Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-12 16:02:05    
Matibabu ya jadi ya kichina yanayopendwa na watu wa Afrika

cri

Siku moja ya mwezi Machi mwaka jana, mkuu wa chuo kikuu cha utibabu cha Tunisia aliugua huku alisikia maumivu sana, hakuweza hata kupata usingizi, alikuwa ametumia dawa nyingi za kimagharibi lakini bado hazikuweza kupunguza maumivu yake. Lakini baada ya kupata matibabu ya akyupancha ambayo ni matibabu ya jadi ya kichina, maumivu yake yalipungua haraka, na muda mfupi baadaye aliweza kwenda kazini. Madaktari wa Tunisia walisifu sana tiba ya akyupancha kwa kuwa na ufanisi mzuri kiasi hiki. Mifano mingi kama huo imeipa matibabu ya akyupancha ya kichina sifa ya "sindano ya miujiza".

Katika miaka 43 iliyopita tangu serikali ya China ianze kutuma madaktari barani Afrika, ustadi mzuri wa matibabu na maadili mema ya madaktari wa matibabu ya jadi ya kichina vimewafahamisha watu wa barani Afrika siku hadi siku ufanisi mzuri wa matibabu ya jadi ya kichina. Katika nchi nyingi za Afrika, viongozi, maofisa na wakazi wa kawaida wote wanapenda kutibiwa na madaktari wa matibabu ya jadi ya kichina, na baadhi ya wanafunzi wa Afrika pia wamekuja China kujifunza matibabu ya jadi ya kichina.

Katika miaka miwili iliyopita, madaktari wa akyupancha wa kikundi cha madaktari wa China nchini Tunisia waliwahudumia wagonjwa zaidi ya elfu 20, ufanisi mzuri na huduma bora zimewafurahisha wagonjwa wengi. Mbunge mmoja wa nchi hiyo baada ya kupungua maumivu yake kwa matibabu ya akyupancha, alipendekeza wizara ya afya ya Tunisia kuendeleza matibabu ya akyupancha nchini humo. Gazeti la chama tawala cha Tunisia liliwahi kuchapisha makala ndefu kuwasifu madaktari wa matibabu ya jadi ya kichina waliotoa mchango mkubwa katika kuzidisha urafiki kati ya Tunisia na China kwa vitendo halisi vya kuwahudumia wagonjwa wa huko.

Matibabu ya jadi na dawa za mitishamba za kichina zimetumiwa katika hospitali ya Muhimbili ya Tanzania kwa miaka 19. Kutokana na mwaliko wa rais wa kwanza wa Tanzania hayati mwenyekiti Julius Nyerere, madaktari wa matibabu ya jadi ya kichina walianza kutumwa nchini Tanzania mwaka 1987. Katika miaka 19 iliyopita madaktari hao wa China wamewahudumia wagonjwa zaidi ya elfu 10 wa ukimwi. Kwa kuwa bei za dawa za mitishamba za kichina ni ya chini zikilinganishwa na bei za dawa za kimagharibi, hivyo zinawafaa wagonjwa wa nchi hiyo. Bi. Fatuma aliyethibitishwa kuugua ugonjwa wa ukimwi mwaka 1995, ameshikilia kutumia dawa za mitishamba za kichina, hadi sasa anajisikia vizuri, alisema madaktari wa China wamempa matumaini ya kuishi.

Madaktari wa matibabu ya jadi ya kichina barani Afrika wanatilia maanani kuwafundisha madaktari wenyeji wa huko matibabu ya kichina, lakini baadhi ya madaktari wa Afrika wanatarajia kuja China kujifunza hatua kwa hatua nadharia na njia za matibabu ya jadi ya kichina. Daktari wa Guinea Bwana Kamara ni mmoja wa wanafunzi waliotimiza ndoto yao. Bwana Kamara alikuwa mmoja wa kikundi cha kwanza cha wanafunzi wa Guinea kuja kusomea matibabu nchini China baada ya nchi hizo mbili kuanzisha uhusiano wa kibalozi. Kuanzia mwaka 1973 alikuwa anasoma katika hospitali ya Zhongshan mkoani Guangdong kwa miaka minane. Baada ya kurudi nchini kwake, Bw. Kamara anajishughulisha na matibabu ya akyupancha. Kutokana na juhudi zake, hivi sasa matibabu ya akyupancha yanakubaliwa na kupendwa na wakazi wa huko. Mwaka 2000 Chuo Kikuu cha matibabu cha Konakry ambacho ni chuo kikuu kikubwa kabisa cha Guinea kiliweka somo la matibabu ya akyupancha kuwa ni kozi ya lazima, hicho kilikuwa ni chuo kikuu cha kwanza barani Afrika kufanya hivyo.

Kuanzia miaka ya 60 ya karne iliyopita hadi leo, wanafunzi elfu moja hivi wa nchi za Afrika wamekuja China kusomea matibabu ya jadi ya kichina. Baadhi yao walijifunza kwa miezi mitatu, na wengine walijifunza kwa miaka mitano hata zaidi na kupata shahada ya pili. Wanafunzi hao walikuwa wameshinda matatizo ya kutofahamu lugha ya kichina na tofauti ya kiutamaduni, walijifunza pamoja na wanafunzi wa China na kufanya mtihani kama walivyofanya wanafunzi wa China. Baada ya kumaliza masomo nchini China na kurudi nyumbani kwao wengi wao wamechangia kuboresha afya ya wananchi wenzao kwa matibabu ya jadi ya kichina waliojifunza nchini China.

Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 10 tu ya bajeti ya utafiti wa afya duniani inatumiwa katika kinga na tiba ya magonjwa makubwa yanayohatarisha maisha ya asilimia 90 ya idadi ya watu duniani, magonjwa mengi yanalipuka mara kwa mara na kuwasumbua watu wengi wa nchi zinazoendelea, matibabu ya dawa za kimagharibi ni ya gharama kubwa kwa wagonjwa. Naibu mkuu wa idara ya usimamizi wa dawa za mitishamba ya China Bwana Fang Shuting alisema, matibabu ya jadi na dawa za mitishamba za kichina zinazotumiwa kwa gharama ndogo na kupata ufanisi mzuri zitatoa mchango mkubwa katika kupunguza pengo kubwa la afya kati ya nchi zinazoendelea na nchi zilizoendelea.

Bw. Fang alitoa mfano akisema, baadhi ya nchi za Afrika zinakumbwa na milipuko ya magonjwa mara kwa mara, hivi sasa vimelea vya ugonjwa wa malaria umekuwa sugu kwa dawa ya quinine ambayo ni dawa ya jadi ya kimagharibi ya kutibu malaria. Nchi nyingi za Afrika zimeanza kutumia dawa za kichina zilitotenegnezwa kutokana na mitishamba ya artemisinin na kupata ufanisi mzuri. Hivi sasa shirika la afya duniani WHO limezifanya dawa zilizotengenezwa kutokana na artemisinin kuwa chaguo la kwanza la kutibu ugonjwa wa malaria. Bw. Fang aliongeza kuwa katika matibabu ya ukimwi, dawa za jadi za kichina zimepata ufanisi mzuri katika kupunguza maambukizi, kurekebisha mfumo wa kukinga maradhi, na kuinua sifa ya maisha ya wagonjwa.

Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2002 China ilisafirisha dawa za kichina zenye thamani zaidi ya dola za kimarekani milioni 10 katika nchi za Afrika, kiasi hicho kilichukua asilimia 1.5 tu ya jumla ya thamani ya dawa za kichina zilizosafirishwa ng'ambo, hivyo ushirikiano kati ya China na Afrika katika sekta ya afya na tiba bado una nguvu kubwa.

Idhaa ya kiswahili 2007-01-12