Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-11 11:07:23    
Watoto wa kike waliokosa elimu shuleni wafundishwa kazi za ufundi

cri

Watoto wa kike ni kinamama wa siku zijazo. Nchini China kuna baadhi ya watoto wa kike waliokosa nafasi ya kwenda kusoma shuleni kutokana na familia zao kuwa masikini, hivi sasa watoto hao wamekua na kuzidi umri wa kusoma shuleni. Kwa bahati nzuri wanapata nafasi ya kufundishwa kazi za ufundi katika mradi wa ushirikiano kati ya China na Uingereza. Kutokana na mafunzo hayo, wasichana hao wamejenga moyo wa kujiamini, na kuinua maisha yao kwa kuchapa kazi.

Mradi huo wa kuwapa mafunzo ya kiufundi watoto wa kike wenye umri mkubwa ulianzishwa miaka minee iliyopita na serikali za nchi mbili za China na Uingereza. Kwa upande wa China, shirikisho la wanawake la China linashughulikia utekelezaji wa mradi huo. Katibu wa ofisi ya sekrieriti ya shirikisho hilo Bibi zhang Shiping alieleza kuwa, mpaka hivi sasa wasichana wenye umri mkubwa zaidi ya elfu 10 wamepewa mafunzo bila malipo kutokana na mradi huo, watoto hao wanatoka mikoa mitatu ya magharibi ya China ikiwemo Sichuan, Gansu na Yunan. Alisema

"Tangu mradi huo uanze kutekelezwa mpaka sasa, watoto wa kike waliokosa elimu shuleni wamenufaika, wao wana umri wa miaka kati ya 15 na 18, na wanatoka familia yenye umaskini. Walipewa mafunzo ya aina mbalimbali, kwa mfano masomo ya Kichina na hesabu, mbinu za maisha na ufundi. Katika mafunzo hayo, wasichana hao walipata mawazo mapya, maisha yao na ya familia yao yaliboreshwa."

Hivi sasa wasichana waliohitimu mafunzo hayo wameanza kupata kipato kwa kutumia ufundi waliofundishwa, baadhi yao wamekwenda mijini kufanya kazi, wengine wamepata ajira katika makwao, baadhi yao walianza kujishughulisha na kilimo na ufugaji. Wasichana wengine wanawasidia sana wazazi wao katika shughuli za kilimo, wakiwafundisha wazazi namna ya kutambua mbegu na mbolea bora.

Zhang Hui ni mmoja kati ya wasichana walionufaika na mradi huo. Msichana huyo mwembamba ana umri wa miaka 16. Alisema "Mafunzo yakimalizika mwenyekiti wa shirika la wanawake la kata yetu alizungumza na mama Chen Jufang, ambaye ni hodari katika mifugo ya sungura, alinipa sungura watano. Nikaanza kuwafuga kwa kutumia ufundi niliofundishwa. Naona nina uwezo, kwani naweza kuchuma pesa na kumsaidia baba yangu."

Mama wa msichana huyo alifariki dunia na sarantani miaka mitatu iliyopita na kuwaacha Zhang Hui, baba na dada yake mdogo. Kwa sababu ya mzigo mkubwa wa madeni unaoikabili familia hiyo, mwaka juzi baba yake alimwomba Zhang Hui asiende shuleni. Alikubali ombi hilo.

Mwezi Julai mwaka jana, akisaidiwa na shirika la wanawake, msichana huyo alishiriki kwenye semina ya watoto wa kike wenye umri mkubwa iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa serikali za China na Uingereza. Baada ya mafunzo ya siku 40, Zhang Hui alipata ufundi wa mifugo na kuanza kufuga sungura. Hivi sasa idadi ya sungura imeongezeka sana kutoka watano hadi zaidi ya 80, aliuza baadhi yao na kupata pesa, yeye na baba yake walifurahi sana.

Bw. Tony Voutas kutoka Shirikisho la utamaduni la Uingereza (the British Council) ambaye ni mmoja wa wataalamu wa kutoa thamini juu ya mradi huo, alieleza maoni yake kuhusu maendeleo waliyopata wasichana hao, akisema "Kwa uhakika ninyi mmepata maendeleo katika ufundi na uwezo wa kuwasiliana na wengine, sasa ninyi ni wapole zaidi na wenye matumaini makubwa zaidi kwa mustakabali. Mtakapomaliza mafunzo na kurudi nyumbani, mtawaonyeshea jamaa zenu maendeleo mliyopata na kuwasaidia wapate maendeleo pia."

Maendeleo ya wasichana hao yanatokana na mafunzo, na matokeo mazuri ya mafunzo yanatokana na mbinu maalumu kwamba, mafunzo hayo yanafanyika si kama tu darasani, bali pia maishani. Kwa mfano walifundishwa upandaji wa miti ya matunda kwenye shamba la miti ya matunda, walifundisha ufundi wa kukata nywele ndani ya saluni, pamoja na ujuzi wa wauguzi hospitalini.

Zhang Hui alisema "Niliwahi kufundishwa namna ya kununua vitu ndani ya supermarket, ambapo tulikwenda tukiongozwa ma mwalimu wetu. Katika somo la Kichina na hesabu, mwalimu Wu alituambia kuwa, tukitaka tunaweza kufanya maonesho mbele ya wenzetu. Niliimba wimbo kwani napenda sana kuimba. Wengine walionesha mchezo wa kuigiza. Inapendeza sana."

Kabla ya kushiriki kwenye semina hiyo, Zhang Hui amekuwa alibanwa na shughuli mbalimbali za nyumbani na kumtunza dada yake mdogo, hakuwa na wazo lingine. Lakini hivi sasa msichana huyo ana ndoto kwamba, kwanza anafuga sungura ili apate pesa za kulipa madeni ya familia na kujenga nyumba mpya. Akiwa na pesa nyingine atawasaidia wasichana wengine waliokosa elimu shuleni walioishi kwenye sehemu zeney umaskini, ili waweze kujenga moyo wa kujiamini.

Mwalimu Xie Weiqiang aliyeshiriki kwenye mradi huo alisema moja ya mafanikio ya mafunzo hayo ni kuwajengea wasichana hao moyo wa kujiamini. Alikumbusha akisema, "Lengo kuu la mafunzo hayo ni kuleta mabadiliko ya mawazo. Mara ya kwanza nilipoanza kuwafundisha, nilimwuliza msichana mmoja jina lake, akalia kutokana na hofu. Lakini hivi sasa msichana huyo ana imani ya kuanzisha biashara yake mwenyewe."

Msichana huyo anaitwa Zhang Fangfang mwenye umri wa miaka 18. Hivi sasa amehimitu mafunzo hayo na kufanya kazi katika saloon moja mjini Nanjing, mashariki mwa China. Alisema "Kabla ya kushiriki kwenye semina hayo, sikuthubutu kutarajia kitu chochote, sikuwa na ndoto kabisa. Lakini sasa nina ndoto ya maisha, nataka kumiliki saloon moja. Kwa sababu sitaki kuajiriwa siku zote, nataka kuanzisha shughuli zangu mwenyewe kwa kuchapa kazi."

Idhaa ya kiswahili 2007-01-11