Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-19 19:12:35    
Mazungumzo ya pande sita kuhusu suala la nyuklia ya peninsula ya Korea yatarajiwa kurudishwa

cri

Mkutano kati ya viongozi wa ujumbe wa Marekani na Korea ya Kaskazini ulioshiriki kwenye mazungumzo ya pande 6 kuhusu suala la nyuklia ya peninsula ya Korea, ulimalizika tarehe 18 huko Berlin, nchini Ujerumani. Hapo baadaye kiongozi wa ujumbe wa Marekani ambaye pia ni msaidizi wa waziri wa mambo ya nje Bw. Christopher Hill alielekea ziarani nchini Korea ya Kusini, China na Japan kuziarifu nchi hizo tatu maendeleo ya mkutano huo na kusawazisha misimamo yao. Wachambuzi wamesema hii ni ishara kwamba mazungumzo ya pande 6 yanatarajiwa kurudishwa hivi karibuni.

Mkutano huo wa siku tatu ulianza tarehe 16. Inasemekana kuwa mkutano huo ulifanyika kutokana na matakwa ya Korea ya Kaskazini. Marekani ilisisitiza kuwa mkutano ulifanyika ili mazungumzo ya pande 6 yarudishwe na kupata maendeleo. Mjumbe wa Marekani Bw. Hill alisema mkutano huo umeleta manufaa na maendeleo, na kutumai mazungumzo ya pande 6 yatarudishwa mwishoni mwa mwezi huu. Tarehe 17 Bw. Hill alitoa ripoti kuhusu mkutano huo kwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bibi Condoleezza Rice ambaye yuko ziarani nchini Ujerumani huko Berlin, ambapo Bibi Rice alieleza kuwa mkutano huo kati ya Marekani na Korea ya Kaskazini unasaidia kuandaa mazingira mazuri ya kurudishwa kwa mazungumzo ya pande 6.

Wachambuzi wamekubaliana kuwa, duru la tano la mazungumzo ya pande 6 yaliyofanyika mwezi Desemba mwaka jana kushindwa kupata maendeleo halisi, kunatokana na tofauti kubwa kati ya Korea ya Kaskazini na Marekani katika hatua halisi za kutekeleza taarifa ya pamoja na vikwazo vya fedha vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Korea ya Kaskazini. Katika mkutano huo uliofanyika mjini Berlin, mjumbe wa Korea ya Kaskazini Bw. Kim Kye-Gwan alisema Korea ya Kaskazini haitafikiria kuacha mpango wa nyuklia bila Marekani kuondoa vikwazo vya fedha dhidi yake. Aliongeza kuwa atawasilisha pendekezo lililotolewa na Marekani katika mkutano huo kwa viongozi wa Korea ya Kaskazini. Kutokana na kauli hizo, wachambuzi kadhaa wanasema kwenye mkutano huo wa Berlin, Korea ya Kaskazini na Marekani kila upande ulikuwa ukijaribu kupima matakwa ya kimsingi ya upande mwingine. Lakini baadhi ya wachambuzi wa Korea ya Kusini walikuwa na matumaini na mkutano huo wa Berlin, wakiona ulipata maendeleo makubwa na kuondoa vizuizi vya kurudishwa mapema kwa mazungumzo ya pande 6.

Marekani na Korea ya Kaskazini hazitaki kuzungumzia mambo halisi ya mkutano huo. Hata hivyo imedokezwa kuwa, katika mkutano huo pande hizo mbili zilijadili hatua za mwanzo za kutekeleza taarifa ya pamoja iliyokubalika kwenye mazungumzo ya pande 6, na huenda Korea ya Kaskazini ilitoa majibu kwa pendekezo lililotolewa na Marekani katika mazungumzo ya pande 6 yaliyofanyika hapa Beijing mwezi Desemba mwaka jana. Kwa mujibu wa pendekezo hilo, endapo Korea ya Kaskazini itaacha mpango wa nyuklia, Marekani itaipa uhakikisho wa usalama na itaweza kurejesha uhusiano wa kawaida na Korea ya Kaskazini.

Vyombo vya habari kadhaa vilitoa maelezo kuwa, Marekani ilikubali kuondoa sehemu ya vikwazo vya fedha dhidi ya Korea ya Kaskazini. Lakini msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Tom Casey alisema suala la vikwazo vya fedha si kati ya masuala yaliyozungumzwa sana kwenye mkutano wa Berlin. Alisema suala hilo ni suala la kisheria tu, Marekani haitabadili sheria au sera zake kwa sababu ya suala hilo.