyo ni kutoa mpango wa utatuzi wa uhimizaji mauzo kwa wafanyabiashara. Hivi sasa kampuni ya Bw. Yu Zhou inaendelea vizuri, anaona kuwa hali nzuri ya kampuni yake inatokana na sera za uungaji mkono za eneo la sayansi na teknolojia la Zhongguancun.

"Zhongguancun inatoa misaada mingi kwa kampuni ndogo zinazoanzisha shughuli huko. Kabla ya kuingia hapo, tuliwahi kuwasiliana na baadhi ya idara, na tulifahamishwa sera husika zilizopo na zitakazotolewa hapo baadaye. Tulivutiwa sana na mazingira ya huko, hususan mazingira ya sera nzuri."

Shughuli muhimu za Jengo la "Huduma za Uanzishaji Shughuli" ambalo ilipo kampuni ya Bw. Yu Zhou, ni kama "zana ya kutotolesha vifaranga", (incubator) ambalo linatoa misaada kwa kampuni ndogo na kutoa huduma mbalimbali kwa kampuni zilizoko katika jengo hilo. Bw. Yu Zhou alisema, jengo hilo linatoa huduma mbalimbali kwa kampuni za huko zikiwemo usajiri wa kampuni, kukusanya kodi kwa niaba ya idara ya serikali, uhasibu na kuajiri wafanyakazi wanaohitajiwa. Kutokana na huduma hizo, kampuni hazina haja ya kushughulikia mambo hayo yanayochukua muda na yenye matatizo, tena gharama za uendeshaji shughuli za kampuni zinapungua.

Ni kama Bw. Yu Zhou alivyofanya, Bw. Yang Xicheng mwaka jana alianzisha kampuni ya software ndani ya jengo hilo hilo. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, sera zenye nafuu zinazotolewa na jengo la "Huduma za Uanzishaji Shughuli" zinanufaisha sana maendeleo ya kampuni yake.

"Serikali inatoa ruzuku ya Yuan 0.5 kwa siku kwa kila mita 1 za mraba, ukubwa wa ofisi yetu ni mita 120 za mraba, hivyo manufaa hayo ni halisi na tunaweza kuyaona. Sera hizo zinapendwa sana na kampuni zilizoanzishwa muda si mrefu uliopita, kwani kampuni hizo hazina mitaji ya kutosha katika kipindi hicho."

Bw. Yang Xicheng anafurahia sana mazingira ya uanzishaji shughuli ya eneo la sayansi na teknolojia la Zhongguancun, tena ana imani kubwa kuhusu mustakabali wa maendeleo ya kampuni yake. Alisema ingawa kampuni yake ni ndogo sana katika kipindi cha mwanzoni, lakini mazingira bora ya uanzishaji shughuli yanaisaidia kampuni yake kupata maendeleo mzuri.

Hivi karibuni eneo la sayansi na teknolojia la Zhongguancun la Beijing limechukua hatua kadhaa za kuboresha mazingira ya uanzishaji shughuli na maendeleo kwa kampuni za wastani na ndogo, moja ya hatua hizo ni kujenga jengo la "Huduma za Uanzishaji Shughuli". Ujenzi wa mradi wa kipindi cha kwanza ulioanzishwa mwanzoni mwa mwaka 2006 na kamati ya usimamizi ya eneo la sayansi na teknolojia la Zhongguancun na kampuni ya mali zisizohamishika ya eneo hilo unapendwa sana na kampuni ndogo na za wastani. Kutokana na msingi huo, ujenzi wa jengo la "Huduma za Uanzishaji wa Shughuli" lenye mita za mraba elfu 40 wa kipindi cha pili umekamilika hivi karibuni, jengo hilo lenye huduma nzuri zaidi linaweza kutosheleza mahitaji ya kampuni mbalimbali.

Mratibu mkuu wa jumuiya ya kampuni za mali zisizohamishika ya Zhongguancun Bw. Dai Jian alisema, kampuni zinazoingia kwenye jengo hilo zinanufaika kutokana na sera zenye unafuu.

"Ili kupunguza gharama za uanzishaji wa shughuli kwa kampuni za sayansi na teknolojia, Zhongguancun imejenga majengo ya "Huduma za Uanzishaji Shughuli" ikiwa na lengo la kutoa ruzuku ya kodi za nyumba kwa kampuni za sayansi na teknolojia; kwa upande mwingine tumekamilisha huduma za wakala, ambazo ni pamoja na shughuli za viwanda na biashara, ukusanyaji kodi, utoaji habari za kisheria na usimamizi, na kuzisaidia kampuni zilizoko katika jengo hilo kufanya shughuli ndogo za kawaida."

Mbali na kujenga jengo lenye "Huduma za Uanzishaji wa Shughuli", eneo la sayansi na teknolojia la Zhongguancun limefungua ofisi ya utoaji mikopo iliyoanzishwa na benki za biashara, kampuni, idara husika za serikali pamoja na wakala, ambayo inatoa dhamana kwa kampuni ndogo kupata mikopo ya kuanzisha shughuli. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2005, ofisi hiyo imetoa dhamana kwa mikopo ya Yuan bilioni 2.8 iliyoombwa na kampuni ndogo karibu 300.

Naibu mkurugenzi wa kamati ya usimamizi ya eneo la sayansi na teknolojia la Zhongguancun Bw. Ran Qi alisema, ili kuunga mkono maendeleo ya kampuni za wastani na ndogo, eneo hilo linajitahidi kuingiza uwekezaji wenye hatari. Alisema,

"Ili kuanzisha mazingira ya uwekezaji ya kuzisaidia kampuni ndogo kuanzisha shughuli kwenye eneo la Zhongguancun, sisi tumekuwa na ushirikiano na mashirika zaidi ya 20 ya uwekezaji wenye hatari, mashirika ya uwekezaji yakiwekeza katika kampuni za teknolojia ya kisasa hapa Zhongguancun, sisi tunashiriki bila masharti kwenye asilimia 20 ya uwekezaji. Licha ya hayo, tumeanzisha uwekezaji kwa mbegu (yaani kuwekeza kwenye kampuni ndogo zilizoko katika kipindi cha uanzishaji wa shughuli zake), endapo kampuni ya uwekezaji inawekeza kwa kampuni zilizoko katika kipindi cha mbegu, sisi tutashiriki kwa asilimia kubwa zaidi ya hapo. Mbali na hayo, tumeanzisha mfuko wa fedha wa uwekezaji wenye hatari kwa kushirikiana na mashirika ya uwekezaji kwa mtindo wa ubia."

Habari zinasema, eneo la sayansi na teknolojia la Zhongguancun pia limeanzisha mazingira bora kwa uanzishaji shughuli na maendeleo ya kampuni za wastani na ndogo katika ujenzi wa utamaduni. Kwa mfano kamati ya eneo la sayansi na teknolojia la Zhongguancun imetoa wazo la "kuhimiza uanzishaji wa shughuli na kuvumilia kushindwa", ambalo limeboresha mazingira ya uanzishaji shughuli katika eneo hilo. Alipozungumzia sera zitazotolewa za kuzisaidia kampuni za wastani na ndogo, Bw. Ren Ranqi alisema,

"Kutoa huduma na kuanzisha mazingira ya uanzishaji shughuli kwa kampuni za wastani na ndogo ni lengo muhimu la matumizi ya fedha ya umma la serikali. Pamoja na mahitaji ya maendeleo ya kampuni ndogo, sisi tutatoa mazingira bora zaidi kwa kampuni nyingi zaidi kuanzisha shughuli kwenye eneo la Zhongguancun.

Mazingira bora ya uanzishaji wa shughuli yamesaidia kampuni za wastani na ndogo zilizoko kwenye eneo hilo kuimarika kwa haraka. Katika miaka karibu miwili iliyopita, ongezeko la kampuni mpya kwenye eneo hilo kwa mwaka ni kiasi cha 4,000, wakati ongezeko la kampuni zenye pato la zaidi ya Yuan milioni 100 kwa mwaka ni kiasi cha 100, na wastani wa ongezeko la thamani ya uzalishaji mali wa eneo hilo ni zaidi ya 20% kwa mwaka.

Idhaa ya kiswahili 2007-01-09