Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-12 16:00:44    
Wanajeshi wa kulinda amani wa China wamaliza jukumu lao kwa mafanikio nchini Liberia

cri

Liberia ni nchi yenye mandhari nzuri iliyoko katika sehemu ya Afrika ya magharibi, lakini nchi hiyo imeharibiwa vibaya kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 14. Ingawa kuna wanajeshi 558 tu wa China kati ya wanajeshi elfu 15 wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Liberia, lakini sifa ya wanajeshi wa China ya kufuata nidhamu na kuchapa kazi imepongezwa sana na wananchi wa Liberia na tume maalum ya Umoja wa Mataifa nchini humo. Mwandishi wa habari wa China alipotembelea nchini Liberia kila akiuliza kuhusu hali ya maofisa na askari wa China waliotekeleza jukumu la kulinda amani nchini Liberia, wakazi wa huko waliwasifu sana askari hao.

Kikundi cha nne cha wanajeshi wa China waliotekeleza jukumu la kulinda amani nchini Liberia kiliundwa na vikosi vitatu vya uhandisi, uchukuzi na matibabu. Tangu wanajeshi hao wa China kupelekwa nchini Liberia, wameshakamilisha majukumu ya aina mbalimbali waliyopewa kwa uhodari na kwa ufanisi wakiwa wameshinda matatizo ya aina mbalimbali kama vile joto, mvua nyingi, kutofahamu mazingira, maambukizi ya magonjwa na vurugu za kijamii.

Wanajeshi wa kikosi cha uhandisi wamemaliza ukarabati wa barabara kuu yenye urefu wa kilomita 380, madaraja, uwanja wa ndege, na ujenzi wa miradi ya utoaji maji na umeme. Wanajeshi wa kikosi cha uchukuzi walisafiri kwa usalama kwa umbali wa kilomita laki 9.6, na wamehakikisha usafirishaji wa wanajeshi elfu 15 wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa hadi mahali walikopangiwa, na uchukuzi wa vifaa, nishati, maji na vifaa vya msaada. Wanajeshi wa kikosi hicho wametembelea karibu nchi nzima, na kusafirisha tani laki saba za vifaa. Madaktari wa kikosi cha matibabu kwa jumla wametoa huduma kwa wagonjwa zaidi ya 3200, na kuwaokoa wagonjwa mahututi zaidi ya 200, hakuna hata mmoja aliyekufa.

Naibu mkuu wa kikosi cha uhandisi Bwana Chen Dajun alisema, "ni vigumu kutengeneza barabara za Liberia, msingi wake una mchanga mwingi, mvua ikinyesha udongo na mchanga vinakuwa matope. Lakini baada ya jitihada za wanajeshi wa China, barabara zilizokuwa na mwendo wa kilomita 30 kwa saa moja sasa zimekuwa barabara kuu zenye mwendo wa kilomita 60 hadi 80 kwa saa."

Mkuu wa jimbo la Dajid Bwana Cristoph Bely aliwashukuru sana wanajeshi wa kikosi cha uhandisi cha China kwa mchango wao mkubwa. Alisema si kama tu wanajeshi wa China wamechangia ukarabati wa jimbo hilo, bali pia wameishi kwa masikilizano na wenyeji wa huko kama wa familia moja. Mkuu wa shule iliyoko kwenye sehemu ya kaskazini mashariki ya Liberia Bwana Henry alisema: "Tunawashukuru askari wahandisi wa China, wametusaidia kukarabati barabara na madaraja, kujenga miundo mbinu ya utoaji maji na umeme, ili kutuwezesha kufanya ukarabati vizuri."

Mwalimu wa siasa wa kikosi cha uchukuzi Bwana Fu Yuetao alisema, siku moja wanajeshi wa kikosi hicho walipopeleka vifaa kwenye kituo kilicho kwenye umbali wa kilomita 500, magari yalikwama barabarani kwa siku tano. Katika siku hizo tano wanajeshi wa China walifuata nidhamu kwa makini na kumaliza jukumu lao ipasavyo. Mkuu wa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa nchini Liberia aliwasifu sana wanajeshi hao wa China. Alisema bila ya kikosi cha uchukuzi cha China, wanajeshi wote wa kulinda amani nchini Liberia wasingeweza kutekeleza vizuri majukumu yao.

Wanajeshi wa kikosi cha matibabu cha China pia wamesifiwa sana na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na wananchi wa huko kwa ustadi wao wa matibabu na huduma bora. Usiku wa manane wa siku moja ya Septemba, askari mmoja kutoka Ethiopia alikumbwa na ugonjwa wa moyo kwa ghafla, alipopelekwa hospitalini baada ya saa tatu tayari alikuwa mahututi. Madaktari wa jeshi la kulinda amani la China walifanya uokoaji wa dharura kwa dakika 18 tu, mapigo ya moyo wa askari huyo yalirudi kama kawaida, dalili kubwa za ugonjwa zikawa zimepungua. Jenerali wa jeshi la Ethiopia aliyeshuhudia mchakato wote alisifu sana uhodari wa madaktari wa China.

Juhudi za wanajeshi wa China zimeonesha matunda. Wakati wanajeshi wa China walipokamilisha jukumu lao la miezi minane la kulinda amani nchini Liberia, walitunukiwa nishani ya heshima ya amani ya Umoja wa Mataifa. Kwenye sherehe ya kutoa nishani, naibu mkuu wa tume maalum ya jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa nchini Liberia Jemadari Louis Dacostar alisema, maofisa na askari wa jeshi la kulinda amani la China walikuwa wamekamilisha vizuri majukumu yao, huku wakiwa wametoa mchango mkubwa kwa amani na ukarabati wa Liberia. Kuwatunukia nishani ya heshima ya amani ya Umoja wa Mataifa kwa kusifu ushujaa, uchapa kazi na mafanikio waliyopata katika kutekeleza jukumu la kulinda amani.

Idhaa ya kiswahili 2007-01-12