Tarehe 16 waziri wa mambo ya nje wa Marekani Codoleezza Rice alifika Kuwait, kituo chake cha mwisho katika ziara yake ya Mashariki ya Kati, na alifanya mazungumzo na wajumbe wa nchi sita za Kamati ya Ushirikiano wa Nchi za Ghuba na mawaziri wa mambo ya nje wa Misri na Jordan, na kujadili masuala kuhusu hali mbaya ya usalama na namna ya kurudisha amani na utulivu nchini Iraq na kusukuma mchakato wa amani kati ya Palestina na Israel.
Bi. Codoleezza Rice alianza ziara yake ya Mashariki ya Kati kuanzia tarehe 13. Inasemekana kwamba ziara yake ina nia mbili, moja ni kutaka kusukuma mchakato wa amani kati ya Palestina na Israel, nyingine ni kuzishawishi nchi za Kiarabu ziunge mkono sera mpya za Marekani kuhusu Iraq. Lakini dalili zote zinaonesha kuwa Bi. Rice hajavuna chochote alichotaka katika ziara yake.
Kwanza, kuhusu kusukuma mchakato wa amani kati ya Palestina na Israel. Kwa sababu Condoleezza Rice hakuwa na ujanja mpya aliopewa na serikali ya Marekani kuhusu utatuzi wa mgogoro kati ya Palestina na Israel na namna ya kusukuma mchakato wa amani kati ya nchi hizo mbili, ila tu alisisitiza kusukuma mbele na kutekeleza mpango wa "ramani ya amani" uliotolewa miaka minne iliyopita, na anashikilia mpango huo utekelezwe bila kukiuka kipindi hata kimoja kikiwemo kipindi cha pili cha kuanzisha taifa la Palestina lenye mipaka ya muda na lenye dalili ya nchi yenye mamlaka. Hii ni kinyume na matakwa ya nchi nyingi za Kiarabu zinazotaka kufanya mazungumzo kuhusu kuthibitisha hadhi ya mwisho ya Palestina na Israel katika kipindi cha mwisho cha mpango huo. Kwa hiyo ziara hiyo ya Condoleezza Rice ilipuuzwa. Zaidi ya hayo, uamuzi wa Israel wa kupanua makazi ya Wayahudi kwenye ukingo wa magharibi wa mto wa Jordan uliofanywa tarehe 12 umekuwa kama maji baridi kwa Condoleezza Rice anayetaka kusukuma mbele mchakato kati ya amani ya Palestina na Israel.
Jambo ambalo Condoleezza Rice anajivunia katika ziara yake hiyo ni kufanikiwa kupanga mazungumzo kati yake na waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert, pamoja na mwenyekiti wa mamlaka ya Palestina Mahmud Abbas, lakini kama mazungumzo hayo ambayo itakuwa ni mara ya kwanza kufanyika tokea miaka sita iliyopita yataweza kufanyika au la bado ni tatizo, kwa sababu kundi la Hamas linaloshika madaraka ya serikali ya Palestina halitaki kuitambua Israel, na waziri mkuu wa Israel Bw. Olmert alisema Israel haitafanya mazungumzo yoyote na Palestina kabla ya nchi hiyo kuitambua Israel, kwa hiyo hata kama mazungumzo hayo yakifanyika, huenda hayatapata mafanikio yoyote.
Wakati Condoleezza Rice anapotangaza sera mpya za Marekani kuhusu Iraq hakupokewa kwa uchangamfu. Nchi mbalimbali za Ghuba zinaonesha wazi kwamba sera mpya za Marekani ni kichocheo cha migogoro kati ya madhehebu ya kidini nchini Iraq, na mauaji huenda yakaenea hadi kwenye sehemu nyingine za Mashariki ya Kati. Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Saud al-Faisal alisema Saudi Arabia inakubali nia ya sera mpya za Marekani za kutaka kuisaidia Iraq kupata amani, lakini ina msimamo wa tahadhari kuhusu namna ya kuifikia nia hiyo, alisema amani na utulivu nchini Iraq unategemea watu wa Iraq. Mazungumzo yaliyofanyika tarehe 16 kati ya Condoleezza Rice na Kamati ya Ushirikiano wa Nchi Sita za Ghuba na mawaziri wa mambo ya nje wa Misri na Jordan pia hayakupata mafanikio yoyote. Taarifa iliyotolewa baada ya mazungumzo hayo ilisema, inapinga nchi yoyote kuingilia kati mambo ya ndani ya Iraq.
Kwa ufupi ni kuwa ziara ya Condoleezza Rice katika Mashariki ya Kati haikupata mafanikio yoyote ya maana, haikuletea nchi za Kiarabu matumaini yoyote ya kuanzisha kipindi cha mwisho cha mpango wa ramani ya amani ya Palestina na Israel, na wala haikuondoa mashaka ya nchi za Kiarabu kwamba kweli sera mpya za Marekani kuhusu Iraq zinaweza kuisaidia Iraq kupata utulivu na kuleta amani ya Mashariki ya Kati.
Idhaa ya kiswahili 2007-01-17
|