Tarehe 12 Jumanne ilikuwa ni "siku ya mkosi" kwa waziri mkuu Ehud Olmert wa Israel, kwani siku hiyo jioni kamanda mkuu wa jeshi la Israel Bw. Dan Halutz alitangaza kujiuzulu, ambaye ni ofisa wa ngazi ya juu kabisa aliyejiuzulu kutokana na mgogoro uliotokea kati ya Israel na Lebanon katika majira ya joto mwaka jana, kisha watu wengi wa Israel walitaka Olmert na waziri wa ulinzi Amir Peretz pia wajiuzulu. Waziri huyo anakabiliwa shinikizo kubwa la kisiasa.
Bw. Halutz alijiuzulu kutokana na kushinikizwa na hali ambayo raia wa Israel wamekuwa wakizidi kuwalalamikia viongozi wa serikali na jeshi. Baada ya mgogoro kati ya Israel na Lebanon kumalizika mwezi Agosti mwaka jana, jeshi la Israel lilishindwa kuwaokoa askari wake waliotekwa nyara na kuvisambaratisha vikosi vya Hezbollah, watu wa Israel wanaona kuwa jeshi la Israel lilishindwa katika vita hivyo na wakaanza kuwalalamikia waziri wa ulinzi Peretz na waziri mkuu Olmert.
Kutokana na kushinikizwa na malalamiko mengi ya watu wa Israel, serikali ya Bw. Olmert iliunda tume ya uchunguzi kuhusu uongozi wa kijeshi na kiserikali katika vita dhidi ya Lebanon. Hivi sasa uchunguzi umekamilika, na tume hiyo kimsingi inaona kuwa uongozi wa kijeshi ulikuwa haufai katika vita hivyo. Kwenye barua ya kujiuzulu Bw. Halutz alisema amemaliza jukumu lake baada ya vita kumalizika yaani kupata mafunzo kutoka vita hivyo, na sasa anataka kujiuzulu ili "kuwajibika". Baada ya kupata barua ya kujiuzulu kwa Halutz, Bw. Olmert alitoa taarifa akisikitishwa na kujiuluzu kwa Olmert. Alisema, aliwahi kujaribu kumtaka abaki madarakani lakini alikataa, na atajadilianana na idara husika na kuamua kamanda mkuu mpya.
Vyombo vya habari vimesema tukio hilo ni kama "tetemeko la ardhi" kwa waziri mkuu Olmert. Gazeti la Jioni la Israel lilisema, "Bw. Halutz amejiuzulu, waziri wa ulinzi ameacha ufunguo, Bw. Olmert je? Tuone watu watasemaje." Redio ya Israel katika siku hiyo pia ilitangaza kuwa tukio hilo huenda likasababisha matukio mfululizo ya kujiuzulu kwa Amir Peretz na Olmert.
Wabunge wa vyama vya upinzani wanataka moja kwa moja Bw. Olmert ajiuzulu, mbunge wa mrengo wa kulia la chama cha Likud Yisrael Katz alisema, kujiuzulu kwa Halutz kumethibitisha kuwa Israel imeshindwa katika mgogoro kati ya Israel na Lebanon, waziri mkuu na waziri wa ulinzi ni lazima wajiuzulu. Mbunge wa mrengo wa kushoto wa chama cha Meretz Bw. Zahava Gal-On alisema haifai kufuatilia tu majukumu ya jeshi tu, viongozi wa serikali pia ni lazima wawajibike kutokana na maamuzi mabaya.
Kujiuzulu kwa Bw. Halutz ni kama "msumari wa moto kwenye kidonda". Saa chache kabla ya kujiuzulu kwa Halutz polisi ilitangaza kuwa itafanya uchunguzi kuhusu kitendo cha kukiuka sheria. Bw. Olmert alishukiwa kumsaidia rafiki yake kupata faida kupitia kununua hisa za benki wakati Benki ya Wananchi ya Israel ilipobinafsishwa mwaka 2005. Kabla ya hapo habari kuhusu ufisadi wa Olmert pia ziliwahi kutangazwa mara kadhaa.
Kutokana na ufisafi wake na tukio la kujiuzulu kwa Halutz, kiasi cha uungaji mkono kimeshuka haraka hadi kufikia 14%, na nusu ya watu walioulizwa maoni yao wanaona Olmert ni lazima ajiuzulu, na 85% ya watu hao wanaona kuna ufisadi mkubwa katika ngazi ya juu ya serikali. Pamoja na hayo, kiasi cha uungaji mkono kwa chama cha Kadima cha Bw. Olmert pia umeshuka na chama cha Likud kimepata kiasi kikubwa cha uungaji mkono. Uchunguzi wa maoni ya raia unaonesha kuwa kama uchaguzi mkuu ukifanyika hivi sasa chama cha Likud kitapata viti mara tatu kuliko sasa na kitakuwa chama tawala.
Wachambuzi wanaona kuwa ingawa shinikizo ni kubwa lakini Olmert hatajiuzulu katika muda mfupi ujao, na kama akijiuzulu raia wa Israel watashindwa kupata kiongozi mwingine ambaye anafaa zaidi kuwa waziri mkuu kuliko Bw. Olmert. Ni dhahiri kwamba serikali ya Bw. Olmert itakabiliwa na matatizo mengi. Mtaalamu wa kisiasa wa Israel Bw. Ephraim Imbar alisema, haijafahamika ni vipi serikali inaweza kupita salama kipindi hicho, lakini tukio la kujiuzulu kwa Bw. Halutz ni dalili ya mwanzo wa msukosuko wa kisiasa nchini Israel.
Idhaa ya kiswahili 2007-01-18
|