Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bibi Condoleezza Rice, ambaye hivi sasa anaitembelea sehemu ya mashariki ya kati, na waziri mkuu wa Israel Bw. Ehud Olmert wamekubali kuwa na mazungumzo tarehe 15 mwezi Januari pamoja na mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Mahmoud Abbas. Lakini katika siku hiyo hiyo, waziri mkuu wa Israel Bw. Olmert alisisitiza kuwa, Israeli inakubali kuwa na mazungumzo na serikali ya Palestina inayoitambua Israel, kuacha kutumia nguvu za kimabavu na kutambua mikataba iliyosainiwa kati ya Palestina na Israel, licha ya hayo serikali ya Israeli siku hiyo pia ilitoa mpango wa kuongeza makazi ya wayahudi. Hayo yamefanya watu kuwa na wasiwasi kuhusu udhati wa Israel wa kurejesha mazungumzo ya amani.
Bibi Rice siku hiyo alikuwa na mazungumzo marefu pamoja na Bw. Olmert huko Jerusalem, ofisa mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe, baada ya mazungumzo hayo aliviambia vyombo vya habari kuwa Bi Rice na Bw Olmert wanakubali kufanya mazungumzo ya pande tatu pamoja na Bw Abbas kuhusu mambo ya siasa ya Palestina katika siku za baadaye, ambayo yanatarajiwa kufanyika ndani ya wiki tatu au nne zijazo. Pia alisema hayo ni mazungumzo yenye lengo kubwa zaidi kati ya Palestina na Israel mnamo miaka 6 iliyopita. Bibi Rice alipokuwa na mazungumzo na rais Hosni Mubarak wa Misri hapo baadaye katika siku hiyo pia alisema, mazungumzo ya pande 3 yatajadili zaidi namna ya kuanzisha nchi ya Palestina, ambayo ni kazi ya mwanzo ya mazungumzo ya kurejesha hadhi ya Palestina.
Lakini Bw Olmert alitoa taarifa haraka iliyoweka masharti ya kwanza kwa mazungumzo kati ya Palestina na Israel. Katika taarifa hiyo Bw Olmert alisema Israel inakubali kushiriki kwenye mazungumzo hayo ya pande tatu, lakini serikali ya Palestina inayoshiriki kwenye mazungumzo ni lazima itimize masharti matatu yaliyotolewa na jumuiya ya kimataifa, yaani kuitambua Israel, kuacha kutumia nguvu za kimabavu na kutambua mikataba iliyosainiwa kati ya Israel na Palestina, na kabla ya serikali ya Palestina kukubali masharti hayo, Israel haiwezi kufanya mazungumzo. Mbali na hayo taarifa hiyo inataka vipindi kadhaa vilivyotajwa katika mpango wa "ramani ya njia" vitekelezwe kimoja baada ya kingine kwa kufuata utaratibu wake.
Kutokana na hali halisi ya hivi sasa ya nchini Palestina pamoja na masharti ya kwanza yaliyotolewa na Bw Olmert, wachambuzi wanashuku udhati wa Israel wa kurejesha mazungumzo ya amani, pamoja na matokeo yanayotarajiwa na watu ya mazungumzo hayo ya pande tatu.
Kwanza ni vigumu kwa Palestina kuanzisha taifa linalolingana na matakwa ya Israeli katika muda mfupi. Tangu kundi la Hamas lishike madaraka ya serikali mwaka mmoja uliopita, halitaki kuitambua Israel. Waziri mkuu wa serikali ya Palestina, ambaye ni kiongozi wa kundi la Hamas Bw. Ismail Haniyeh tarehe 15 alisisitiza kuwa, kamwe kundi la Hamas halitaitambua Israel. Ingawa kulikuwa na habari iliyosema kuwa kundi la Hamas na kundi la Fatah la chama cha ukombozi wa taifa wa Palestina, kinachoongozwa na Abbas wamepata maendeleo hivi karibuni kwenye mazungumzo kuhusu uundaji wa serikali mpya, lakini ni vigumu kwa serikali mpya kuundwa ndani ya mwezi mmoja tu, tena hata baada ya serikali mpya kuundwa, kuweza au la kuitambua Israel bado hakuwezi kufahamika hivi sasa. Serikali ya Israel inatakiwa kutambua vizuri suala hilo, katika hali hiyo inataka serikali ya Palestina iitambue Israeli ni kama kutaka kuyawekea kikwazo mazungumzo hayo.
Aidha siku Bi Rice na Olmert walipokuwa na mazungumzo, serikali ya Israel ilitangaza kuwa itajenga nyumba 44 kwenye eneo la Maale Adumim, ambalo ni makazi ya kwanza kwa ukubwa ya wayahudi kwenye ardhi inayokaliwa ya upande wa magharibi wa mto Jordan, jambo ambalo linafanya watu kushuku udhati wa Israel wa kurejesha mazungumzo ya amani. Mpango huo unakiuka moja kwa moja mpango wa "ramani ya njia" wa amani ya mashariki unaosisitizwa mara kwa mara na Bi Rice. Kutokana na mambo ya kipindi cha kwanza cha mpango wa "ramani ya njia", ni lazima Israel isimamishe vitendo vya kujenga makazi ya wayahudi, wakati Palestina ni lazima iache kutumia nguvu za kimabavu. Mwakilishi wa kwanza wa Palestina kwenye mazungumzo, Bw Saeb Erekat alisema Israel haina budi kuchagua kati ya amani na makazi ya wayahudi, jumuiya ya amani ya huko imeikosoa kitendo cha Israel kama ni kuitemea mate usoni serikali ya Marekani.
|