Kuanzia tarehe 9 Januari, 2007, Idara kuu ya ulinzi ya Japan itapandishwa ngazi na kuwa Wizara ya ulinzi, ambapo Wizara mpya ya ulinzi ya Japan itainuliwa hadhi yake ya kisheria, kuongezwa madaraka ya utoaji maamuzi na kuongezwa madaraka ya kifedha, na mabadiliko mbalimbali yatatokea mfululizo. Waziri mkuu wa Japan Bw Shinzo Abe tarehe 9 atakwenda ziarani barani Ulaya, ambapo atakuwa waziri mkuu wa kwanza wa Japan atakayetembelea makao makuu ya NATO huko Brussels, na pande mbili zitajadili ushirikiano katika kulinda amani, ukarabati wa baada ya vita na shughuli nyingine za kijeshi.
Hali halisi ni kwamba kupandishwa ngazi kwa Idara kuu ya ulinzi ya Japan, na mwelekeo wa kufanya ushirikiano wa kijeshi na Jumuiya ya NATO, pamoja na shughuli zake nyingine kama vile kugombea nafasi ya kuwa mjumbe wa kudumu wa baraza la usalama, na kuhimiza marekebisho ya "katiba ya amani", zote zimeonesha juhudi za kuthibitisha malengo mapya ya nchi na kufanya marekebisho ya kimkakati zilizofanywa na Japan katika hali mpya ya kimataifa baada ya vita vya baridi. Bw Junichiro Koizumi na Bw Shinzo Abe wote wanatetea kuifanya Japan ijitoe kutoka kwenye "mfumo wa baada ya vita", na kuwa "nchi ya kawaida", wanaona Japan haipaswi kuridhika na hadhi yake ya nchi kubwa kiuchumi, bali inapaswa kujitahidi kuwa nchi kubwa kisiasa na kijeshi.
Hivi sasa katika hali ambayo muungano wa kijeshi wa sehemu mbalimbali duniani umefilisika au kudhoofika mmoja baada ya mwingine, lakini Muungano wa kijeshi wa Japan na Marekani unaimarishwa siku hadi siku, ushirikiano kati ya nchi hizo mbili unafanyika katika kanda ya Asia na Pasifiki, pia umeanza kupanuka hadi dunia nzima. Watu fulani nchini Japan wanaona kuwa Japan ya hivi leo na Marekani zinapaswa kushirikiana na Marekani kutuma askari wengi zaidi kwenda nchi za nje kwa kisingizio cha "kuendesha haki ya kujilinda kwa pamoja", ili kutimiza ndoto ya kuwa nchi kubwa kijeshi. Kutokana na sababu hiyo watu fulani nchini Japan wanapiga makelele zaidi ya kutaka "katiba ya amani irekebishwe, na kuondoa kikomo cha "madaraka ya kujilinda kwa pamoja".
Kwa kuwa Bw Junichiro Koizumi alipokuwa madarakani alikwenda mara kwa mara kwenye hekalu la Yasukuni kutoa heshima kwa mizimu ya wahalifu wa kivita, uhusiano kati ya Japan na nchi jirani ulirudi nyuma sana. Baada ya waziri mkuu mpya Bw Shinzo Abe kuingia madarakani, watu wanaona kuwa Japan inajitoa siku hadi siku kutoka hali ya upweke wa kidiplomasia. Lakini kutokana na hali ilivyo maalum ya siasa ya kijiografia katika sehemu ya Asia ya kaskazini ya mashariki pamoja na msimamo wa Japan kuhusu masuala ya kihistoria, nchi jirani za Japan zinapaswa kuchukua tahadhari juu ya kupanda ngazi kwa mfululizo kwa sera ya kujilinda ya Japan.
Matokeo ya vita vikuu vya pili vya dunia yameonesha kuwa, kufuata msimamo wa kujifanya kuwa nchi kubwa kijeshi na kutishia nchi jirani ni njia isiyo na mwangaza; hivi sasa amani na maendeleo ni mkondo mkuu duniani, ambapo nchi mbalimbali zote zinafanya juhudi za kupata fursa ya kujiendeleza katika utandawazi wa uchumi kwenye kanda mbalimbali. Nchini Japan mawazo ya kushika njia ya amani baada ya vita pia yametia mizizi mioyoni mwa watu, Japan imepita kipindi cha maendeleo ya haraka ya uchumi na ustawi wa jamii, yote hayo yanatokana na "katiba ya amani" iliyotangazwa na Japan mwaka 1947. Ndiyo maana kupandisha ngazi ya idara kuu ya ulinzi kuwa wizara ya ulinzi na kuweka kazi ya kurekebisha "katiba ya amani" kwenye ajenda, kutatingisha msingi wa amani na utulivu wa Japan baada ya vita, na mwishowe hakika kutadhuru maslahi ya kimsingi ya Japan yenyewe.
Idhaa ya Kiswahili 2007-01-09
|