Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-17 20:48:47    
Mkurugenzi mkuu mpya wa shirika la afya duaniani Bi. Margaret Chan

cri

Tarehe 4 mwezi Januari, Bi. Margaret Chan kutoka Hongkang, China alishika rasmi madaraka ya mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO, na amekuwa mchina mwenye wadhifa wa juu kabisa katika idara za Umoja wa Mataifa. Je Bi. Margaret Chan aliwahi kupata uzoefu na mafanikio gani ili kupata uungaji mkono wa nchi mbalimbali? Baada ya kushika wadhida huo, ataweza kuongoza vipi shirika hilo muhimu?

Bi. Margaret Chan mwenye umri wa miaka 59 alipata shahada ya udaktari ya elimu ya matibabu nchini Canada, Singapore na Uingereza, na alianza kushika wadhifa wa mkuu wa idara ya huduma za afya ya Hongkong mwaka 1994. mwaka 1997, Bi. Margaret Chan alikumbwa na changamoto kubwa kwa mara ya kwanza tangu ashike wadhifa wa mkuu wa idara hiyo.

Mwezi Mei mwaka 1997, maambukizi ya homa ya mafua ya ndege yaligunduliwa katika sehemu moja ya kufugia kuku huko Hongkong, na hilo lilikuwa ni tukio la kwanza la homa ya mafua ya ndege kugunduliwa huko Hongkong. Katika miezi kadha iliyofuata, ugonjwa huo ulienea kwa kasi, na kuku wengi walikufa. Lakini jambo lililoshangaza watu ni kwamba virusi hivyo ambavyo vilikuwa vinaambukiza ndege wa kufugwa tu vimekuwa na mabadiliko mapya na vikaweza kuambukizwa kwa wanyama wanaonyonyesha na hata binadamu. Mwezi Agosti mwaka huo, mtoto mmoja wa kiume alikufa kutokana na kuambukizwa homa ya mafua ya ndege, hilo pia lilikuwa ni tukio la kwanza ya binadamu kuambukizwa ugonjwa huo duniani.

Ili kukabiliana na ugonjwa huo mpya wa kuambukiza, Bi. Margaret Chan alichukua hatua mara moja, na kutoa amri ya kuchinjwa kuu milioni 1.6. mtaalamu mashuhuri wa matibabu Bw. Zhu Zonghan aliyewahi kufanya kazi pamoja na Bi. Margaret Chan alisema,

"yeye ni mwanamke mpole, lakini alipotoa maamuzi ya kazi hakusitasita hata kidogo. Wakati huo alifanya uamuzi wa kuchinjwa kuku wote milioni 1.6 huko Hongkong katika siku tatu. Tukio hilo lilileta mshituko mkubwa kwa jamii ya Hongkong."

Kwa kuwa hii ni mara ya kwanza kwa homa ya mafua ya ndege kuambukizwa kwa binadamu, wakati huo sekta ya matibabu ya Hongkong haikukuwa na uzoefu hata kidogo kuhusu hali hiyo, Bi. Margaret Chan alifanya uamuzi huo mara moja na kufanikiwa kudhibiti hali ya maambukizi ya ugonjwa huo huko Hongkong. Baada ya hapo, hatua hiyo imekuwa mbinu muhimu katika kudhibiti maambukizi ya homa ya mafua ya ndege kote duniani.

Wakati homa ya mafua ya ndege ilipolipuka mwaka 2003, Bi. Margaret Chan alikabiliana na chamgamoto nyingine. kila mara alipokabiliwa na maswali magumu kutoka kwa waandishi wa habari, aliwajibu kwa uthabiti. Alisema:

"tunafuata njia hii kwa pamoja, tunapaswa kuwafahamisha kuhusu matatizo yetu na changamoto tunayokabiliana nayo. Kwa kweli, tulikabiliwa na shinikizo kubwa. Mimi sipendi kuficha ukweli wa mambo, niliwaambia wakazi kama nilivyojua, na kama sijui niliwaambia sijui."

Bi. Margaret Chan aliwahi kuwa daktari, alipoona kuwa watumishi wa matibabu walifariki kutokana na kuambukizwa virusi vya SARS, alitokwa na machozi. hii inaonesha tena upole wake. Katika mapambano ya dharura dhidi ya SARS, Bi. Margaret Chan alionesha kikamilifu uzoefu na maarifa yake ya matibabu, pamoja na uvumilivu na ushujaa.

Uwezo wa Bi. Margaret Chan umesifiwa na shirika la afya duniani WHO. Mwezi Agosti mwaka 2003, aliteuliwa kuwa mkurugenzi mkuu wa hifadhi ya mazingira ya binadamu katika shirika la afya duniani, baadaye alihamishwa kuwa msaidizi wa mkurugenzi mkuu anayashguhulikia mambo ya magonjwa ya kuambukiza. Katika muda wa miaka mitatu alipofanya kazi katika shirika hilo, Bi. Margaret Chan alifanikiwa kuongeza idadi ya nchi zilizoweka mpango wa kukabiliana na maambukizi ya homa ya mafua ya ndege kufikia zaidi ya 170 kutoka 50, pia alihimiza nchi za China, Thailand, Vietnam na Mexico kuendeleza teknolojia ya kinga dhidi ya magonjwa, pia alifanikiwa kushawishi kiwanda cha kutengeneza dawa cha F. Hoffmann-La Roche cha Uswiss kuchangia vidonge vya dawa za mafua zaidi ya milioni 20 kwa nchi 20 zilizo nyuma kiuchumi, na kutoa mchango mkubwa kwa udhibiti wa maambukizi ya magonjwa katika nchi hizo.

Mwezi Mei mwaka 2006, mkurugenzi mkuu wa zamani wa shirika la afya duniani WHO Lee Jong-Wook alifariki dunia ghafla kutokana na tatizo la mishipa ya damu ya kwenye ubongo, shirika hilo liliamua kuchagua mkurugenzi mkuu mpya katika mwezi Novemba mwaka huo, Bi. Margaret Chan mwenye uzoefu wa shughuli za matibabu kwa miaka 30 alipendekezwa na serikali ya China kugombea wadhifa huo. Na Hatimaye alijitokeza kati ya wagombea 13 na kuchaguliwa kuwa mkurugenzi kuu wa shirika la afya duniani, kipindi cha madaraka yake kitaendelea hadi mwezi Juni mwaka 2012.

Shirika la afya duniani lililoanzishwa mwezi Aprili mwaka 1948 ni idara maalum inayoshughulikia mambo ya afya katika Umoja wa Mataifa. Majukumu ya shirika hilo ni pamoja na kuhimiza kinga na tiba za magonjwa ya kuambukiza, kutoa na kuboresha mafunzo na mazoezi kuhusu afya ya umma, matibabu ya magonjwa na shughuli nyingine husika. Lakini hivi sasa shirika hilo bado linakabiliwa na changamoto nyingi. Naibu mkurugenzi mkuu wa zamani wa shirika hilo alisema:

"changamoto zinazolikabili shirika la afya duniani ni ngumu na kubwa. Bado kuna magonjwa mengi ya kuambukizwa ambayo hayajadhibitiwa, na magonjwa mengi mapya yanaendelea kutokea. Mbali na haya, magonjwa mengi yasiyo ya kuambukiza yanatokea mara kwa mara."

Aidha, namna ya kuzisaidia nchi zilizo nyuma kiuchumi kuinua kiwango cha afya ya wananchi wake, na kuhimiza nchi zilizoendelea kuongeza misaada kwa nchi zinazoendelea, yote ni masuala yanayopaswa kufuatiliwa na shirika la afya duniani.

Bi. Margaret Chan alisema, atashikilia kanuni ya haki, usawa na kutopendelea upande wowote kuhudumia nchi wanachama 193 wa shirika hilo kwa ajili ya afya ya binadamu duniani. Alipofafanua sera za uongozi wake, alisema kuwa jukumu lake muhimu ni kuboresha hali ya afya ya umma barani Afrika na hali ya afya kwa watoto na wanawake kote duniani. Alisema:

"bara la Afrika linaathiriwa vibaya zaidi na magonjwa mbalimbali kote duniani. Hivyo kama sitaweka mkazo katika afya ya watu wa Afrika, afya ya watoto na wanawake kote duniani, nitashindwa kushiklia barabara vigezo vya kutathmini ufanisi wa kazi za shirika la afya duniani."

Bi. Margaret Chan pia alisema hatafanya marekebisho makubwa ya miundo ya shirika hilo katika muda mfupi, bali atajitahidi kuhimiza idara mbalimbali za shirika hilo ziweze kushirikana kwa pamoja. Mageuzi ya miundo ya shirika hilo yatakuwa tulivu na yenye nguvu.