Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-11 11:12:20    
Watu wa kabila la Wajing wanaoishi visiwani karibu na mpaka wa Vietnam

cri

Miongoni mwa makabila yote 56 hapa nchini China, kabila la Wajing ni kabila lenye watu wachache sana, ambao wanaishi kwenye visiwa vitatu vilivyopo kusini mwa China, kwenye mpaka kati ya China na Vietnam. Hivi karibuni mwandishi wetu wa habari aliwatembelea watu hao kwenye kijiji kiitwacho Wanwei.

Baada ya kuingia kwenye kijiji cha Wanwei, mwandishi wetu wa habari aliona nyumba za ghorofa zikiwa zimepangwa vizuri kwenye kando mbili za barabara, na mbele ya nyumba nyingi kuna magari mapya yanayoegeshwa. Kijiji hicho kina barabara safi. Wanakijiji walikuwa wana pilikapilika, wakipeleka samaki na kamba kwa magari hadi viwanda vya mjini. Mkuu wa kijiji cha Wanwei Bw. Su Mingfang alimwambia mwandishi wa habari kuwa, miaka 20 na 30 iliyopita kijiji hicho kilikuwa kipo nyuma kimaendeleo, wanakijiji walikuwa ni wavuvi wanaotegemea bahari. Kwa vile mashamba yaliyopo pwani hayana rutuba, ni vigumu sana kwa wanakijiji hao kulima mazao ya chakula. Wanakijiji walikuwa wanapaswa kupeleka samaki hadi kwenye sehemu ya mlimani yenye umbali wa kilomita makumi kadhaa ili kubadilisha chakula.

Alisema  "Katika miaka ya 70 ya karne iliyopita, kijiji chetu cha Wanwei kilikuwa kiko kisiwani, ambapo kila mara ilitubidi tusubiri kupwa kwa maji halafu kwenda sokoni. Wakati huo huo hali ya mawasliano ilikuwa mbaya."

Bw. Su aliongeza kuwa, miaka zaidi ya 20 iliyopita, kutokana na serikali ya China kuanza kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango, wakazi wa kijiji cha Wanwei walianza kutambua kuwa, uchumi wa kutegemea uvuvi peke yake hauwezi kuwaletea maendeleo, bali inapaswa kutafuta mbinu mpya zinazolingana na hali halisi ya kijiji hicho. Kwa hiyo baadhi ya wanakijiji walianza kujishughulisha na mifugo ya mazao ya maji, na wengine waliofahamu lugha ya Viet Nam, walianza kufanya biashara na watu wa Viet Nam.

Mfanyabiashara Liang Shaode ni mmoja kati ya watu hodari wa kabila la Wajing waliopata maendeleo makubwa kwa kutumia mbinu hizo. Bw. Liang mwenye umri wa miaka 38 alikuwa mwanakijiji wa kwanza aliyejishughulisha na utengenezaji na biashara ya mazao ya maji. Yeye si mrefu, lakini anaonekana ni mwenye busara kama Wachina wengine wanaoishi katika sehemu ya kusini ya China. Zaidi ya miaka 10 iliyopita, Bw. Liang alikuwa anategemea uvuvi kama wanakijiji wenzake. Alikumbusha akisema

"Nilivua samaki wengi zaidi kuliko wenzangu, mimi mwenyewe niliuza samaki, nilipata pesa nilinunua mashua ya uvuvi, nikaanza kufanya biashara ya samaki. Baada ya kipindi fulani, jina langu lilijulikana miongoni mwa wafanyabiashara walioko kwenye miji ya Shanghai na Beijing, ambao walianza kuagiza samaki kutoka kwangu, hatua kwa hatua nilifahamiana na watu wengi na biashara yangu ilikua sana."

Hivi sasa Bw. Liang Shaode ana kampuni ya mazao ya maji inayowaajiri wanakijiji wa huko zaidi ya 100. Zaidi ya hayo, alianzisha viwanda viwili vya kutengeneza mazao ya maji nchini Vietnam.

Kati ya familia zaidi ya elfu moja za watu wa kabila la Wajing katika kijiji cha Wanwei, nyingi zinafanya utengenezaji na biashara ya mazao ya maji, na ufugaji ya mazao ya majini.

Katika kijiji hicho jengo moja kubwa lenye kuta nyeupe na paa jekundu lilimvutia sana mwandishi wetu wa habari. Mkuu wa kijiji Bw. Su Mingfang alieleza kuwa, jengo hilo ni mahala ambapo watu wa kabila la Wajing wanapofanya matambikiko. Wajing walihamia China kutoka Vietnam miaka 500 kutoka kwa Viet Nam. Hivi sasa kabila hilo lenye watu zaidi ya elfu 20 tu linaendelea na mila zao za kusherehekea sikukuu ya Hajie kila mwezi wa Juni, ambapo Wajing wanakusanya kwenye jengo hilo wakiimba nyimbo za kusifu mungu na kufanya ibada.

Mzee Su Weifang alianza juhudi za kukusanya na kueneza utamaduni wa kabila la Wajing. Kwa sababu aliwahi kufundishwa lugha ya Kijing na babu yake, mzee Su anafahamu sana lugha hiyo. Alisema  "Hatua ya kwanza niliyofanya ni kukusanya lugha hiyo, niliwatafuta wazee wanaofahamu lugha hiyo kwenye visiwa vitatu wanapoishi Wajing. Halafu niliitafsiri. Hatua nyingine ni kuandaa semina ya lugha hiyo. Niliandaa semina mbili ziliwashirikisha watu 19, wakiwa wazee kwa vijana."

Mkuu wa kijiji cha Wanwei Bw. Su Mingfang alisema, hivi sasa kijiji hicho kimepata maendeleo, na kina uwezo wa kuhifadhi utamaduni wa kabila la Wajing. Alisema zaidi ya hayo, wana mpango wa kueneza utamaduni huo mionogni mwa watu wa makabila mengine. Alisema "Tuna mpango wa kujenga jumba la makumbusho la kabila la Wajing. Jengo hilo litasanifiwa kulingana na umaalumu wa utamaduni wa kabila letu. Kwenye jumba hilo, tutaonesha vifaa mbalimbali tunavyotumia katika uvuvi na maisha, pia tutaonesha mabadiliko ya maisha ya Wajing katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, ili watu wa vizazi vijavyo wafahamu jinsi Wajing walivyoishi."

Idhaa ya kiswahili 2007-01-11