Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-18 14:46:24    
Wazee wanastahili maisha ya raha mustarehe

cri

China ni nchi yenye watu bilioni 1.3, na ni moja kati ya nchi ambazo idadi ya wazee inaongezeka kwa kasi. Hivi sasa wananchi wa China wenye umri wa zaidi ya miaka 60 wamefikia watu milioni 144, idadi ambayo ni nusu ya wazee wa bara zima la Asia. Inakadiriwa kuwa hadi kufikia mwaka 2020, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kwa watu milioni 100. Namna ya kuwahakikisha wazee waishi kwa raha mustarehe ni suala linalofuatiliwa na jamii ya China.

Nchini China, sambamba na kuongezeka kwa idadi ya wazee, tatizo la ajira pia lipo, hali ambayo inaleta matokeo kwamba, inawabidi wazee wengi waishi peke yao, kwani watoto wanatingwa na kazi na wanakosa nafasi ya kuwatunza wazazi wao. Lakini kuzeeka sana kunawafanya baadhi ya wazee washindwe kujitegemea. Kutokana na hali hii, wazee wengi wa China wanaishi kwenye vituo mbalimbali vya kutunza wazee.

Mliyosikia ni rekodi ya mazungumzo kati ya Bibi Zheng Xuelan na mzee mmoja. Bibi Zheng ni mkuu wa kituo cha kuwatunza wazee cha mji wa Shangrao, mkoani Jiangxi, katikati ya China. Kwenye rekodi hiyo alikuwa akijifunza kilugha cha mkoa wa Zhejiang, ambapo ni makazi ya mzee huyo. Mzee huyo alihamia kwenye kituo hicho mwezi mmoja uliopita, ana ugonjwa wa akili. Ana hali mbaya na kupenda kupiga kelele na kukasirika. Ili kuwasiliana na mzee huyo, Bibi Zheng alimwomba amfundishe kilugha chake, na hatua kwa hatua akapata uaminifu na upendo wa mzee huyo.

Katika kipindi cha miaka 17 iliyopita, wazee zaidi ya 300 walikuwa wanaishi kwa raha mustarehe kwenye kituo hicho cha kuwatunza wazee. Hivi karibuni usiku wa siku moja ya majira ya siku za baridi, mzee Yang Yitang mwenye umri wa miaka 95 kabla ya kufariki kwake, alieleza kutaka kula tikiti maji. Bibi Zheng aliyekuwa akimtunza alipanda baiskeli kwenda kwenye mji wa wilaya uliopo mbali kwa kilomita zaidi ya 20 kununua tikiti maji kwa ajili ya mzee huyo. Bibi Zheng alisema "Nimejikita kwenye shughuli za kuwatunza wazee. Kitu kinachonivutia ni tabasamu za wazee. Wazee wanafurahi, mimi pia nafurahi."

Kuna vituo vya namna hii elfu 40 hivi vya kuwatunza wazee kote nchini China, ambavyo vina vitanda vipatavyo milioni 1 na laki 5. Hata hivyo ikilinganishwa na idadi ya jumla ya wazee wa China wapatao milioni 144, vituo hivi havitoshi. Wazee wengi wanaishi katika nyumba zao, ambapo wanandoa wazee wawili wanasaidiana na endapo mmoja amefariki dunia, mwingine anaishi peke yake akiwa na upweke.

Mama Zhang Yusheng mwenye umri wa miaka 79 anaishi mjini Shijiazhuang, kaskazini mwa China. Mume wake alifariki dunia miaka zaidi ya 10 iliyopita, mama huyo amekuwa akiishi peke yake. Hivi sasa kutokana na umri mkubwa, ana matatizo ya miguu, ni vigumu kwake kufanya shughuli mbalimbali.

Kuanzia mwaka jana, katika mtaa wa makazi anakoishi mama Zhang, kilianzishwa kituo cha kuwahudumia wazee kiitwacho Yiyangyuan, ambacho kinawasaidia wazee katika shughuli mbalimbali kama vile kununua chakula na dawa. Mama Zhang amenufaika sana na kituo hicho. Alisema  "Sasa nasaidiwa na Yiyangyuan, ni pazuri na pa safi sana. Sasa kila kitu ni shwari."

Huu ni mtindo mpya wa kuwatunza wazee katika nyumba zao, hivi sasa mtindo huo unaenezwa katika miji mbalimbali ya China. Mtindo huo unawahusu wazee wanaoishi peke yao ambao kimsingi wanaweza kujitunza, lakini wanapaswa kusaidiwa na wengine. Wazee wanalipa kiasi kidogo cha fedha kila mwezi, wanapata huduma mbalimbali zikiwemo kununua mahitaji ya kila siku na dawa, kuwapima shinikizo la damu na kuwatembelea kila baada ya siku kadhaa. Zaidi ya hayo, katika baadhi ya mitaa ya makazi, huduma nyingine zinatolewa kukidhi mahitaji yanayolingana na hali halisi, huduma hizo ni pamoja na kuwatibu na kuwahudumia wazee waliofanyiwa upasuaji, huduma ya wauguzi nyumbani na kuwatunza wazee wanaokaribia kufariki dunia.

Bibi Cao Yuke ni mwanzilishi wa kituo cha kuwahudumia wazee cha Yiyangyuan, alieleza maoni yake kuwa, kwa kushirikisha juhudi za serikali, jamii na viwanda, kazi ya kuwatunza wazee ina mustakabali mzuri. Alisema "Inapaswa kutoa huduma zinazokidhi matakwa ya wazee wengi. Vile vile inapaswa kutoa huduma zinazowalenga wazee wenye umri tofauti na matakwa tofauti. Kazi hiyo inaungwa mkono na serikali, inakusanya nguvu za watu binafsi na viwanda vinavyohiari kutoa ufadhili, kila upande unatoa mchango wake, kwa hiyo kazi ya kuwatunza wazee itaendelezwa siku hadi siku."

Maisha ya raha mustarehe si kama tu yanahusu chakula, bali pia yanahusu afya ya kisaikolojia. Pamoja na matatizo mbalimbali yanayosababishwa na uzee, wazee pia wanakabiliwa na tatizo la kisaikolojia, hususan wazee ambao waume au wake zao walishafariki dunia, wanasumbuliwa na upweke na hofu ya kifo. Wiki ijayo katika kipindi hiki tutawaletea makala kuhusu namna ya kuwasaidia wazee kutatua tatizo la kisaikolojia.

Idhaa ya kiswahili 2007-01-18