Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-23 19:05:47    
Mkutano wa mwaka wa Baraza la uchumi duniani kufanyika Uswisi

cri

Mkutano wa 37 wa mwaka wa Baraza la uchumi duniani unatazamiwa kufanyika tarehe 24 hadi 28 huko Davos, Uswisi. Kauli mbiu ya mkutano huo ni "Miundo ya nguvu katika mabadiliko", ambapo viongozi wa serikali na wataalamu wa uchumi wapatao zaidi ya 2400 kutoka nchi na sehemu zaidi ya 90 duniani watajadili kwa kina mabadiliko mapya ya uchumi duniani na kutafuta uvumbuzi wa masuala yanayohusika.

Mkutano wa mwaka wa Davos wa Baraza la uchumi duniani umesifiwa kuwa ni mkutano wa ngazi ya juu kabisa usio wa kiserikali kuhusu uchumi duniani. Mkutano huo kila mwaka huweka kauli mbiu moja ili kuonesha umaalum mkubwa kabisa na hali mpya katika uchumi duniani. Mwanzilishi wa Baraza la uchumi duniani Bwana Klaus Schwab alisema, hivi sasa mabadiliko yanatokea katika nyanja nyingi za kiuchumi duniani na mambo mapya yamejitokeza ambayo hayakutokea hapo kabla katika uchumi duniani. Alisema hivi sasa baadhi ya watu wamepuuza matatizo mengi yaliyojificha na wanaona tu mambo ya uchumi duniani yanaongezeka.

Mkutano huo wa mwaka pia umewekwa kauli mbiu nyingine 4 kuhusu uchumi, siasa ya kijiografia, teknolojia na jamii na viwanda na makampuni. Ofisa wa Baraza la uchumi duniani alisema, uchumi wa dunia unahitaji nguvu mpya na waongozaji. Marekani ikiwa nguzo moja kubwa kabisa katika mambo ya uchumi duniani, maendeleo yasiyo ya uwiano ya uchumi wake na pengo lake kubwa sana la kifedha, yanawafanya watu wawe na wasiwasi kama uchumi wa Marekani utadumisha ongezeko endelevu au la; na kuongezeka kwa thamani ya Euro kumepunguza uuzaji wa bidhaa wa sehemu zinazotumia Euro, hivyo athari yake kwa uchumi wa dunia pia inaonekana siku hadi siku. Zaidi ya hayo hatari kwenye sekta ya fedha pia haipaswi kupuuzwa. Kuhusu siasa ya kijiografia, Baraza la uchumi duniani limeona kuwa, sehemu ya mashariki ya kati, hasa hali wasiwasi ya Iraq, kuenea kwa silaha kali, nishati duniani pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa, yote hayo yanahusiana sana na mambo ya uchumi, hata yamekuwa tishio na changamoto dhidi ya uchumi duniani, pia yameonesha kuwa siasa ya dunia inahitaji nguvu mpya ya uongozi. Lakini katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na maendeleo makubwa ya teknolojia ya mtandao wa Internet, kila mtu anaweza kupata habari duniani kwa muda mfupi, hivyo mabadiliko hayo mapya yanaweza kuleta athari kubwa na ya mbali kwa njia ya usimamizi wa viwanda na makampuni na biashara.

Habari zinasema wakati wa mkutano huo wa mwaka wa Baraza la uchumi duniani, makongamano zaidi ya 200 kuhusu mada maalum mbalimbali zinazohusu uchumi na jamii yatafanyika. Na mada tatu kubwa ni kuhusu hali ya mashariki ya kati, mchakato wa mazungumzo ya raundi ya Doha pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa kuongezeka kuwa joto kote duniani. Mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw Mahmoud Abbas, mfalme Abdullah wa Jordan, waziri mkuu wa Lebanon Fouad Siniora, naibu waziri mkuu wa Israel Shimon Peres na wengineo kutoka sehemu ya mashariki ya kati watakuwa na mazungumzo ili kutafuta njia ya kuvunja hali ya mvutano ya mashariki ya kati. Na katibu mkuu wa Shirika la biashara duniani Bw Pascal Lamy alipendekeza kuitisha mkutano utakaohudhuriwa na mawaziri zaidi ya 30 ili kutafuta njia ya kuanzisha upya mazungumzo ya Doha. Katibu mkuu mtendaji wa Baraza la uchumi duniani anayeshughulikia mambo ya kikanda Bw. Peter Torreele alifahamisha kuwa, viongozi watakaohudhuria mkutano wa mwaka wa Baraza la uchumi duniani wengi wao watazingatia na kujadili kwanza mada kuhusu hali ya hewa kubadilika kuwa joto kote duniani. Aidha wakuu wa nchi au wa serikali zaidi ya 20 pia watahudhuria mkutano huo.

Idhaa ya Kiswahili 2007-01-23